UJUE UGONJWA SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI (CERVICAL CANCER)- CHANZO, DALILI NA TIBA

Saratani ya shingo ya kizazi ni aina ya saratani inayotokea katika chembechembe za shingo ya kizazi, ambayo ni sehemu ya chini ya mji wa mimba (uteri) inayoungana na uke. Ni saratani inayotokea kwa wingi miongoni mwa wanawake duniani kote, hususani wenye umri wa miaka kati ya 20 na 39 na inaongoza kwa kusababisha ugonjwa na vifo kwa wanawake katika nchi zilizoko chini ya jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania.
Inawaathiri watu wa tamaduni na tabaka zote. Kidunia, saratani ya shingo ya kizazi ni ya pili miongoni mwa saratani zinazowapata wanawake ambapo wagonjwa wapya wapatao 529,828 hugunduliwa kila mwaka, 85% wakiwa ni katika nchi zinazoendelea. Inabakia kuwa ya pili baada ya saratani ya matiti kwa kusababisha vifo vitokanavyo na saratani, ambapo huchangia 10% ya vifo vitokanavyo na saratani mbalimbali kwa wanawake. Inakadiriwa kuwa zaidi ya wanawake 275,000 hufa kila mwaka kwa ugonjwa huu, idadi kubwa ni kutoka nchi zinazoendelea Tanzania ikiwemo.

VISABABISHI/ VIPENGELE HATARISHI
Wanawake wengi wanaopata ugonjwa huu huwa na kisababishi kimoja au zaidi kinachojulikana ambacho/ambavyo huongeza hatari ya kuupata. Vifuatavyo ni visababishi vikuu:
 1. Kuanza vitendo vya ngono katika umri mdogo (chini ya miaka 16)
 2. Kuwa na mahusiano ya kimwili na zaidi ya mwanaume mmoja
 3. Maambukizo ya virusi vya HPV (Human papilloma virus)
 4. Maambukizo ya magonjwa ya zinaa
 5. Umri zaidi ya miaka 30
 6. Upungufu wa kinga mwilini (VVU/UKIMWI)
 7. Uvutaji wa sigara
 8. Kupata mimba katika umri mdogo
 9. Idadi kubwa ya watoto na kuzaa mara kwa mara
 10. Hali duni ya kiuchumi
 11. Kuwa na mahusiano ya kimwili na mwanaume ambaye mkewe alikufa kwa saratani ya shingo ya kizazi
 12. Kuwa na mahusiano ya kimwili na mwanaume ambaye hajatahiriwa
 13. Historia ya saratani ya shingo ya kizazi katika familia
Kuanza vitendo vya ngono katika umri mdogo na kuwa na mahusiano ya kimwili na zaidi ya mwanaume mmoja ni visababishi vinavyoongoza. Pia maambukizo ya virusi vya HPV (Human papilloma virus), hususani aina ya 16, 18, 31, 33, 35, 45 na 56 huchangia kwa kiasi kikubwa katika kusababisha ugonjwa huu.

DALILI
Katika hatua za awali za ugonjwa huu kunaweza kusiwe na dalili zozote. Lakini, kadri muda unavyosonga dalili bayana hujitokeza. Dalili za awali ni kutokwa na damu ukeni baada ya tendo la ndoa, kupata maumivu wakati wa tendo la ndoa, kutokwa na maji maji ukeni yasiyo ya kawaida/ yenye harufu na maumivu ya tumbo chini ya kitovu. Muda unavyosonga zaidi, ugonjwa huu unaweza kusambaa kwenda tumboni, mapafuni au popote pale mwilini. Dalili nyinginezo ni kama: maumivu ya mgongo, maumivu ya nyonga, miguu kuuma na/au kuvimba, uchovu, kukosa hamu ya kula, kupungua uzito, kutokwa na damu kwa wingi ukeni, kutokwa na mkojo au kinyesi ukeni (fistula) na kuvunjika mifupa kwa urahisi.
KINGA NA MATIBABU
Saratani ya shingo ya kizazi yaweza kuzuilika kwa:
 • Kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu mara kwa mara.
 • Kupata chanjo dhidi ya virusi vya HPV kabla ya kuanza vitendo vya ngono.
 • Kupata elimu sahihi kuhusu ugonjwa huu.
 • Kujiepusha na mambo hatarishi yanayosababisha kuupata ugonjwa huu.
 • Ugunduzi wa mapema katika hatua za awali za ugonjwa huu na kupatiwa matibabu stahiki na kwa wakati.

BAADHI YA IMANI POTOFU KUHUSU SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI
Zifuatazo ni baadhi ya imani potofu za wanajamii juu ya mtu mwenye ugonjwa huu:
 • Amerogwa
  • Ukweli: Ugonjwa huu hautokani na kurogwa bali ni kutokana na sababu bayana zilizotajwa hapo juu.
 • Mapenzi ya Mungu
 • Ukweli: Huu ni ugonjwa unaosababishwa na maambukizo ya virusi vya HPV (Human papilloma virus) na visababishi vingine kama vilivyoorodheshwa hapo juu.
 • Lazima ana virusi vya UKIMWI
  • Ukweli: Siyo wanawake wote wenye ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi ni waathirika wa VVU/UKUMWI.
 • Anaweza kutibiwa na dawa za kienyeji
  • Ukweli: Saratani ya shingo ya kizazi haitibiwi kwa dawa za kienyeji. Wahi hospitalini mapema mara uonapo dalili za ugonjwa huu ili kupata huduma stahiki na kwa wakati.
 • Hakuna tiba
  • Ukweli: Katika hatua za awali, ugonjwa huu hutibika na mgonjwa hupona kabisa. Nenda hospitali iliyo karibu nawe kwa ajili ya uchunguzi na ushauri hata kama hauna dalili zozote.
Kutokana na imani hizo, wagonjwa wengi hutafuta msaada wa kitabibu mahospitalini katika hatua za mwisho za ugonjwa huu baada ya hali ya kiafya kudodora sana. Hali hiyo hupelekea wagonjwa wengi kupoteza maisha mapema. Hivyo basi, ni vizuri kwenda hospitalini mapema mara tu dalili za awali zijitokezapo ili kupata huduma na matibabu stahiki kwa wakati.

ZINGATIA: Kinga ni bora kuliko tiba. Nenda leo ukapate ushauri wa kiafya na kufanyiwa uchunguzi.Imeandaliwa na Ibrahim M.
Post a Comment
Powered by Blogger.