MKUU WA MKOA WA MOROGORO APATA AJALI USIKU WA KUAMKIA LEO

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Steven Kebwe amepata ajali katikati ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi iliyopo wilayani Kilosa mkoani hapa.
Ajali hiyo ilitokea saa saba usiku wa kuamkia leo Jumatano ambapo inadaiwa gari la mkuu huyo wa mkoa lilimgonga mnyama aina ya Nyati na gari hilo kuharibika vibaya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Urlich Matei amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa taarifa kamili ataitoa mara baada ya kukamilika.
Inadaiwa kuwa ndani ya gari hilo mbali na kuwepo mkuu wa mkoa pia aliambatana na mlinzi wake ambao wote kwa pamoja walitoka salama.
Mwandishi wa Mwananchi alifanya juhudi za kumtafuta mkuu wa mkoa kwa njia ya simu ili kuzungumza naye juu ya ajali hiyo lakini simu yake iliita bila kupokelewa.

Chanzo: Mwananchi
Post a Comment
Powered by Blogger.