AFYA YA MANJI YAANZA KUIMALIKA

Taarifa kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), alikolazwa zinasema hawezi kuruhusiwa kwa sasa.
Msemaji wa JKCI, Anna Nkinda alisema jana kuwa baada ya vipimo, madaktari wameshauri aendelee na mapumziko mpaka watakapoona inafaa kumruhusu.
Mkurugenzi wa Tiba wa JKCI, Dk Peter Kisenge alisema mgonjwa huyo anahitaji vipimo zaidi hivyo ataendelea kubaki katika hospitali hiyo.
Wiki iliyopita, Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Dar es Salaam, John Msumule aliitisha mkutano wa waandishi wa habari na kumtaka kuripoti katika idara hiyo kwa madai kwamba kampuni yake imeajiri wageni 25 wasiokuwa na vibali halali vya kuishi nchini.
Katika mkutano huo Msumule alisema, “Tumekamata pasipoti 126, tumechambua pasipoti 25 hawana vibali vya kufanyia kazi, kwa hiyo wanafanya kazi kinyume na taratibu. Wote hawa hatua zitachukuliwa watapelekwa mahakamani.
“Lakini niseme ukweli, hawa hawatapelekwa peke yao mahakamani, lazima Yusuf Manji ambaye ndiye mwajiri wa watu hawa, ambaye ndiye mmiliki wa kampuni hii lazima afikishwe mahakamani kujibu shtaka la kuajiri wageni wasio na vibali,” alisema.
“Jana ilikuwa tumkamate alale mahabusu na leo tumpeleke mahakamani, bahati mbaya wakati tunafanya zoezi la kwenda kumkamata tukapewa taarifa kwamba amelazwa hospitalini hadi sasa. Mara tu akitoka aripoti haraka ofisi hii ili tumuunganishe kwenye kesi hii ya kuajiri watu wasio na vibali.”
Hata hivyo, katika tangazo lililotoka katika gazeti la The Citizen, Aprili 13, 2016, Manji aliutangazia umma kwamba atastaafu uongozi katika kundi la kampuni za Quality kuanzia Julai 15, 2016 na kubaki kuwa mwenyekiti na mshauri mkuu mwenye uamuzi wa mwisho katika Baraza la Uongozi na Ofisa Mtendaji Mkuu.
Pia, katika gazeti hili lilitolewa tangazo jingine Desemba 20, 2016 kumpongeza Arif Sheikh kuwa msimamizi wa ofisi za Quality Group katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akichukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Manji.
Tangazo hilo lilieleza kwamba Manji atakuwa akizunguka kusimamia kampuni za Quality Group zilizo katika nchi 28 akiendelea na cheo chake cha mwenyekiti na mshauri mkuu mwenye uamuzi wa mwisho katika Baraza la Uongozi na Ofisa Mtendaji Mkuu.
Tofauti na alipofikishwa hospitalini hapo kwa mara ya kwanza Februari 12 ambako kulikuwa na ulinzi mkali wa askari kanzu na waliokuwa wamevaa sare na hata Februari 16 baada kupata dhamana na kuwa chini ya maofisa wa Uhamaji, jana hapakuwa na ulinzi wowote.
Post a Comment
Powered by Blogger.