GWAJIMA NA YUSUF MANJI WAKESHA NA POLISI DAR

Ni kama shughuli zilisimama kwa saa kadhaa katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam wakati watu wawili maarufu nchini, Askofu Josephat Gwajima na mfanyabiashara Yusuf Manji waliporipoti kituoni hapo wakitaka wahojiwe.
Wawili hao, pamoja na wengine 63 walitakiwa waripoti kituoni hapo leo kwa ajili ya kuhojiwa kuhusu biashara ya dawa za kulevya, utumiaji au kama wana taarifa zinazoweza kusaidia Jeshi la Polisi kukomesha biashara hiyo haramu.
Wito huo ulitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye juzi aliita waandishi ofisini kwake na kutaja orodha ya watu 65, wakiwemo wanasiasa, wafanyabiashara na viongozi wa dini.
Lakini, Manji, ambaye ni mwenyekiti wa moja ya klabu kubwa nchini ya Yanga, na Askofu Gwajima, anayeongoza kanisa la Ufufuo na Uzima, walienda kituoni hapo jana na walisikindikizwa na mashabiki na waumini wao.
Manji, ambaye ni Mwenyekiti wa Kampuni ya Quality Group, alifika kituoni hapo saa 4:54 asubuhi akiwa wa kwanza na alifika akiwa ndani ya gari aina ya Range Rover ya rangi nyeusi, akifuatana na watu wawili alioingia nao kituoni.
Dakika chache baada ya kuingia, Manji alitoka ndani na akawa anazungumza na watu waliovalia sare na wengine kiraia na baada ya muda aliingia tena ndani ya kituo.
Ilipotimu saa 6:10 mchana, Manji alitoka na kuonekana anaondoka, lakini alipofika getini askari walimfuata na wakarudi naye ndani.
“Mzuie, mzuie, mzuie,” alisikika mmoja wa polisi akisema wakati Manji akionekana kuondoka. Mfanyabiashara huyo alitii amri na kurudi kituoni.
Wakati Manji akiwa ndani ya kituo hicho, saa 7:33 mchana Askofu Gwajima aliwasili akiambatana na watu wapatao 10 walioonekana kuwa ni viongozi wa kanisa hilo na wote wakaingia kituoni.
Wakati viongozi hao wakiwa ndani, saa 8:00 mchana waumini takribani 20 walionekana kuwa ni wa kanisa la Ufufuko na Uzima walifika wakiwa wamevalia suti nyeusi. Waumini hao wa kike na kiume walikusanyika nje ya kituo hicho na kujipanga mstari nje ya geti la kuingilia kituoni, lakini askari waliwazuia na kuwataka kukaa mbali na eneo hilo ili wasubiri hatma ya askofu wao.
Taarifa kutoka ndani ya kituo hicho zilisema kuwa watuhumiwa hao hawakutoa maelezo yoyote kwa sababu Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Siro alikuwa kwenye kikao ofisini kwa Makonda.
Eneo hilo pia lilifurika mashabiki kadhaa wa klabu ya Yanga waliokuwa wakifuatilia hatma ya Manji.
Baada ya ukimya uliotawala eneo hilo huku waandishi wa habari wakifuatilia matukio hayo kwa mbali kutoka nje, Manji na Gwajima walionekana wakitoka kituoni saa 10:27 jioni na wote kupanda gari dogo jeupe aina ya Toyota Land Cruiser na kuondoka.
Baada ya kurejea, Kamanda Siro aliwaambia waandishi wa habari kuwa hangeweza kuzungumzia suala hilo jana.

