UJUE UGONJWA WA KUKOJOA DAMU (HAEMATURIA)

HAEMATURIA ni ugonjwa wa kukojoa damu ambapo kwenye mkojo kunakuwepo chembechembe za damu nyekundu (Red blood cells).
Kukojoa damu ni dalili ya kuonyesha kuwa mtu anayekojoa ana magonjwa katika mfumo wa mkojo kama vile magonjwa ya kichocho au magonjwa mengine yanayoshambulia kibofu cha mkojo au kwenye figo.

SABABU
Magonjwa yanayoshambulia mfumo wa mkojo kama vile UTI, magonjwa ya zinaa hasa kwa wanawake, vijidudu kama staphylococcus saprophyticus, mawe kwenye figo (kidney stone) kuvimba kwa tezi zinazozalisha manii kwa wanaume ambao umri  umeenda yaani wazee.
Sababu nyingine ni kama kupata ajali na kuumia sehemu za mfumo wa mkojo (trauma), kupata magonjwa kama kansa  ya kibofu cha mkojo, hii hutokea  mara nyingi hasa  vijijini  ambapo watu wanacheza au kuogelea kwenye madimbwi ya maji yasiyotembea.
Sababu zingine  ni mtu kuugua magonjwa ya sickle cell anemia na magonjwa mengine  ya figo kama vile nephotic syndrome na mengine mengi ambayo yanajulikana kwa kitaalamu na siyo rahisi kuyafafanua kwa Kiswahili.

AINA YA UGONJWA WA KUKOJOA DAMU
Kuna aina mbili za damu kutoka  kwenye mkojo, moja ni ile ambayo damu huchuruzika  na kuonekana vizuri kwenye mkojo. Hii hujulikana  kama macroscopic haematuria au gross haematuria ambayo hutokea kwa wagonjwa  wa kichocho au waliopata ajali.
Nyingine ni ile inayoonekana kwa mbali  na mara  nyingine huonekana wakati mgonjwa anapopimwa mkojo, aina hii hujulikana  kama microscopic haematuria.
JINSI YA KUGUNDUA TATIZO (diagnosis)
Mara nyingi tatizo la kukojoa damu hugundulika baada ya mgonjwa kwenda  hospitalini na kuonana na  daktari  na akachukua maelezo yake vizuri na kuagiza mgonjwa akapime mkojo.
Kipimo cha Ultrasound pia  husaidia kujua tatizo linalosababisha mgonjwa akojoe  damu.
Mashine ya X- ray husaidia  kugundua kama mgonjwa  ana mawe kwenye figo. Kipimo kingine  cha kisasa  ni CT scan hiki kina uhakika ila ni ghali sana na hupatikana kwenye hospitali kubwa.

TIBA
Tiba ya uhakika  ni kujua sababu inayosababisha mgonjwa akojoe damu kama ni kichocho basi  mgonjwa atapewa dawa ya kichocho na kama ni UTI mgonjwa atapewa dawa husika na kama ni magonjwa ya zinaa nayo yatatibiwa. Magonjwa mengine ni kama yale ya figo basi nayo yakigundulika yatatibiwa.

USHAURI
Watoto wasichezee maji yaliyosimama hasa kwenye mabwawa vijijini na mijini, wakigundulika kuwa walicheza basi haraka wapelekwe hospitali kupimwa.
Post a Comment
Powered by Blogger.