JIFUNZE NJIA ZA KUHIMILI MISUKOSUKO YA NDOA

Siku moja nilihudhuria sherehe ya harusi ninayoikumbuka hadi leo. Siikumbuki kwa kutokana na mahanjumati, hoihoi au vifijo bali nasaha alizotoa mzazi mmoja.
Aliwaambia maharusi, “Ndoa ni kitu cha ajabu kwani walio nje wanatamani kuingia na walio ndani wanatamani kutoka.” Tangu wakati huo nimeendelea kutafakari kama usemi wa mzazi yule alikuwa sahihi au hapana.
Je, wewe msomaji wangu uliye katika ndoa unakabiliwa na changamoto ambazo wakati mwingine zinakufanya hata ufikirie kutoka katika ndoa yako? Au wewe ni miongoni mwa watu wanaofurahia maisha ya ndoa zao na wala hupambani na misukosuko yoyote.
Bila kujua jibu lako naomba nizirudishe fikira zako kwenye nasaha za yule mzazi kwenye sherehe ya harusi.
 Hebu mchukulie mwanandoa kama nahodha anayeendesha chombo cha baharini. Kwa kawaida nahodha anapokuwa safarini kuna wakati hali ya hewa huweza kubadilika bahari ikachafuka na kukifanya chombo, kikayumba na kusukwasukwa huku na kule. 
Hali hii inapotokea wewe ungemshauri nahodha afanye nini. 
Akiache chombo kizame na kuacha kabisa kazi ya unahodha? Au atumie akili maarifa na ujuzi wake wote kukiongoza chombo hadi tufani itulie na bahari iwe shwari tena ili safari iendelee.
 Misukosuko katika ndoa ni kama tufani katika safari ya baharini. Changamoto zinazotokea mara kwa mara katika ndoa huwa zinahusu mambo ya kawaida wala huwa hazistahili kumfanya mwanandoa kuvunja ndoa yake. Kama isivyo sahihi kwa nahodha kukiacha chombo kizame inapotokea tufani mwanandoa asiiache ndoa yake ikavunjika kutokana na migogoro.
Kama wahenga walivyosema “Majembe mawili yakikaa pamoja hayakosi kugongana.” Vivyo hivyo watu wawili wanapokaa pamoja kwa muda mrefu hawakosi kupishana mawazo. Mtafaruku huwa haitokei kwenye ndoa tu bali katika karibuni aina zote za uhusiano wa binadamu. Lakini, katika ndoa mtafaruku unapozidi huweza kuwa wa kutatanisha hata ukamfanya manandoa akahisi hauwezi kutatuliwa. Hali hii huwa haitokani na mtafaruku bali mtazamo na fikira za mwanandoa mwenyewe. Ukichunguza utagundua kila ndoa iliyoshamiri imepitia katika changamoto nyingi.
Ikiwa mawazo ya mwanandoa atayaelekeza kwenye kuvunja ndoa, hata kama tatizo ni dogo atajikuta wazo hilo ndilo linalotawala katika fikira zake. Kilicho muhimu zaidi kwake ni kuitanguliza ndoa kwanza kama kitu muhimu na ambacho hakistahili kuvunjika. Kisha kufikiria na kutafuta njia zinazoweza kuleta suluhu au maelewano na kuiacha ikiwa salama. Uhodari katika ndoa hauwezi kupimwa kwa urefu wa vipindi vya furaha ambavyo wanandoa wamekuwa navyo bali kwa kiwango cha mitihani ambayo wameivuka katika maisha yao ya ndoa.
Baadhi ya wataalamu wa elimu jamii wamefanya utafiti na kugundua baadhi ya njia zifuatazo ambazo wanandoa wanaweza kuzitumia ili kudhibiti migogoro isiwapelekee kuvunja ndoa.
Kutambua kuwa hasira ni hisia au mihemko ya kawaida tu katika maisha
Mume na mke wanaopendana ni lazima wakubaliane kuwa katika ndoa yao kunaweza kutokea wivu, maudhi, hasira na vitu vingine vya aina hii.
