MADHARA YA DAWA ZA KUPUNGUZA UNENE

Baadhi ya dawa hizi zinaweza kusababisha mapigo ya moyo kwenda haraka kuliko kawaida, shinikizo la damu, maruweruwe (hallucinations), kukosa usingizi, matatizo ya macho (glaucoma) na moyo kushindwa kufanya kazi zake vizuri.

Tafiti nyingi za kisayansi zinaonyesha kuwa dawa hizi kwa kiasi kikubwa zina kemikali kama vile phentermine, sibutramine, phenolphthalein, caffeine, hydroxycitric acid (HCA) na senna ambazo zina madhara makubwa kwa afya ya binadamu.

Je, wewe ni mnene na ungependa kupunguza uzito? Je, wewe ni mwanamke au msichana unayependa kuwa na umbo la kuvutia la namba nane? Kama jibu lako ni ndiyo kwa mojawapo ya maswali hayo hapo juu, inakupasa kuchukua tahadhari.

Tahadhari hiyo ni ya matumizi ya dawa za kupunguza uzito na unene zinazosambazwa katika vituo vya tiba mbadala, waganga wa jadi, maduka ya dawa, super market na ofisi mbalimbali nchini.
Watengenezaji, wasambazaji na wauzaji wa dawa hizi, huzinadi sana kupitia mitandao, vipeperushi, vyombo vya habari na hata matangazo mitaani.
Mojawapo ya sifa hizo ni kuwa zina uwezo mkubwa wa kupunguza unene, kupunguza lehemu mbaya mwilini, kuondoa sumu mwilini, kufanya mwili kuwa mwepesi, kupunguza kitambi, kujenga afya na kuepuka magonjwa sugu kama vile kiharusi, kisukari, uvimbe wa maungio, magonjwa ya moyo na kukoroma wakati wa kulala.
 
Katika utafiti uliofanywa na Ruth Chananie mwaka 2015, ilithibitika kuwa watengenezaji na wauzaji wa dawa hizi hutumia mbinu za kibiashara kuaminisha watu kuwa ni muhimu na hazina madhara.
Cananie anasema kuwa wengi huzitafutia dawa zao uhalali wa kitabibu kwa kuwatumia madaktari, vyombo vinavyoheshimika kama dini na serikali kupitia taasisi zake zenye mamlaka.
Katika matangazo pia hutumia lugha za kitabibu kuelezea ubora wa dawa hizi. Njia nyingine ni kuonyesha kuwa, watu wanene wana kasoro na hawapendezi kama baadhi ya watu maarufu hasa wasanii na wachezaji wenye mafanikio makubwa.
Matokeo ya utafiti huu yalichapishwa katika jarida la Sociological Spectrum toleo la 25.
Hata hivyo, ukichunguza kwa makini utagundua kuwa, watengenezaji wa dawa hizi, baadhi hujilinda kisheria kwa kuweka maandishi ya tahadhari katika bidhaa zao kwa kueleza kuwa bidhaa hizo hazikusudiwi kuwa dawa za kutibu, kugundua au kuzuia ugonjwa.
Tafiti nyingi za kisayansi zinaonyesha kuwa dawa hizi kwa kiasi kikubwa zina kemikali kama vile phentermine, sibutramine, phenolphthalein, caffeine, hydroxycitric acid (HCA) na senna ambazo zina madhara makubwa kwa afya ya binadamu.
Baadhi ya dawa hizi huathiri sehemu ya ubongo inayohusika na hamu ya chakula. Hamu ya chakula ni muhimu kwa ajili ya ubora wa afya na maisha.
Dawa yoyote inayoharibu hamu ya chakula kwa kipindi kirefu, inaweza kusababisha madhara makubwa ya kiafya.

Dawa nyingine huzuia mwili kufyonza wanga, mafuta pamoja na viinilishe vingine muhimu kutoka tumboni na katika utumbo mwembamba.
Dawa hizi pia zinaweza kusababisha tumbo lisisage na kuyeyusha chakula vizuri. Huchochea hali ya kuharisha na kukojoa sana.
Kufanya hivyo husababisha mwili upoteze nyama za mafuta, madini muhimu na maji kwa kasi kubwa ndani ya kipindi kifupi.
Hali hii inaweza kuathiri utendaji wa bakteria rafiki wa tumboni utendaji wa figo na afya ya moyo kwa kiwango kikubwa.

