USAJILI WASHUKA SHULE BINAFSI, WAZAZI WAKIMBILIA ZA SERIKALI

Usajili wa wanafunzi kwa shule za binafsi nchini umedorora baada ya wazazi wengi kuamua kuwapeleka watoto wao shule za Serikali.
Akizungumza na mwandishi wetu aliyetaka kujua hali ya uandikishaji wa wanafunzi na ada kwa shule binafsi, Mkurugenzi Mkuu wa Shirikisho la Watoaji Elimu Wasiotegemea Serikali Kusini mwa Jangwa la Sahara (CIEPSSA), Benjamin Nkonya alisema walichokiaona sasa hivi ni kushuka kwa usajili. Alisema mwaka huu umeshuka kwa asilimia 32 tofauti na 24 za mwaka jana.
Akielezea sababu za kupungua kwa usajili huo Nkonya alisema ni kutokana na kipato kwa wazazi hali iliyosababisha wengi wao kuhamisha watoto wao.
Sababu nyingine ni uboreshwaji wa elimu kwa upande wa Serikali akisema hivi sasa wazazi wanaridhika na hali ya elimu inayotolewa nchini tofauti na miaka ya nyuma. “Hivi sasa Serikali imejipanga kuboresha elimu na hii ndiyo sababu wazazi wanakuwa na imani na shule za Serikali, walikuwa wanaleta watoto wao huku kutokana na changamoto mbalimbali zilizokwepo,” alisema.
Hata hivyo, Nkonya alisema licha ya Serikali kuboresha elimu, bado kuna changamoto ya uhaba wa miundombinu ikiwamo madarasa.
“Sasa tulikuwa tunafikiria kuwaleta wanafunzi kwenye madarasa yetu ambayo asilimia 30 yapo tupu tukawa na mikataba ya Public and Private Partnership (PPP) -- ushirikiano wa Sekta Binafsi na Umma-- kwa sababu kuna baadhi ya shule za Serikali wanafunzi wanasoma 200 darasa moja,” alisema. Alisema kuendelea kushuka kwa usajili kunaweza kusababisha shule za binafsi kufa.
“Ndio maana nimetanguliza rai kwa Serikali waone namna ya kuwalinda hawa wamiliki, kwa sababu hizi ni rasilimali ambazo asilimia 97 ya wawekezaji wa shule binafsi ni Watanzania. Waone namna ya kuwalinda kwa sababu walijinyima kula ili wawekeze,” alisema.
Akizungumza kwa simu kutoka Mpanda mkoani Katavi, Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Mizengo Pinda, Paschal Peleka alisema usajili wanafunzi wanaoanza darasa la kwanza unaenda vizuri na mwitikio ni mkubwa.
Alisema hadi sasa wameandikisha wanafunzi 200 shuleni hapo kati yao 80 wametoka darasa la awali na 120 wapya. “Wanafunzi ni wengi ila changamoto iliyopo hapa ni madarasa, hayo ndiyo yanahitajika zaidi lakini kwa upande wa vitabu na madawati kila kitu kipo sawa,” alisema. Alisema idadi hiyo ya wanafunzi haikupishana sana na ya mwaka jana akibainisha kuwa hiyo ni kutokana na mwamko wa wazazi kutaka watoto wao wasome.
Mkazi wa Ilala Bungoni, Dar es Salaam, Richard Mrutu alisema kushuka kwa usajili katika shule binafsi kumetokana na kuimarika kwa hali ya elimu katika shule za Serikali ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
“Nilichokiona katika hii sera ya elimu bure ni kwamba, wazazi wengi walikuwa hawana uwezo wa kusomesha watoto wao kutokana na michango mbalimbali ikiwamo ada,” alisema. Alisema wazazi walikuwa wanapeleka watoto wao shule za binafsi wa sababu elimu katika shule hizo ilikuwa bora kuanzia miundombinu, mazingira ya kusomea na vitabu.
“Mimi wanangu wanasoma shule za ‘kayumba’ kwanza uwezo wenyewe sina lakini hata hao wanaowapeleka huko (binafsi) bado watashindwa kwa sababu kwa sasa elimu inayotolewa kule ni sawa na hizi za kawaida tu,” alisema.

Chanzo: Mwananchi
Post a Comment
Powered by Blogger.