FAHAMU NAMNA YA KUVURUGIKA KWA MZUNGUKO WA HEDHI

Mzunguko wa hedhi umegawanyika katika maeneo makuu mawili. Kuna ule unaopevusha mayai ‘Ovulatory Cycle’ na usiopevusha mayai ‘Anovulatory Cycle’. Aina hizi za mizunguko tutakuja kuziona kwa undani katika makala zijazo, lakini mzunguko unaopevusha mayai mwanamke anapata ute wa uzazi ambao unavutika na anaweza kupata ujauzito.
Mzunguko usiopevusha mayai mwanamke hawezi kupata ujauzito ingawa katika  mizunguko yote hiyo miwili mwanamke anapata damu ya hedhi kama kawaida. Mwanamke ambaye mzunguko wake hapati ute wa uzazi, hawezi kupata ujauzito. Hii inatokana na mabadiliko katika mfumo wake wa homoni.
Ute wa uzazi umegawanyika katika makundi matatu. Ute mwepesi, ute unaovutika na ute mzito.
Mwanamke asiyepevusha mayai hawezi kupata ujauzito, hivyo hapati ute wa uzazi wengine hupata ute mzito daima kama uchafu fulani mzito unaotoka ukeni ambao hauna harufu wala muwasho.
Tunaposema kuvurugika kwa mzunguko inamaanisha mwanamke hapati siku zake katika utaratibu unaoeleweka.
Wengine hawajui lini wanaingia, hapa kitu cha msingi lazima ujifahamu kwanza.
Jinsi ya kutambua mzunguko
Mzunguko wa hedhi uwe unapevusha mayai au haupevushi umegawanyika katika mizunguko midogo mitatu. Kuna mzunguko mfupi, mrefu na wa kawaida. Mzunguko mfupi ni kati ya siku 22 hadi 27, mzunguko wa kawaida ni kati ya siku 28 hadi 30.
Mzunguko mrefu ni kati ya siku 31 hadi 35.
Kila mwanamke ana mzunguko wake. Katika  makala zijazo tutaelezea kwa undani jinsi ya kuhesabu na kujua mzunguko wako ni upi.
Kuna faida nyingi za kufahamu vizuri mzunguko wa hedhi, unasaidia kupanga uzazi na kuepuka kutumia dawa za kupanga uzazi ambazo wengine huwaathiri kiafya, unasaidia pia kupangilia jinsia ya mtoto unayeweza kumpata, kama unataka kuchagua kupata mtoto wa kike au wa kiume.
Ili kufahamu mzunguko wako ukoje ni vema ukatumia kalenda na ukahesabu siku za kwanza ni ile unayoona damu na siku ya mwisho ni siku moja kabla hujaona damu kwa mwezi unaofuata. Mfano, damu kwa mwezi uliopita umeona tarehe 3 na mwezi huu uneona tarehe kumi, unahesabu kuanzia tarehe 3 mwezi uliopita hadi tarehe tisa mwezi huu, mengine tutakuja kuelimishana zaidi.
Chanzo cha kuvurugika
Kuvurugika kwa mzunguko wa hedhi kunaweza kusababishwa na matatizo ya kisaikolojia mfano mshtuko, hofu, wasiwasi au kuwa na hamu ya kupata ujauzito. Mwanamke mwenye hamu sana ya kupata mimba anaweza akajikuta anapata siku zake au anakosa lakini hana mimba, pia anayehofia kupata mimba anajikuta anapitiliza siku zake lakini hana mimba.
Chanzo kingine ni mabadiliko ya kimwili, hii  inatokana na  kubadilisha hali ya hewa, matumizi ya baadhi ya madawa hasa dawa za homoni, mfano vidonge na sindano za homoni, mfano vidonge na sindano za kupanga uzazi, baadhi ya dawa za tiba.
Magonjwa pia yanaweza kuleta mabadiliko mwilini, mfano magonjwa au matatizo katika mfumo wa uzazi.
Magonjwa sugu yanayoweza kuathiri mfumo wa homoni mwilini mfano maambukizi ya HIV, uvimbe ndani  ya kizazi, kisukari na mengine mengi.
Dalili za tatizo
Mwanamke ambaye mzunguko wake haueleweki hawezi kupata ujauzito au atapata ujauzito bila ya kutarajia hali hii husababisha siku zisitokee kwa mpangilio,  mengine hulalamika maumivu ya tumbo chini ya kitovu au maumivu makali wakati wa hedhi.
Hali ya kuvurugika kwa mzunguko wa  hedhi huambatana na  uwepo wa matatizo mengine ya uzazi, damu inaweza kutoka nyingi au kidogo kidogo kwa muda  mfupi au mrefu.
Uchunguzi
Hufanyika katika kliniki za madaktari bingwa wa magonjwa ya kinamama katika hospitali za mikoa. Vipimo mbalimbali vitafanyika kama  Ultrasound, damu  kuangalia mfumo wa homoni na mengine ambayo daktari ataona  inafaa.
Ushauri
Endapo utahisi hali isiyo ya kawaida ukeni au katika mfumo wa uzazi, basi ni vema  uwahi hospitali kwa uchunguzi na tiba. Athari za matatizo haya ya uzazi ni kupoteza uwezo wa kuzaa.

IMEANDALIWA NA DOCTOR JOH BLOG
Post a Comment
Powered by Blogger.