JE WATAKA KUJUA: CHIMBUKO LA SIKU YA WAJINGA NA MADHARA YAKE

Najua leo umepanga mengi ya kufanya ili kuwadanganya ndugu, jamaa na marafiki ili uifurahie Siku ya Wajinga duniani.
Si wewe tu, hata kampuni, taasisi na vyombo vya habari vya kimataifa vimefanya kama wewe na pengine maelfu ya watu wameingia katika mtego huo.
Hata hivyo wengi tunaisherehekea, lakini hatufahamu asili ya sikukuu hii ambayo kwa lugha ya Kiingereza huitwa Aprils Fools.
Kwa mujibu wa gazeti la Washington Post, asili ya Siku ya Wajinga ilianza mwaka 1582 wakati ambapo Ufaransa ilibadili kalenda ya Julian na kuhamia kwenye kalenda ya Gregorian.
Kubadilika huku kwa kalenda kulibadilisha tarehe za mwaka na hivyo nchi hiyo ikaanza kusherehekea mwaka mpya Januari Mosi badala ya Aprili.
Lakini kwa bahati mbaya maamuzi hayo ya kubadili kalenda ya mwaka yaliyofanywa na Papa Gregory wa 13, hayakuwafikia wananchi wote wa Ufaransa na badala yake baadhi wakaendelea kusherehekea mwaka mpya Aprili Mosi. Hivyo basi waliosherehekea mwaka mpya Aprili Mosi, waliitwa wajinga na siku hiyo ikaitwa ya wajinga.
Wengine wanaihusisha siku hii na sherehe za Warumi zilizoadhimishwa Aprili Mosi ambapo watu walivaa nguo za ajabu na za kuchekesha wakati huo, ilianza kusherehekewa Machi 25 na kumalizika Aprili Mosi.
Baadhi ya wanahistoria wa Uingereza wameihusisha sikukuu hii na sherehe zinazofanywa kila Aprili Mosi nchini India ambapo watu walirushiana vitu na kuchafuana kwa keki au rangi kama sehemu ya utani.

Vyombo vya habari, taasisi zinavyoiadhimisha siku ya wajinga
Kama ilivyo siku ya afya duniani baadhi ya taasisi kubwa duniani nazo huadhimisha Siku ya Wajinga na kuwaweka mtegoni maelfu ya watu.
Mwaka 1957 Televisheni ya Uingereza (BBC), ilionyesha kipande kifupi cha video katika kipindi cha Panorama kinachoonyesha wakulima huko Uswisi wakivuna tambi (spaghetti). Dakika chache baada ya video hiyo kurushwa, mamia ya wananchi walijaa katika ofisi za shirika hilo la utangazaji wakitaka kujua aina hiyo ya kilimo cha tambi.
Mwaka 2008, BBC kwa mara nyingine walirusha video fupi iliyoonyesha pengwini(ndege mnene wa (majini asiyeweza kuruka juu)wakiruka angani na taarifa hiyo ilieleza kuwa wanyama hao wanakimbia hali ya hewa ya bara la Antarctic na kwenda America ya Kusini. Kiasili, pengwini hawezi kuruka.
Duka kubwa la vyakula (supermarket) la Tesco, nchini Uingereza liliweka tangazo kuwa limetengeneza karoti zinazopiga mluzi au mbinja. Tangazo hilo lilieleza kuwa karoti hizo zina nafasi katikati na ukizipika zinapiga mluzi. Wateja walimiminika kwenda kuzinunua.
Mwaka 2006, gazeti moja hapa nchini lilitoa tangazo lililowataka wasichana wote mabikira kufika katika ofisi za gazeti hilo ili wapate ajira. Mamia ya wasichana walifurika asubuhi siku hiyo katika ofisi za gazeti hilo.

Dini inachosema kuhusu siku hii
Mchungaji wa Kanisa la Jesus Gospel Ministry, Arnold Malecela alisema Biblia haisemi lolote kuhusu siku hii hivyo kila mtu ataongozwa na dhamiri yake.
“Kama Biblia imekaa kimya katika hili, basi nadhani kila mtu atatakiwa kuongozwa na dhamiri yake. Kwa sababu hakuna mstari unaoonyesha imekataza au imekubali” alisema
Alisema hata yeye akiwa kama ni kiongozi wa dini, atafanya kulingana na dhamira yake.
“Hata kipindi cha mababu waliotajwa katika Biblia, kwa mfano Yakobo na kina Esau, waliishi kwa dhamiri kwa sababu hakukuwa na sheria, baadhi ya mambo yameeleweka zaidi baada ya Musa kutoa torati,” alisema.
Lakini, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza la Kiislamu la Taifa (Bakwata) Sheikh Khamis Mataka anatofautiana na Mchungaji Malecela.
Sheikh Mataka alisema katika Uislamu uongo hauruhusiwi hata kama ni wa mzaha.
“Hata kama uongo huo ni mzaha na baadaye utaelezwa ukweli, bado ni dhambi. Lakini pia uongo wa siku hii unaweza kuleta madhara na ndiyo maana dini haiikubali siku hii,” alisema.
Alisema wakati mwingine watu hudanganyana siku ya wajinga na kusababisha madhara, baadhi hudanganya kuhusu msiba na kuwafanya watu kupata mshtuko mkubwa.
“Nasisitiza kwamba Uislamu unataka siku hiyo iepukwe kwa sababu inaweza kuleta madhara,” alisema.
Alifafanua zaidi na kusema siku hiyo ni ya kigeni na hivyo si busara kwa Watanzania kuiga hata ujinga na upuuzi.
“Thamani ya uzalendo wetu ipo wapi iwapo tunaiga hata ujinga. Hatuna muda wa kupoteza,” alisema.

Madhara ya Siku ya Wajinga
Pamoja na kuwa utani au uongo unaofanywa siku hii hauna nia mbaya,lakini imewahi kutokea ukaleta madhara.
Kwa mfano, mwaka 1986, Ofisa Upelelezi wa Israel alitumia Aprili Mosi kuandika ujumbe mfupi na kuusambaza kuwa kiongozi wa Shi’ite, Nabih Berri, amejeruhiwa vibaya na watu waliopanga kumuua.
Habari zikatangazwa katika redio za Israel na za Kiebrania na baadaye katika vyombo vya habari vya Kiingereza.
Habari hizo zilisababisha mshtuko katika eneo hilo na baadaye, Waziri wa Ulinzi Yitzhak Rabin akatangaza kukamatwa kwa ofisa huyo.
Post a Comment
Powered by Blogger.