POLISI WAKABILIANA NA WAFUASI WA NASA NAIROBI NCHINI KENYA

 Umati mkubwa wa wafuasi wa muungano wa Nasa umejitokea kumpokea kiongozi wao, Raila Odinga katika sherehe zilizogeuka kuwa za vurugu, mabomu ya machozi na mapambano ya kukimbizana na polisi.
 Watu wawili wanadaiwa kufariki dunia baada ya kupigwa na kinachosadikiwa kuwa ni risasi wakati polisi wakiwatawanya watu waliokuwa wanatembea kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) walipokuwa wakitembea sambamba na msafara wa kiongozi huyo wa Nasa aliyerejea mchana leo akitokea Marekani alikofanya ziara ya siku 10.
Mapema, polisi na wafuasi wa Raila walipambana katika barabara ya kuelekea uwanja wa ndege kabla ya Raila kuwasili.
Licha ya ulinzi huo na moshi wa mabomu ya machozi wafuasi wa Nasa wapatao 200 wakiwemo wanawake walifanikiwa kupita utepe uliowekwa na vyombo vya usalama na wakaingia hadi ndani ya uwanja.
Helikopta ya polisi ilikuwa ikizunguka juu ya uwanja huo huku magari ya maji ya kuwasha na magari ya maalumu ya kusafisha njia yalikuwepo uwanjani hapo na yalitumika kuzima moto wa matairi.
Lakini wakati Raila akiondoka katika msafara wenye makumi ya magari yakiwemo ya viongozi wa Nasa na mamia ya wafuasi, yalizuka mapambano huku polisi wakitumia magari ya kurusha maji ya kuwasha, mabomu ya machozi huku waandamanaji wakirusha mawe na fimbo.

Chanzo: Mwananchi
Picha na Daily Mail
Post a Comment
Powered by Blogger.