Watuhumiwa bomba la mafuta waomba dhamana

Upande wa utetezi katika kesi ya kuhujumu uchumi inayomkabili mfanyakazi mstaafu wa Shirika la Mafuta Tanzania na Zambia (Tazama), Samwel Nyakirang'ani (63) na wenzake sita umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iwapatie dhamana wateja wao.
Akiwasilisha maombi ya dhamana, wakili wa utetezi Kusalika Augustine amesema leo Februari 15, 2018 mahakamani hapo kuwa wateja wake wanahitaji kupata dhamana kwa sababu mashtaka yanayowakabili yanadhaminika.
Mbali na Samwel, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Nyangi Mataro (54) ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi Ufukoni na mkazi wa Kisiwani Mkajuni Kigamboni.
Wengine ni mfanyabiashara Farijia Ahmed(39) mkazi wa Soko Maziwa Kigamboni, Malaki Mathias (39) mkazi wa Magogoni, Kristomsi Angelus (25) mkazi wa Soko Maziwa, fundi ujenzi Pamfili Nkoronko (40) mkazi wa Tungi Kasirati na Hunry Fredrick (38) mkazi wa Tungi, Kigamboni.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka matatu ya uhujumu uchumi kwa kujiunganishia isivyo halali bomba la mafuta ya dizeli kinyume cha sheria ya uhujumu uchumi.
Hata hivyo, baada ya kuwasilisha maombi hayo, upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Peter Maugo akisaidiana na Turumanywa Majigo ulidai mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya usikilizwaji, maombi ya dhamana na kwamba wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kujibu maombi hayo.
Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 22, ambapo upande wa mashtaka utajibu maombi yaliyowasilishwa na upande wa utetezi kuhusiana na washtakiwa hao kudhaminiwa. Washtakiwa wamerudishwa rumande.

Chanzo:Mwananchi
Post a Comment
Powered by Blogger.