LWANDAMINA AIPIGA MKWARA SIMBA

JOTO la pambano la watani wa jadi linazidi kuongezeka baada ya wachezaji na uongozi wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga kuahidi watacheza kwa kiwango cha juu kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika mechi dhidi ya Simba.

Mechi hiyo itakayofanyika kesho kutwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini, Dar es Salaam.

Katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyofanyika Oktoba Mosi mwaka jana, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1, Shiza Kichuya akiisawazishia Simba katika dakika ya 87.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina, alisema kuwa kikosi chake kimeiva na wanachosubiri ni kutekeleza maelekezo waliyowapa ya kusaka pointi tatu muhimu.

Lwandamina ambaye mechi yake dhidi ya Simba kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi alikubali kichapo, alisema kuwa anataka kuona wanaibuka na ushindi ili safari yake ya kutwaa ubingwa na Yanga kuweka rekodi ya kushinda taji la Ligi Kuu Bara kwa mara ya tatu mfululizo wanalitimiza.

"Ni mechi kubwa na muhimu kwa kila upande, ila Yanga tutaingia uwanjani tukifahamu tunachokwenda kukifanya, ushindi ndiyo jambo tunalolitarajia, tunataka pointi tatu muhimu," nahodha msaidizi wa Yanga na kiungo wa kimataifa kutoka Rwanda, Haruna Niyonzima alisema jana.

Naye Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, Salum Mkemi, alisema kila mchezaji amejipanga kufanya vizuri kwenye mchezo huo na kuhakikisha timu yake inaondoka na ushindi mnono ili kulinda heshima yao, viongozi, wanachama pamoja na timu yao.

“Tutaifunga Simba magoli mengi sana, na mwaka huu ni lazima ishuke daraja kwa sababu tutawafunga magoli mengi kipindi cha kwanza, hivyo hawatarudi kipindi cha pili na kwa sheria za TFF ( Shirikisho la Soka Tanzania), timu isiporudi uwanjani inashushwa daraja,” alisema.

Kuhusu hali ya straika, Donald Ngoma, kuwa katika hatihati ya kutocheza mechi hiyo, kiongozi huyo alisema hawana wasiwasi wowote kwa sababu kikosi chao kina washambuliaji wengi wenye uwezo wa kuifunga Simba.

Aliongeza kuwa benchi la ufundi la Yanga linamuandaa mshambuliaji huyo kutoka Zimbabwe kwa ajili ya kuwavaa Zanaco katika mechi ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayofanyika Machi 11 hapa jijini na marudiano wiki moja baadaye huko Lusaka, Zambia.
Post a Comment
Powered by Blogger.