Waamini vitu kama hivi vinapotokea kuwa hakuna sababu kwa mmoja wao kufadhaika au kupata hofu au kukata tamaa.
Hakika watambue kuwa mwenzake unapokasirika kufadhaika au kughadhibika kwa jambo ulilomtendea siyo kwamba mapenzi yake kwako yamekwisha. Waamini kwa dhati katika akili na nafsi zao kuwa maudhi na vikwazo katika ndoa ni vitu vya kuja, vikajadiliwa na maelewano kufikiwa na kisha vikaondoka bila kuathiri mapenzi na upendo katika ndoa yao. Wakijenga imani hii wakaikubali na kuifanya ikawa sehemu ya maisha yao hawatakubali kuyumbishwa na vitu hivi vya kawaida ambavyo havitokei tu katika ndoa bali hutokea kote katika jamii.
Jenga unyenyekevu katika ndoa
Kuna jambo moja ambalo kila ninapowaeleza wanandoa huwa hawakubaliani na mimi lakini baada ya muda mrefu wa maisha ya ndoa huwa wanakiri kuwa nimesema kweli “Hakuna mtu yeyote anayeweza kuishi katika ndoa bila kumtendea mwenzake kosa lolote. Anayeamini hivyo kwangu mimi ni kama ndoto. Wanandoa wote hutendeana makosa ya aina mbalimbali, makubwa na madogo. Hivyo hakuna haki ya mwanandoa mmoja kumshutumu mwenzake kama ndiye mkosaji pekee.
Jambo la muhimu ni kujifunza kuaminiana na kusameheana. Tuzoee kusema “Samahani mpenzi ninasikitika” kwani watu wawili wanaoishi pamoja hawawezi kuepuka kabisa kukwazana. Hata hivyo haifai kumkwaza mwenzako, hivyo omba msamaha kila unapomkosea.
Mjali mwanandoa mwenzako na tambua anapokuwa hana raha
Migogoro ya ndoa inaweza kutokana na sababu za ndani kwa wanandoa wenyewe au nje ya wanandoa. Kuna mambo kadhaa kazini au katika jamii yanayoweza kumchanganya mwenzako hadi akashindwa kuwa katika hali ya kawaida ya mapenzi. Inapotokea hali kama hii usimchukie mwenzako.
Muulize haya maswali mawili “Mpenzi wangu kuwa jambo nimekufanyia lililokuudhi?” Iwapo atasema hakuna, muulize swali jingine, “Je mpenzi wangu kuna jambo gani unafikiri nikufanyie ili ufurahi?” Hata kama ataendelea kusema hakuna, bila shaka atakueleza sababu iliyomuhudhunisha. Hali hii itatokana na maswali utakayokuwa umemuuliza ambayo kwake yatakuwa ni zawadi kubwa.
Kamwe usikubali kushindwa kuizuia hisia inayoweza kukufanya ukate tamaa
Baadhi ya wanandoa wanapoona misukosuko imezidi katika ndoa hukimbilia uamuzi wa kumuacha mwenzake akiwa mume au mke. Baada ya muda huamua kupata mwenza mwingine katika ndoa ya pili wakihisi kuwa hilo litakuwa suluhisho. Lakini mara nyingi waliofanya hivyo wamejilaumu kuwa huo haukuwa uamuzi wa busara kwani changamoto walizozikimbia mwanzo huziona zinarudi tena katika ndoa ya pili.

Hitimisho
Washauri wa ndoa huamini kuwa “Mapenzi bora katika ndoa hupatikana kwa watu wawili wanaoishi pamoja huku wakijua na kukubali kuwa kutofautiana hulka ni jambo la asili kwa binadamu” Wanachohitaji kufanya ni kila mmoja kujirekebisha na kwa busara kumuathiri mwenzake ili waweze kuendana vyema katika ndoa na maisha yao kwa ujumla.
Post a Comment
Powered by Blogger.