Viongozi watatu kwimba wakamatwa na polisi kwa kumlinda mmiliki wa mitambo ya gongo.

Zaidi ya lita 300 za pombe haramu aina ya gongo, mapipa 13 na mitambo 7 inayotumika kutengenezea pombe hiyo, imekamatwa katika kijiji cha nyang’honge wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, huku viongozi watatu akiwemo afisa mtendaji wa kijiji hicho wakikamatwa kwa agizo la mkuu wa wilaya hiyo kwa tuhuma za kuhusika kumtorosha mmiliki wa mitambo ya gongo.
Mkuu wa wilaya ya Kwimba Mhandisi Mtemi Simeon Msafiri, amesema katika operesheni hiyo iliyofanywa na kamati ya ulinzi na usalama wilayani humo wamegundua kuwepo kwa kiwanda kikubwa kinachotengeneza pombe haramu ya gongo inayosafirishwa katika maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya wilaya hiyo.

Katika operesheni hiyo, mkuu wa wilaya ya Kwimba Mhandisi Mtemi Msafiri, ameliagiza jeshi la polisi kuwakamata afisa mtendaji wa kijiji cha Nyang’honge Bernard Maige, Mwenyekiti wa kitongoji cha Nyang’honge ‘A’ Kulwa Juma pamoja na mMenyekiti wa kijiji hicho Enos Masanja ambaye ametoroka, viongozi hao wana tuhuma za kumtorosha mmiliki wa mitambo ya kutengenezea gongo Bw. Solo Madata ili asitiwe nguvuni na polisi.

Baadhi ya wakazi wa eneo ilipokamatwa gongo hiyo pamoja na mitambo yake, wamesema kuwa wao siku zote hawakuwahi kujua  kama pombe hiyo haramu ilikuwa ikipikwa katika eneo hilo.

Wilaya ya Kwimba kuanzia mwezi Agosti mwaka jana, ilianza kutekeleza zoezi la kuwasaka watu wanaojihusisha kutengeza na kutumia pombe haramu aina ya gongo, wakiwemo watumiaji wa madawa ya kulevya hususani bangi zoezi ambalo mkuu wa wilaya hiyo amesema litakuwa endelevu.
Post a Comment
Powered by Blogger.