Gwajima amvaa Makonda
Awali, Gwajima alizungumza na waumini wa kanisa lake na kumuomba Rais John Magufuli ambadilishe kazi Makonda, akimsifu kuwa ni mchapakazi, lakini hawezi kazi ya utawala kutokana na ama kutokomaa au kutokuwa na uzoefu.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya kuongea na waumini, Askofu Gwajima alisema kitendo cha Makonda kumtaja hadharani akihusishwa na dawa za kulevya kinaonyesha ana nia ovu na kanisa hilo.
“Sisemi Magufuli amfukuze kazi, hapana, Makonda ni jasiri na mchapakazi, lakini kazi ya utawala, kuongoza watu imemshinda atamharibia Rais,” alisema.
“Usalama wa Taifa watakuwa wanafahamu kama Askofu Gwajima anahusika au hahusiki kwa namna moja ama nyingine na dawa za kulevya. Kitendo cha Makonda kunitaja kupitia vyombo vya habari kinaonyesha ana chuki na mimi na hajui masuala ya utawala.
“Hivi hafahamu kwamba nina waumini zaidi ya 70,000, nina makanisa 400 na maaskofu 25. Ameshindwa vipi kuchunguza na kuniita hadi atangaze kwenye vyombo vya habari?”
Alisema sababu nyingine ya kutaka Rais Magufuli ambadilishe kazi ni kutokana na viongozi wa Serikali hivi sasa kufanya kazi kwa hofu.
“Mawaziri, wakuu wa mikoa wanaogopa wanaposikia sauti ya Makonda, wanadhani kila anachofanya ametumwa na Rais Magufuli. Si kweli anawatisha tu huyo,” alisema.
“Magufuli amekuwa akimpongeza Makonda kwa kazi nzuri anazozifanya, lakini si kila anachofanya anatumwa na Rais.”
Aliwataka viongozi wengine kutokuwa na hofu na Makonda kwa kuwa anachokifanya ni kuwatisha wenzake kwa kutumia jina la Rais.
“Nimekuwa nikijiuliza sifahamu chochote kuhusu dawa za kulevya, huyu Makonda ananipakazia hivi ili kumfurahisha nani?” alihoji.

Wivu na chuki binafsi
Askofu Gwajima alisema hivi karibuni walikuwa kwenye mechi ya soka kati ya viongozi wa dini na wa serikali ambayo yeye na Makonda walicheza timu moja.
“Kwa kuwa nilichelewa, niliamua kutumia helikopta hadi uwanjani lakini wakati tukicheza mpira, Makonda alikuwa ananiangalia kwa jicho la chuki mpaka nikawa nashangaa. Sasa leo nimeamini kijana mwenzangu ana chuki binafsi,” alisema.
Alisema Makonda anatakiwa kufahamu kwamba si kila anayefanikiwa kiuchumi anakuwa anajihusisha na dawa za kulevya.
Askofu Gwajima alisema ana shahada ya uzamivu ya filosofia (PhD) na hulipwa dola 1,000 za Kimarekani (sawa na zaidi ya Sh2.2 milioni) kwa saa anapofanya uhadhiri vyuoni.
“Nimetoka Japan ambako nilikaa miezi mitatu, unadhani nitachuma kiasi gani?” alihoji.
“Sasa kijana mwenzangu Makonda asiwe na chuki binafsi, bali angeniuliza unapataje fedha, lakini si kuvunja heshima yangu niliyoijenga siku nyingi.”
Alisema hajawahi kunywa pombe, kuvuta sigara na wala hajui dawa za kulevya zikoje.

Makonda kanisani
Gwajima alisema Makonda akiwa na spika wa zamani wa Bunge, Marehemu Samuel Sitta waliwahi kufika kanisani kwake kuombewa.
“Nilimkaribisha Makonda madhabahuni na akazungumza na waumini akisema ni heshima kubwa kupata nafasi ile na tulisali pamoja. Je, kipindi kile hakuhofia kuwa nahusika na dawa za kulevya?” alihoji.
Nisirudishwe kwa Lowassa
Alipoulizwa kama patashika anazopata zinatokana na kuwa karibu na aliyekuwa mgombea wa Chadema, Edward Lowassa, mchungaji huyo alisema anashangaa kuona anarudishwa kwa mtu aliyeona anafaa kuwa Rais.
“Wakati wa uchaguzi kila mtu aliona mtu aliyefaa kuwa Rais na mimi niliona Lowassa ndiye aliyekuwa anafaa kuwa Rais,” alisema Gwajima.
“Lakini bahati nzuri Lowassa hakuchaguliwa na badala yake amechaguliwa Magufuli ambaye anafanya kazi ambayo ingeweza kufanywa na wapinzani. Kwa hiyo namuunga mkono. Nashangaa kwamba mimi namuunga mkono, lakini wanazidi kunirudisha kwa yule.
“Mimi si mnafiki. Wakati Rais Jakaya Kikwete akiwa madarakani niliikosoa sana Serikali yake, lakini nashukuru sasa Magufuli anafanya kazi zilizotarajiwa na Watanzania wengi, ndiyo maana mara nyingi nampongeza.”
Post a Comment
Powered by Blogger.