Method Mwanjali wa Simba kuwa nje mwezi mzima

Mchezaji wa klabu ya Simba, Mzimbabwe Method Mwanjali ataendelea kuwa nje kwa mwezi wote wa Machi kutokana na maumivu ya goti.

Mwanjali hajajumuishwa katika kikosi ambacho kimeenda ziarani mkoani Dodoma kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya wenyeji, Polisi Jumamosi wiki hii Uwanja wa Jamhuri.
Daktari wa klabu ya Simba, Yassin Gembe amesema kwamba Mwanjali hatakwenda Dodoma na hatahusishwa kwenye programu yoyote ya timu mwezi huu wa Machi. Aliuambia mtandao wa Binzuberry.
Gembe amesema kwamba wanataka Mwanjali aendelee kupatiwa matibabu hadi awe fiti kabisa, ili akirejea iwe amerudi rasmi kuisaidia timu.

“Tunataka apone vizuri kabisa ndiyo arejee uwanjani. Kwa hiyo Machi yote hatakuwemo kwenye programu za timu,”amesema Gembe.
Mwanjali aliumia goti katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Prisons Februari 11, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba ikishinda 3-0.

Mwanjali aliye katika msimu wake wa kwanza Simba SC, alitolewa kwa machela siku hiyo na nafasi yake kuchukuliwa na kiungo Mwinyi Kazimoto dakika ya 62.
Post a Comment
Powered by Blogger.