AFYA YA MANJI YAIMARIKA, VITA DAWA ZA KULEVYA YAENDELEA

Afya ya mfanyabiashara maarufu, Yusuf Manji inaendelea vizuri baada ya jopo la madaktari wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), kuendeleza matibabu yake baada ya kupata dhamana akitokea mahakamani.
Hii ni mara ya pili kwa Manji kuugua ghafla na kulazwa hospitalini hapo, mara ya kwanza ilikuwa polisi alipokuwa akihojiwa ambako aliugua ghafla jioni na alipelekwa JKCI.
Akizungumza jana na gazeti hili, Mkurugenzi wa Tiba wa JKCI, Dk Peter Kisenge alisema walimpokea Manji akitokea mahakamani na kwamba anaendelea na matibabu na afya yake inazidi kuimarika.
“Tunaendelea kumpatia matibabu yanayohitajika kwake kwa sasa na anaendelea vizuri,” alisema Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya moyo katika taasisi hiyo.
Taarifa za ndani zaidi zilidai kuwa Manji kwa sasa anasumbuliwa na ugonjwa wa moyo. Hata hivyo, madaktari wa JKCI bado wameendelea kusita kuzungumzia tatizo linaloisumbua afya ya Mwenyekiti huyo wa klabu ya Yanga.
Hata hivyo, mara baada ya kufikishwa hospitalini hapo, Manji alikutana na wingi wa wagonjwa kiasi cha kumfanya alazwe na wagonjwa wengine baada ya vyumba vya wagonjwa mashuhuri kujaa.

Vita dawa za kulevya
Vita dhidi ya dawa za kulevya imeendelea kupamba moto nchini hasa baada ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya kukabidhiwa majina 97 ya wauzaji wakubwa, pia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuzindua Baraza la Taifa kukabiliana na uhalifu huo.
Ni vita ambayo haipiganwi Tanzania pekee, Kenya kuna watuhumiwa wamefikishwa mahakamani nchini Marekani, Rais Donald Trump ameanza mapambano hayo huku nchini Ufilipino Rais wake, Rodrigo Duterte aliishaanza kwa kuwapiga risasi watumiaji na wauzaji.
Kinachotokea sasa nchini ni mwendelezo wa kilichoanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliyeanza na wasanii na baadaye akataja watu 65 na hivi karibuni alikabidhi majina 97 kwa Kamishna Mkuu Rogers Sianga akisema wanaweza kuwa na taarifa zinazoweza kusaidia katika vita hiyo.
Pia, wakati Makonda akikabidhi majina 97 kwa Kamishna Sianga, alitoa amri ya kukamatwa Chid Mapenzi (Rashid Said) na kesho Jumatatu kwa mujibu wa Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Siro watuhumiwa watatu wa dawa za kulevya, Agnes Gerald ‘Masogange, Chid Mapenzi na Walid Nasher watafikishwa mahakamani.
Wakati Makonda akikabidhi majina hayo, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima alitangaza vita dhidi ya Makonda baada ya kumtaja kwenye orodha ya wanaojihusisha na uhalifu huo.
Askofu Gwajima alisema hayo katika ibada ya Jumapili iliyopita iliyofanyika kanisani kwake Ubungo, baada ya kuachiwa na polisi, alitumia fursa hiyo kuwaeleza waumini wake na Watanzania kilichotokea tangu aliporipoti polisi.

Ilivyokuwa Jumatatu
Akizungumza katika kikao alichokiita cha awamu ya tatu ya kutaja majina wanaojihusisha na dawa za kulevya, kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mwalimu Nyerere, Makonda alisema ana majina mengine 97 baada ya majina ya wasanii na yale 65.
Awamu ya kwanza ilikuwa mapema mwezi huu, Makonda alitangaza hadharani majina ya wasanii aliodai wanajihusisha na dawa za kulevya akiwataka wafike kituo cha polisi cha kanda maalumu kwa ajili ya mahojiano huku awamu ya pili akiwataja wanasiasa na viongozi wa dini akiwataka pia wafike katika kituo hicho.
Makonda alisema kundi hilo la tatu, limewahusisha baadhi ya watu ambao wako ndani ya nchi aliodai wana mtandao na watu wa nje ambao kuingiza kilo 2,000 au 5,000 siyo jambo gumu kwao.
Siku hiyo hiyo, Kamishna Sianga alitumia fursa hiyo kusema kuwa atawaagiza maofisa wa Serikali waliopitisha tani 21 za viuatilifu vya kutengeneza dawa za kulevya kukamatwa na kuhojiwa na wakibainika watachukuliwa hatua.

