WANAODAIWA KUMUUA DADA WA BILIONEA MSUYA WAONGEZEKA

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
WATUHUMIWA wa mauji ya dada wa bilionea Erasto Msuya, Aneth Msuya wameongezeka baada ya mfanyabiashara
wa Arusha, Revocatus Muyela (40) kupandishwa kizimbani kwa tuhuma za mauaji hayo.
Muyela alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mwishoni mwa wiki na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Magreth Bankika.
Mshtakiwa anatuhumiwa kumuua dada wa mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite bilionea, marehemu Erasto Msuya, Aneth Msuya.
Kupandishwa kizimbani kwa mfanyabiashara huyo kunafanya idadi ya watu wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji hayo yaliyotokea Kibada, Kigamboni, Dar es Salaam, kufikia wawili baada ya kushitakiwa mke wa bilionea huyo, Miriam Msuya.
Mfanyabiashara huyo alisomewa shtaka la mauaji na Wakili wa Serikali, Diana Lukondo.
Diana alidai mshtakiwa huyo, Mei 25 mwaka huu, eneo la Kibada, Kigamboni, Dar es Salaam, alimuua Aneth.
Mshtakiwa hakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji bali husikilizwa na Mahakama Kuu.
Wakili alidai upelelezi haujakamilika na kuomba kuahirishwa kesi hadi tarehe nyingine kwa kutajwa.
Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 6, mwaka huu na mshtakiwa alirudishwa rumande hadi tarehe hiyo.
Agosti 24, mwaka huu, mke wa bilionea Msuya, Miriam Msuya alifikishwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Magreth, akikabiliwa na shtaka la mauaji ya wifi yake huyo.
Miriam (41), mfanyabiashara na mkazi wa Sakina kwa Idd, Arusha, alikamatwa Arusha na kusafirishwa hadi Dar es Salaam kwa ajili ya kusomewa shtaka hilo.
Mke wa bilionea huyo aliposomewa shtaka hilo hakutakiwa kujibu kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.
Miriam alipelekwa rumande hadi Septembaa 6, mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa tena.
Aneth, ambaye ni dada wa bilionea Erasto Msuya, aliuawa kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake eneo la Kibada block 16, Kigamboni.

Chanzo: Mtanzania
Post a Comment
Powered by Blogger.