UBALOZI WA NORWAY WASAINI MKATABA WA BIL. 10.6 NA UN KWA AJILI YA KUWASAIDIA WAKIMBIZI, KIGOMA

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Kwa kutambua hali ya kimaisha ambayo inawakabili wakimbizi waliopo mkoani Kigoma, ubalozi wa Norway nchini umesaini mkataba wenye thamani ya dola milioni 4.8 (Tsh. Bilioni 10.6) na Umoja wa Mataifa (UN) kupitia Mpango wa Misaada ya Maendeleo (UNDAP 2) kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi waliopo nchini.

Akizungumza katika hafla ya utiliaji saini mkataba huo, Balozi wa Norway ncini, Hanne-Marie Kaarstad alisema pesa ambazo wamezitoa zinalenga zaidi kuwasaidia wakimbizi waliopo Kigoma ili waweze kuwa na shughuli za kuwasaidia na hasa kwa wanawake na watoto.

"Kwetu ni jambo muhimu kushirikiana na UN kwa ajili ya kuwalinda watu ambao wanaingia nchini kutoka nchi jirani, tulichangia katika mpango wa kwanza wa misaada ya maendeleo na sasa tumejiunga katika mpango mwingine wa maendeleo wa 2016-2021,

"Tunafahamu Kigoma mwaka jana mwezi Mei ilipokea wakimbizi wengi kutoka Burundi na sasa tunaona ni vyema tukishirikiana na mashirika ya UN ili kuwasaidia na zaidi kwa wanawake na watoto na wote tunatambua kuwa wanawake ndiyo chanzo kikuu cha uchumi na hili sio Kigoma tu, maeneo yote ipo hivyo," alisema Kaarstad.

Nae Mratibu Mkuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN), Alvaro Rodriguez alisema ni jambo zuri kuona Norway inaendeleza ushirikiano na Tanzania na wao wamejipanga kuhakikisha wakimbizi wanaokusudiwa kunufaika na pesa hizo zinawafikia na kufanya kazi ambayo zimepangiwa kufanyika.

"Tunajivunia ushirikiano imara wa UN na Norway kwa kuwa tayari kusaidia watoto na wanawake , Norway imekuwa ikisaidia Tanzania na leo ni heshima kuona wakisaidia kwa mara nyingine,

"Sehemu ambazo zinakuwa na wakimbizi zina changamoto zake na hata kwa nchi kunapokuwa na wakimbizi kunashughuli za kijamii zinakuwa zinasimama, sisi kama UN tutashirikiana na serikali kufanya ambacho mnakilenga na kufikia malengo yaliyowekwa hadi 2021," alisema Rodriguez.

Aidha alisema msaada ambao umetolewa na ubalozi wa Norway utatekelezwa sambamba na malengo ya dunia ambayo ni pamoja na kumaliza umaskini, usawa wa kijinsia na uhifadhi wa mazingira.

Na Rabi Hume, MO BLOG
Balozi wa Norway, Mheshimiwa Hanne-Marie Kaarstad (kushoto) akisaini mkataba wa dola za Marekani milioni 4.8 (sawa na shilingi bilioni 10.6) na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez zilizotolewa na serikali ya Norway kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo nchini Tanzania kwa kipindi cha miaka miwili, katika hafla fupi iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ubalozi huo jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Zainul Mzige, MO BLOG)
Balozi wa Norway, Mheshimiwa Hanne-Marie Kaarstad (kushoto) wakibadilishana hati za mkataba wa dola za Marekani milioni 4.8 (sawa na shilingi bilioni 10.6) na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (kulia) katika ofisi za ubalozi wa Norway jijini Dar es Salaam.

Balozi wa Norway, Mheshimiwa Hanne-Marie Kaarstad (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari mara tu baada ya kuhitimisha zoezi la utiaji saini wa makubaliano hayo. Kulia ni Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez.
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (kulia) akiishukuru serikali ya Norway kwa mchango wao mkubwa katika kuwezesha Umoja wa Mataifa kutekeleza wajibu wake, huku akisema kwamba Norway imekuwa na mchango mkubwa katika programu mbalimbali za umoja huo nchini Tanzania. Kushoto ni Balozi wa Norway, Mheshimiwa Hanne-Marie Kaarstad.
Baadhi ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wakichukua kumbukumbu ya tukio hilo lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ubalozi wa Norway jijini Dar es Salaam.
Post a Comment
Powered by Blogger.