Korosho zawapandisha kizimbani watu saba

Watu saba akiwamo raia wa Zambia wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matatu ya kula njama, wizi na utakatishaji fedha kiasi cha Sh120.5 milioni.
Akiwasomea hati ya mashtaka inayowakabili leo Jumatano Machi 7, 2018 wakili wa Serikali, Mwanaamina Kombakono mbele ya hakimu mkazi mkuu, Huruma Shaidi amewataja washtakiwa hao kuwa ni Robert Silaa (26) ambaye ni wakala wa usafirishaji.
Wengine ni Isihaka Ngubi (25) ambaye ni dereva, Cathbeth Mlugu (35) mlinzi wa Zambia Cargo and Logistic Ltd; Mrisho Mindu; Giften John (32); Maulid Said (40) wote makarani; Kirby Ng'andu ambaye ni meneja mwendeshaji wa kampuni ya Zambia Cargo and Logistic Ltd.
Wakili Kombakono amedai kuwa kati ya Januari mosi na Februari 6, 2018 katika kampuni ya Zambia Cargo and Logistic Ltd iliyopo Dar es Salaam, washtakiwa hao walikula njama ya kutenda kosa la wizi.
Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa katika kipindi hicho, waliiba katoni 700 za korosho zilizobanguliwa zenye thamani ya dola 54,180 za Marekani (zaidi ya Sh120.5 milioni) mali ya Barabara Trading Tanzania Limited.
Iliendea kudaiwa katika shtaka la utakatishaji fedha, walijihusisha moja kwa moja na muamala wa katoni 700 za korosho zilizobanguliwa zenye thamani ya Sh120,563,909.55 wakati wakijua mali hiyo ilikuwa ni zao la wizi.
Baada ya washtakiwa kusomewa mashtaka hayo yanayowakabili, wote walikana na upande wa mashtaka alidai kuwa upelelezi haujakamilika.
Washtakiwa walipelekwa rumande kwa sababu shtaka la utakatishaji wa fedha kwa mujibu wa sheria halina dhamana.
Kesi imeahirishwa hadi Machi 9,2018 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.

Chanzo: Mwananchi
Post a Comment
Powered by Blogger.