Bulembo kutogombea tena uenyekiti wazazi

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Alhaji Abdallah Bulembo ametangaza kutogombea tena nafasi hiyo kwenye uchaguzi wa Jumuiya hiyo unaotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu.
Jumuiya za Chama Cha Mapinduzi (CCM) zinatarajiwa kufanya uchaguzi mwaka huu. Hivi karibuni Rais John Magufuli alimteua Bulembo kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza mjini hapa katika mkutano wa dharura wa Jumuiya hiyo, Bulembo alisema ameamua kukaa pembeni na kuwaachia wengine wagombee katika nafasi hiyo, kwani uongozi ni kupokezana kijiti.
Alisema yeye si king’ang’anizi wa madaraka na ndio maana nafasi nyingi za uongozi amekuwa akizishikilia na kuziachia ili wengine wapate fursa ya kuongoza.
“Sitagombea tena mwaka huu, nang’atuka kuwa mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi sasa ni wakati wenu kugombea. Huu ni mwaka wa uchaguzi, msiulize ni kwanini? na wala hoja si ubunge ni kawaida yangu na historia yangu,” alisem Bulembo.
Alisema amepata kuwa diwani kwa miaka 15 na alipotaka kuondoka kwenye nafasi hiyo, watu wakaanza kuhoji kwanini anafanya hivyo.
“Kuna wakati unatakiwa kuwapa fursa na watu wengine kuongoza nimeongoza FAT (Chama cha Soka Tanzania) niliondoka na kuwaachia wengine,’’ alisema na kuongeza kuwa, anaondoka ndani ya jumuiya hiyo akiicha ikiwa imara.
Pamoja na hayo alisema mwaka huu ni wa uchaguzi hivyo wale watakaogombea wanatakiwa kujipima kama kweli wanafaa kutokana na utendaji kazi wao. Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), ambayo ni jumuiya nyingine ya CCM, Sophia Simba naye alitangaza kutowania tena wadhifa huo.
Post a Comment
Powered by Blogger.