Kafulila ajivua uanachama wa CHADEMA

Mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila ambaye Desemba mwaka jana alijiunga na Chadema, ametangaza kung’oka upinzani kwa madai hauna dhamira ya dhati ya kupambana na ufisadi.
Kafulila aliyekuwa mbunge 2010-2015 alitikisa kwenye mapambano ya sakata la ufisadi wa mabilioni ya akaunti ya Tegeta Escrow iliyoitikisa serikali katika utawala wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete ametangaza uamuzi huo leo Novemba 22.
Akizungumza na Mwananchi kuthibitisha waraka wake alioutoa wa kujivua uanachama wa Chadema amesema ‘’ni kweli nimeondoka na siwezi kusema nakwenda wapi kwa sasa.”
Katika waraka huo, Kafulila amesema tangu Rais John Magufuli achaguliwe na kukabidhiwa jukumu la kuongoza nchi, vita ya miaka mingi dhidi ya ufisadi imechukua sura mpya.
“Wahusika na watuhumiwa wakubwa wa rushwa ambao walikuwa hawaguswi huko nyuma tunashuhudia wakifikishwa mbele ya vyombo vya sheria. Kutokana na juhudi za kupambana na rushwa na ufisadi zinazoendelea nchini…juhudi hizi zinapaswa kuungwa mkono,” amesema Kafulila
“Vyama vya upinzani vinaonekana kupigwa ganzi na kupooza katika juhudi zake za kupambana na ufisadi. Ghafla ufisadi sio tena agenda kuu ya vyama vya upinzani nchini, kwa sababu hii, ni wazi kuwa upinzani sio tena jukwaa salama la kuendesha vita dhidi ya ufisadi,” ameongeza
Kafulila ambaye ni mme wa mbunge wa viti maalum Chadema, Jesca Kishoa amesema ‘’kwa kuwa sina imani tena na upinzani kama jukwaa salama la kupambana na ufisadi, nimeamua kwa hiari na utashi wangu kujivua uanachama wa Chadema kuanzia leo.”
“Nitatangaza katika siku za hivi karibuni jukwaa jipya la harakati zangu dhidi ya ufisadi. Nawatakia safari njema waliobaki ndani ya Chadema kwa kile wanachokiamini.”
Post a Comment
Powered by Blogger.