Jumanne
Jina la Makonda lilitawala kila kona nchini ikiwamo kutajwa katika mkutano wa Bunge uliomalizika hivi karibuni na kujadiliwa zaidi katika mitandao ya kijamii, ikiwamo makundi ya WhatsApp na mingine.
Wakati mkuu wa mkoa huyo akitawala kila kona, mfanyabiashara Manji aliyekuwa yupo hospitali kwa ajili ya matibabu akiwa chini ya ulinzi, alikumbwa na mkasa mwingine baada ya Kampuni ya Quality Group kudaiwa kuajiri wageni 25 wasiokuwa na vibali vya kufanya kazi nchini.
Ofisa Uhamiaji wa Dar es Salaam, John Msumule aliwaeleza wanahabari kuwa uchunguzi uliofanywa na idara hiyo ulibaini watu 128, waliajiriwa katika kampuni tofauti ambazo ni miongoni mwa kampuni 20 zilizo chini ya Quality Group.
Msumule alisema kutokana na hali hiyo, wamepanga kumshtaki Manji kama mmiliki wa Quality Group kutokana na tuhuma za kuajiri raia wa kigeni wasio kuwa vibali, na kutoa wito kumtaka kuripoti uhamiaji baada ya kutoka polisi

Jumatano
Manji alitoka hospitali Jumatano saa 10.00 jioni baada ya kupatiwa matibabu kwa siku tatu, ingawa haikufahamika alikwenda nyumbani au polisi. Mbali na hilo, siku hiyo vyombo vya habari viliripoti kukamatwa kwa mwanadada anayetamba katika video za nyimbo mbalimbali za bongo fleva, Agnes Gerald ’Masogange’ kwa tuhuma za kujihusisha na dawa za kulevya.

Alhamisi
Manji alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu, akitokea hospitalini alikokuwa amelezwa baada ya kuugua ghafla akiwa katika kituo cha polisi.
Manji alipandishwa kizimbani kwa tuhuma za kutumia dawa za kulevya aina ya heroin, hata hivyo mfanyabiashara huyo alikana shtaka hilo.
Katika kesi hiyo, Manji aliwakilishwa na mawakili watatu ambao ni Alex Mgongolwa, Hudson Ndusyepo na Jeremiah Mtobeya wakati upande wa Serikali uliwakilishwa na Osward Tibabyekoma , Kishenyi Mutalemwa (Wakili Mwandamizi wa Serikali) na Shedrack Kimaro.
Tibabyekomwa alidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na akaomba kesi hiyo ipangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika.
Wakili Mgongolwa kwa niaba ya jopo la mawakili wa Manji aliomba Mahakama kumpa dhamana mteja wao kwa sababu shtaka linalomkabili kisheria linadhaminiwa na kwamba apewe masharti nafuu.
Hata hivyo, Tibabyekoma aliiambia mahakama hiyo kuwa hawana pingamizi kwa sababu shtaka hilo linadhaminika kisheria.
Baada ya maelezo hayo, Manji alitakiwa kutimiza masharti ya dhamana kwa kuwa na mdhamini mmoja anayeaminika ambaye atasaini hati ya dhamana ya maneno ya thamani ya Sh10 milioni.
Manji alidhaminiwa na Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa ambaye aliikamilisha kazi hiyo na Manji kuachiwa huru.

Ijumaa
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwataka wakuu wa mikoa nchini na wilaya kutotangaza majina ya watuhumiwa kabla ya kufanyika uchunguzi na kujiridhisha.
Majaliwa alitoa kauli wakati akizindua Baraza la Taifa la Dawa za Kulevya, hafla iliyofanyika ofisini kwake Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wakuu wa mikoa mbalimbali wakiwamo wakuu wa majeshi ya ulinzi na usalama. Aliwataka wakuu wote wa mikoa kushiriki vita hiyo kwa kuwa wao ni wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama kwenye maeneo yao ya kazi, pia kwa kuzingatia sheria na kanuni wana uwezo huo.
Post a Comment
Powered by Blogger.