VYAKULA VITATU VINAVYOWAPITA ‘KUSHOTO’ WATANZANIA

Wakati ulaji wa nyama unaoshauriwa kwa mwaka na Shirika la Afya duniani (WHO) ukiwa kilo 50, kiwango cha ulaji wa kitoweo hicho hapa nchini kwa mwaka 2015/16 kilikuwa kilo 15 kwa kila mtu, huku tatizo likichangiwa na gharama za mifugo husika.
Licha ya ulaji wa nyama kuwa chini tofauti na mapendekezo ya WHO, unywaji wa maziwa nao uko chini ukidaiwa kuwa ni lita 45 kwa mwaka ilhali kiwango kinachopendekezwa na shirika hilo kikiwa lita 200.
Katika ukanda wa Afrika Mashariki nchi ambayo wananchi wake hunywa maziwa kwa wingi ni Kenya.
Hata hivyo, wakati Watanzania wakiwa nyuma kwa unywaji wa maziwa na ulaji wa nyama, pia ulaji wa samaki ni wa kiwango cha chini ikilinganishwa na mapendekezo ya Shirika la Chakula Duniani (FAO), kutokana na uzalishaji usiokidhi mahitaji ya soko.
Kwa mujibu wa FAO, kila mtu kwa mwaka anatakiwa kula kilo 15 za samaki, lakini kwa hapa nchini ulaji ni kilo 7.6.
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba alisema juzi wakati wa ufunguzi wa mradi wa kufugia samaki wa Ruvu Fish Farm uliopo Miswi wilayani Kibaha kuwa, Watanzania wanashindwa kufikia mapendekezo ya shirika hilo kutokana na uzalishaji mdogo wa samaki.
Alisema hali husababisha wafanyabiashara kuagiza bidhaa hiyo nje ya nchi.
Akizungumzia ufugaji wa samaki, Dk Tizeba aliitaja changamoto ya upatikanaji wa vifaranga na teknolojia za kisasa kuwezesha kuwapo kwa ufugaji unaofuata taratibu.
Mkurugenzi wa Ruvu Fish Farm, Poul Hansen alisema kwa sasa wanazalisha tani saba za sato kwa mwezi na vifaranga vya samaki 500,000 kwa mwaka huku wakiwa na mabwawa 30.
Alisema mradi huo ulioanza mwaka 2015 ukiwa na wafanyakazi watano, hivi sasa umeajiri watu 20.
Balozi wa Denimark nchini, Einar Jensen alisema mradi huu ulitokana na mazungumzo ya kibiashara ambayo yaliandaliwa na ubalozi huo na umefadhiliwa na Shirika la Misaada la Denimark (Danida) kwa gharama ya Sh2 bilioni.
Post a Comment
Powered by Blogger.