BODABODA, BAJAJ SASA ZATUMIKA KUFANIKISHA MICHEPUKO DAR

Kuna msemo usemao “sikio halilali njaa”, ndivyo ilivyo jijini Dar es Salaam ambako kuna kila aina ya matukio, hasa ya kijamii.
Lakini, Mwananchi haikutaka kuishia kusikia tu, bali kufanya uchunguzi wa shughuli za huduma ya usafiri wa bodaboda na bajaji.
Na ilichobaini ni jinsi madereva wa vyombo hivyo vya moto vinavyofanikisha wanaume au wanawake kutoka nje ya ndoa, maarufu kama kuchepuka.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuzidi kuongezeka kwa tabia hiyo ya ukosefu wa uaminifu katika ndoa kunakorahisishwa na vyombo hivyo vya usafiri, hasa bodaboda na bajaj ambazo ni za gharama nafuu.
Wanandoa wengi, hasa wanawake, walio na wapenzi wa nje (michepuko), hutumia usafiri huo kufika eneo la miadi na kurudi nyumbani kutokana na kuwa wa bei nafuu na unaotumia muda mfupi kutoka eneo moja hadi jingine.
Kwa kawaida, nauli ya bodaboda kwa umbali wa hadi kilomita mbili, ni Sh1,000 wakati usafiri wa bajaj, ambazo zina usiri zaidi kutokana na kuzungushiwa turubai, gharama yake hufikia hadi Sh5,000 kwa umbali huo.
Tofauti na gari ndogo za abiria, vyombo hivyo viwili haviathiriwi na foleni za magari kutokana na uwezo wake wa kujipenyeza pembeni au kupita katikati ya barabara na pia kutosimama kwenye taa za kuongozea magari, hivyo kuwa usafiri wa haraka unaoweza kufanikisha uovu huo.
“Ni kweli usafiri huu unatumiwa zaidi na watu wanaochepuka. Si wanawake tu hadi wanaume,” alisema dereva wa bodaboda aliyejitambulisha kwa jina la Simon Mussa ambaye anafanya kazi zake eneo la Ubungo.
Alisema kwa uzoefu wake, wanawake wengi aliowahi kuwabeba wanaonekana wanafanya hivyo kwa ajili ya kujipatia fedha za kukidhi mahitaji yao, hasa kulipia marejesho ya mikopo au michango ya vicoba ambayo ni ya fedha kidogo na mara nyingi hufanywa kila wiki.
“Mwanamke ana vicoba zaidi ya vitano, huku anadaiwa kupeleka mrejesho na kule anadaiwa. Akimwomba mume, naye pesa hana. Mwisho wa siku mwanamke anatafuta wa kumpa Sh10,000 au Sh5,000,” alisema Hamis Abdalah dereva teksi wa Tabata.
“Nimewahi kumbeba mwanamke, nilikuwa nampeleka gesti (nyumba ya kulala wageni) moja sitaitaja. Nikiwa naye kwenye gari, muda wote huyo mama alikuwa akilalamika kuhusu madeni ya vicoba akaniambia anadaiwa Sh300,000,” alisema.
Alisema alipomfikisha alimkuta anasubiriwa na kijana mdogo ambaye alimuona ana umri ambao angeweza kuwa mtoto wa huyo mama.
“Ukimtazama huyo kijana ana uwezo kifedha. Alimlipia nauli ya teksi ya Sh25,000 kisha wakaingia gesti,” alisema.
“Kwa kumwangalia tu yule mama moja kwa moja nilijua yule kijana ni mchepuko maana alikuwa na woga na wasiwasi hata alipokaribishwa.”
Alisema aliacha namba kwa miadi ya kumrudia huyo mama baadaye. Dereva huyo alisema baada ya saa moja na nusu, alipigiwa simu na kumfuata yule mwanamke ili amrudishe nyumbani.
“Cha kushangaza mama aliniomba nimshushe njiani akachukua usafiri wa bodaboda licha ya kuwa nilipewa nauli ya kumfikisha hadi nyumbani,” alisema.
Dereva mwingine wa bodaboda anayefanya shughuli zake Sinza jijini Dar es Salaam, Suleiman John alisema ni vigumu kuthibitisha kama abiria wako ni mke au mume wa mtu, lakini akasema chombo chake hutumika kuwapeleka wanaume na wanawake sehemu anazohisi ni za kuchepuka.
“Wapo wanawake wanaochepuka na wapo wanaume pia wanachepuka, tena hawa huchepuka na wasichana wadogo, hasa wanafunzi au wafanyakazi wa ndani. Lakini wanaoongoza ni wanawake na wengi wanatembea na vijana wadogo,” alisema John.
“Kwa siku unaweza kubeba wanawake sita hadi 10 unawapeleka nyumba za kulala wageni na kuwarudisha. Huwa tunajua wanawake wanaokwenda kwenye michepuko huwa hawalalamikii gharama. Ukimtajia tu anakubali sababu hulipiwa na michepuko,” alisema John.
“Mimi niliwahi kumbeba mke wa mtu. Huyo dada nilikuwa najuana na mume wake ila yeye alikuwa hanijui. Nikiwa naye kwenye gari simu yake iliita akaniomba nizime redio na nisimamishe gari,” alisema Jeffa Juma.
Juma alisema baada ya kusimamisha gari aliongea na simu kwa sauti ya mahaba akisema “niko nyumbani baby (mpenzi) nimelala,” alisema akimnukuu mwanamke huyo.
Dereva mwingine wa bodaboda kutoka Ubungo, Msafiri Kharimu alisema mara nyingi wanaume wanaochepuka ni wale wenye uwezo na huwa hawatumii usafiri wa jumuiya, wao wanakuwa na usafiri wao binafsi. “Hawa huwapigia wapenzi wao simu na kuwaelekeza walipo, anaweza kuja mwanamke anakwambia nipeleke gesti fulani au hoteli fulani, Ukimfikisha unakuta mwanaume yupo na gari yake anamsubiri,” alisema.

Wanawake na wanaume wanena
Mtaani, wakazi wanaonekana kuzoea kushuhudia vitendo hivyo.
“Ni kweli wanawake wanachepuka na wengi wanatumia usafiri wa bodaboda na bajaji. Hawatumii sana teksi,” anasema Asha Abdallah mkazi wa Mabibo.
“Unajua haya mambo yanafanywa kwa kificho na usiri. Mtu hawezi kuchukua teksi kwa sababu anahofia kuchelewa kutokana na foleni. Siku hizi wengi wanatumia bodaboda au bajaji ili kuwahi anakokwenda na atarudi.”
Lakini Fikiri Said, ambaye ni mkazi wa Ubungo, anakwenda mbali kiasi cha kumtuhumu mkewe kuwa huenda anafanikisha kuchepuka kwake kwa kutumia bodaboda.
“Nahofia huwa nikienda kazini kuna mahali anakwenda kuchepuka na usafiri wake ni bodaboda. Kwa maana mpaka huwa ninajiuliza anaenda wapi na ukiangalia namwachia pesa kidogo ya kununua mboga?” alisema.
Post a Comment
Powered by Blogger.