JINSI YA KUJUA KAMA UNA UPUNGUFU WA MAJI MWILINI

Umeshawahi kwenda hospitali kumlalamikia daktari kuwa mwili wako hauna nguvu na unajisikia kuchokachoka sana na baada ya kukuchunguza, akakwambia huna tatizo lolote isipokuwa una upungufu wa maji mwilini tu? 

Mwili kuishiwa nguvu huwa ni miongoni mwa dalili za upungufu wa maji mwilini na chanzo kikiwa ni wewe mwenyewe kutopenda kunywa maji. Ni kawaida kwa baadhi ya watu kutokunywa maji hadi pale wanaposikia kiu.

Katika makala ya leo, nitakujuza dalili za mwili kuishiwa maji ambazo hujitokeza na kukuhimiza kunywa maji hata kabla hujasikia kiu. Uonapo dalili hizo, hupaswi kuzipuuzia bali kunywa maji kwa wingi tena haraka.

UPUNGUFU WA MAJI MWILINI NI NINI?

Pale mwili unapopoteza kiasi kingi cha maji kwa njia mbalimbali, ikiwemo jasho na mkojo, mwili hupungukiwa maji na hivyo mtu huyo huambiwa ana upungufu wa maji. Tunaelezwa kuwa karibu theluthi mbili ya miili yetu imejaa maji.

Ili mwili uweze kufanya kazi yake vizuri, kiwango cha maji mwilini hakipaswi kupungua hata kidogo, hivyo kila mtu ana wajibu wa kunywa maji ya kutosha kila siku ili kulinda kiwago chake cha maji kisipungue na kinapopungua ndipo hapo mwili huanza kuonesha dalili za kukaukiwa maji (dehydration).

NINI HUSABABISHA?
Sababu zinazosabababisha mwili kukaukiwa maji huweza kuwa nyingi, lakini zinazojulikana zaidi ni pamoja na:

- Kuacha kunywa maji
- Kukaa kwenye joto kwa muda mrefu
- Kunywa kiwango kikubwa cha pombe,
- Ungonjwa wa kisukari ambao husababisha mtu kukojoa mara kwa mara
- Kutokwa na jasho jingi, kwa sababu ya ama kufanya kazi ngumu au mazoezi. Hivyo inashauriwa mtu anayetokwa jasho jingi kunywa maji mara kwa mara wakati akiendelea na shughuli inayomtoa jasho.
- Kama ukiugua au ukipatwa na homa kali, huweza kupungukiwa na maji mwilini
- Kutapika na kuharisha nako huweza kupoteza maji mwilini.

DALILI ZA KUKAUKIWA MAJI KWA WATOTO
Kwa kawaida, dalili za upungufu wa maji mwilini hujitokeza zaidi kwa watoto wadogo kuliko watu wazima au wazee. Dalili za upungufu wa maji mwilini kwa watoto huweza kusabababishwa ama na kuharisha, kutapika, kutokunywa maji au vimiminika vingine vya kutosha.

Mtoto mwenye dalili za upungufu wa maji huweza kuonesha dalili zifutazo:
- Kukojoa mara chache sana
- Mtoto kutokuwa mchangamfu
- Macho, tumbo au mashavu kubonyea
- Mdomo na ulimi kukauka
- Mtoto kulia mara kwa mara na anapolia machozi hayatoki.

DALILI ZA UPUNGUFU WA MAJI KWA WAZEE
Dalili za upungufu wa maji kwa wazee ni tofauti na watu wazima. Wazee wa umri zaidi ya miaka 60 huwa na ngozi iliyosinyaa na hata ukiiminya, hubaki katika hali hiyo kwa muda na unapoikwaruza alama hubaki.

Halikadhalika, wazee hukosa haja ndogo kwa muda mrefu, hupungukiwa uzito kwa kiasi kikubwa na hupatwa na homa.

DALILI ZA UPUNGUFU WA MAJI KWA WAJA WAZITO
Upungufu wa maji mwilini kwa waja wazito ni hatari kwa mama pamoja na mtoto. Dalili zinazoweza kujitokeza kwa waja wazito ni pamoja na:

- Kukojoa mkojo wa njano nyeusi
- Kuumwa na kichwa
- Mwili kukosa nguvu
- Kichefuchefu na kutapika
- Kukaukwa na mdomo

Ili kujiepusha na matatizo ya upungufu wa maji na hatimaye kujikuta unakumbwa na dalili kadhaa zilizoelezewa hapo, ambazo ziko pia kwa watu wazima wengine, ni kuwa na mazoea ya kunywa maji ya kutosha kila siku. Hata utakapozidiwa na kukimbizwa hospitali, hakuna dawa nyingine utakayopewa zaidi ya maji (re-hydrating solution). Kwa nini usubiri hali hiyo ikutokee wakati unaweza kuizuia kwa kunywa maji tu.IMEANDALIWA NA DOCTOR JOH BLOG
Post a Comment
Powered by Blogger.