WATU WAWILI WAJINYONGA MANYARA

Watu wawili wamefariki dunia wilayani Simanjiro mkoani Manyara kwa kujinyonga akiwemo mwanafunzi wa darasa la saba wa shule msingi iliyopo mji mdogo wa Mirerani.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Agustino Senga akizungumza leo Alhamisi amesema matukio hayo ya vifo yametokea kwenye mazingira tofauti.
Kamanda Senga amesema tukio la kwanza lilitokea kwenye Kata ya Endiamtu mji mdogo wa Mirerani ambalo limemuhusu mwanafunzi wa darasa la saba wa Shule ya Msingi Songambele, Neema Achuu (15).
Amesema mwanafunzi huyo anayeishi na shangazi yake alijinyonga chumbani kwao jana Jumatano saa saba mchana kwa kutumia mtandao na kufariki dunia papo hapo.
Amesema chanzo cha kifo hicho hakijajulikana na polisi bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na mwili wa marehemu huyo umehifadhiwa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.
Amesema kwenye tukio lingine mkata mkaa wa eneo la Kidawash, Tarafa ya Moipo, Isack Mlokole (60) alijinyonga na kamba kwenye mti.
Amesema polisi walipopata taarifa jana Jumatano saa 4 asubuhi walifika eneo la tukio na kukuta mfuko ukiwa pembeni ya mwili wake uliokuwa ukining'inia.
"Kwenye huo mfuko aliouacha marehemu tulikuta ujumbe kuwa ameamua kujiua mwenyewe na mtu yeyote asisumbuliwe wala kuulizwa juu ya kifo chake kwani ni uamuzi wake mwenyewe ukiwa na jina lake," alisema Kamanda Senga.
Post a Comment
Powered by Blogger.