Rais Magufuli aagiza TCRA kuzifuta kampuni za simu zitakazoshindwa kujiunga na soko la hisa

Rais John Magufuli ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuyafuta makampuni ya simu yatakayoshindwa kujiunga na Soko la hisa la Dar es Salaam.
Rais Magufuli amesema hayo leo Juni Mosi, wakati akizindua mfumo mpya wa ulipaji kodi kwa njia ya kielektroniki, Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
Pia ameziagiza taasisi za Serikali na kampuni binafsi kujiunga na mfumo wa ukusanyaji mapato ili kuiwezesha Serikali kupata kodi bila uonevu kwa upande wowote.
Rais Magufuli amesema dhamira ya Serikali ni kukusanya kodi bila kuwepo kwa malalamiko kutoka upande wowote.
Pia amepiga marufuku wizara na taasisi nyingine za Serikali kuanzisha vituo vya taarifa kwa kuwa vilivyopo ni vingi na wakati huo vinatumia gharama kubwa katika kuanzisha.
“Data Centre kama hii ni mkombozi mwingine wa kupunguza kero mbalimbali, kwa sababu ukijaza vocha yako uko Zanzibar, ukinunulia vocha yako Kigoma au Moshi, hiyo pesa inakuja TRA, hakuna mabishano” amesema
Kadhalika Rais Magufuli amesema anajivunia kuwa na mitandao mingi ya simu ambayo inamsaidia kuwasiliana bila kero wakati wowote.
“Mimi nina mitandao yote ya simu, nina Tigo, Airtel, Vodacom na hata TTCL, mtu akinitafuta huku Airtel,akanikosa ninaweza kuweka Tigo, ili mradi ninatambalika kila mahali,” amesema
Pia amesema, mitandao hiyo ya simu inamsaidia kupata taarifa mbalimbali zinazoendelea nchini na duniani.
Hata hivyo, Rais amezitaka kampuni za simu kuhakikisha zinalipa kodi ili serikali isikose mapato yake.
Amesema mfumo huo wa ulipaji kodi kwa njia ya kielektroniki una faida yake na hivyo akawaomba watanzania, wawekezaji na wafanyabiashara kukitumia chombo hicho kwa manufaa ya taifa zima.
“Lengo la serikali ni kukusanya mapato. Wenye moyo wa kulipa kodi zao kihalali ni wachache, lakini wapo wasiotaka kulipa kodi na wapo wanaoonewa kwa kubambikiwa kodi. Lakini kwa wale wasiolipa, muarobaini wao ndiyo huu,” amesema
Pia Rais amesema amefurahi baada ya kutembelea kituo cha ukusanyaji taarifa (Data Centre)na kueleza kuwa umuhimu wake ni kukusanya na kulinda taarifa za nchi.
“Nimefurahi kwa sababu haya ni mafanikio makubwa kwa nchi yetu na ninapenda kuwashukuru waliowezesha kufikia mafanikio haya.” amesema
Post a Comment
Powered by Blogger.