SHAHIDI AELEZA WALIVYOMNASA MSHTAKIWA MENO YA TEMBO

Shahidi ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jinsi polisi walivyomnasa mshtakiwa Salvius Matembo anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa kujihusisha na biashara ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh5.4 bilioni.
Shahidi huyo kutoka Idara ya Upelelezi na Makosa ya Jinai ya Polisi, Koplo Emmanuel John akiongozwa na Wakili wa Serikali, Paul Kadushi kutoa ushahidi jana alidai kuwa Mei 14, 2014 akiwa ofisini na wenzake, waliitwa na msaidizi wa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai na kupewa jukumu la kumtafuta Matembo.
Alidai alipata maelekezo kuwa Matembo anapatikana Sinza na Kimara.
Koplo John alidai Mei 21, 2014 mchana akiwa karibu na maeneo ya ofisi yake akipata chakula, alipigiwa simu kuwa Matembo yupo baa ya Kilimanjaro iliyopo Sinza.
Alidai kuwa aliwasiliana na mtu aliyepiga simu na kumpeleka kwenye baa hiyo na kumuonyesha mshtakiwa wanayemtafuta.
Baada ya kuonyeshwa walimfuata eneo alipokuwa amekaa na kujitambulisha kuwa yeye ni polisi na kumuamuru kuwa yupo chini ya ulinzi kwa kujihusisha na biashara ya meno ya tembo.
Alidai kuwa mshtakiwa huyo baada ya kuwekwa chini ya ulinzi alitaka kutoroka lakini kwa kuwa walijipanga, walimkamata.
Alidai waliwasiliana na mkubwa wao na kuwaelekeza wampeleke Kituo cha Polisi Kijitonyama na kwamba wakati wakiwa njiani aliwashawishi kwa kuwapa rushwa ili wamuachie lakini walikataa.
Alidai baada ya kumfikisha polisi aliingia mapokezi ambako walimkuta Sajenti Beatus na kumkabidhi.
Kesi hiyo itaendelea leo kwa ajili ya kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni raia wa China, Yang Feng Glan (66), anayedaiwa kuwa malkia wa meno ya tembo na Manase Philemon.
Washtakiwa hao wanatetewa na Wakili Masumbuko Lamwai, Jeremiah Mtobesya na Hassan Kihangio.
Washtakiwa hao wanadaiwa kati ya Januari Mosi, 2000 na Mei 22, 2014 walijihusisha na biashara ya nyara za Serikali.
Katika kipindi hicho washtakiwa wanadaiwa kufanya biashara ya vipande 706 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 1,889 zenye thamani ya Sh13 bilioni bila ya kuwa na leseni iliyotolewa na Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Post a Comment
Powered by Blogger.