Baadhi ya dawa hizi zinaweza kusababisha mapigo ya moyo kwenda haraka kuliko kawaida, shinikizo la damu, maruweruwe (hallucinations), kukosa usingizi, matatizo ya macho (glaucoma) na moyo kushindwa kufanya kazi zake vizuri.
Madhara yanaweza kuwa makubwa zaidi kwa wanawake wajawazito, wanyonyeshao na wazee.
Katika utafiti wa mwaka 1996 uliofanywa huko Ufaransa na jopo la watafiti chini ya uongozi wa Lucien Abenhaim, ilibainika kuwa dawa za kupunguza unene zinazopunguza hamu ya kula, zinasababisha ugonjwa wa damu kujaa katika mishipa inayosambaza damu kati ya mapafu na moyo.
Utafiti huu ulichapishwa katika jarida la afya la The New England Journal of Medicine toleo la 335.
Kutokana na madhara yake kwa afya ya binadamu, Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani (FDA) ilipiga marufuku matumizi ya dawa nyingi katika kundi hili, baada ya kuzifanyia uchunguzi na kubaini kuwa zina kemikali zinazochochea kutokea kwa maradhi ya moyo, saratani, kiharusi, ugonjwa wa kusahau (dementia) na vifo vya ghafla.
Pia dawa hizi zinaweza kusababisha muingiliano kinzani na baadhi ya dawa za hospitalini kama vile za kisukari, mfano statins na monoamine oxidase inhibitors (MAOIs).
Ili kunusuru afya ya jamii, dawa zilizogundulika kudhuru afya ziliondolewa sokoni mwezi Oktoba, 2010 na FDA inaendelea kuwatahadharisha watu dhidi ya dawa za kupunguza unene.
Mnamo Aprili 2013, vyombo vingi vya habari huko Uingereza, vilitangaza habari za kifo cha mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Leeds katika Kitivo cha Udaktari Sarah Houston, mwenye umri wa miaka 23.

Binti huyo aliyepoteza maisha kutokana na matumizi ya dawa za kupunguza unene aina ya DNP (2, 4 Dinitrophenol).
Taarifa ya uchunguzi wa kifo baada ya kupima damu yake ilibainisha kuwa alikuwa akitumia dawa hizo kwa muda mrefu na ndizo zilizosababisha kifo chake kutokea ghafla.
Wataalamu wa masuala ya dawa Deborah Mitchel na David Dadson, katika kitabu chao kilichochapishwa mwaka 2002, kijulikanacho kwa jina la “The Diet Pill Guide: The Consumer’s Book of Over-the-Counter and Prescription Weight-Loss Pills and Supplements,” wanasema:
“Ingawa ushahidi wa madhara ya dawa hizi unazidi kuongezeka, bado watu wengi wanaaminishwa kwa uongo kuwa dawa hizi zina manufaa.
“Hata hivyo, pia watu wanaendelea kuamini kuwa dawa hizi zinatokana na mimea na ni dawa salama za asili zinazofanyiwa utafiti wa kina na kudhibitiwa na mamlaka za udhibiti wa usalama wa dawa kama dawa zingine za hospitalini.”
Mtaalamu wa sayansi ya lishe katika hospitali moja iliyopo Jimbo la Kogi huko Nigeria, Uche Ogbanufe anasema kwamba watu wengi wanaotumia dawa za kupunguza unene, wanapata madhara kwa sababu zimekusudiwa kupunguza unene kwa haraka katika kipindi cha muda mfupi.
Anaongeza kusema kuwa huwezi kupunguza unene pamoja na uzito kwa mtindo huo bila kuharibu mfumo mzima wa mwili.
Ogbanufe aliyasema hayo wakati alipokaririwa na waandishi wa habari wa mtandao wa Realnews Magazine.

Mnamo April 2012, mkurugenzi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), mfamasia Hiiti Sillo alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akizungumzia uwepo na matumizi ya dawa za kupunguza unene hapa nchini.
Sillo alisema TFDA haizitambui dawa hizo kwa kuwa hazijasajiliwa na kwamba wanaoziuza wako kinyume cha sheria za nchi zinazohusu usalama wa dawa.
Sillo aliongeza kusema kuwa ni lazima ieleweke kwamba ni kinyume cha Sheria ya Chakula na Dawa ya Mwaka 2003 kuingiza au kuuza dawa nchini bila kufuata taratibu zilizopo.
“Kwa kuwa dawa hizo hazijasajiliwa ni vigumu kujua kama zina madhara au la... Dawa yoyote kabla ya kuanza kutumika ni lazima isajiliwe ili kujua ubora na usalama wake kabla ya kuanza kutumika,” alisema Sillo.

Njia bora na salama ya kupunguza unene na uzito ni kufanya mazoezi kila siku, kujishughulisha na kazi mbalimbali zinazohitaji matumizi ya nguvu na ulaji unaozingatia kanuni za afya na lishe bora.
Ni bora kujiepusha na vyakula vyenye sukari nyingi na mafuta mengi hasa yenye asili ya wanyama. Ni vyema pia kuepuka vyakula na vinywaji vyenye sukari nyingi vilivyosindikwa viwandani.

Chanz0: Doctorjoh Blog

Post a Comment
Powered by Blogger.