SAMANI ZA OFISI YA MBOWE KUPIGWA MNADA NA NHC BAADA YA SIKU 14 ZA KULIPA DENI KUISHA

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


VIFAA vilivyokamatwa jana vya klabu ya usiku ya Bilicanas na ofisi ya gazeti la Tanzania Daima, vyote vinavyomilikiwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, vitapigwa mnada na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) siku 14 kuanzia jana, endapo atashindwa kulipa Sh. bilioni 1.2 za deni la pango la miaka 20.

Mbowe alikuwa mpangaji katika jengo la NHC lililopo makutano ya mitaa ya Mkwepu na Indira Gandhi, katikati ya jiji la Dar es Salaam.

Vyombo hivyo vilikamatwa jana na kampuni ya udalali ya Fosters Auctioneers and General Traders iliyopewa kazi ya kuondoa vifaa hivyo baada ya Mbowe kushindwa kulipa deni hilo ndani ya miezi miwili ya notisi ambayo shirika hilo lilikuwa limempatia.

Meneja wa Kitengo cha Kukusanya Madeni kutoka NHC, Japhet Mwanasenga aliyekuwa akisimamia ukamataji wa vyombo hivyo, alisema Mbowe ana muda wa wiki mbili kuanzia jana kulipa deni la Sh. bilioni 1.172 vinginevyo vitapigwa mnada.

Vifaa vilivyokamatwa ni pamoja na kompyuta, meza na viti.

Alisema taratibu zote zilifuatwa kabla ya kumuondoa mteja wao, ikiwamo notisi na kwamba vifaa hivyo vitashikiliwa kwa muda huo wa wiki mbili.

“Tunashikilia vyombo kwa muda wa wiki mbili na iwapo atashindwa kulipa vitapigwa mnada na dalali, (mdaiwa) akishindwa kulipa anapangishwa mwingine,” alisema.

Alisema shirika hilo linahitaji fedha kwa ajili ya ujenzi na uendelezaji wa majengo yake hivyo mteja ambaye anadaiwa ajiandae kuondolewa wakati wowote na kwamba zoezi la jana ni mwanzo tu.

Baadhi ya watu wamelihusisha tukio la kuondolewa Mbowe katika ofisi hizo na masuala ya kisiasa.

Lakini Mwanasenga alisema uamuzi wa kumuondoa ofisi hizo hauna uhusiano na masuala ya kisiasa.

Alisema wapangaji wa jengo hilo wapo wengi pamoja na wadaiwa na kwamba baada ya mchakato huo kuanza mdaiwa yeyote atakayeshindwa kulipa kodi ataondolewa.

Akizungumza na waandishi wa habari katikati ya wiki iliyopita, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu alisema pamoja na Bilicanas, shirika linazidai taasisi za umma, binafsi na watu binafsi jumla ya Sh. bilioni 15.

Notisi ya siku 60 ya kuondoka Bilicanaa pamoja na majengo ya wadaiwa wengine ilishatolewa, Mchechu alisema. Notisi hiyo ilikuwa inaisha juzi.

Alisema baada ya muda huo kumalizika, utekelezaji wa kuondolewa katika majengo hayo utaanza ukiambatana na uchukuaji wa hatua za kisheria.

Mchechu alisema mbali ya Bilicanas, wadaiwa wengine ni Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi inayodaiwa Sh. bilioni mbili, Benki ya Azania (Sh. milioni 161) na Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa (Sh. milioni 631).

Wadiawa wengine walitajwa kuwa ni Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Sh. bilioni 1.3), Wizara ya Ujenzi (Sh. bilioni mbili), Tume ya Utumishi (Sh. milioni 109) na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Sh. bilioni moja.

Mchechu alisema ukusanyaji wa madeni hayo kwa nguvu ni mkakati wa shirika hilo kukusanya fedha ili kusaidia ujenzi wa nyumba za watumishi wanaohamia Dodoma.

"Mwaka huu ujenzi unaanza Dodoma," alisema Mchechu, hivyo "fedha tunazodai zitatusaidia kukamilisha uwekezaji mjini humo."

Alisema kuwa fedha hizo zitatumika kwa ujenzi wa nyumba za watumishi 300 hadi 500 mkoani Dodoma.
 
Alisema ujenzi huo unatarajia kuanza mara moja na utachukua miezi 12.

Kwa mujibu wa Mchechu, Sh. bilioni 60 za ujenzi wa nyumba hizo zitatokana na fedha za ndani.

Alisema shirika hilo limenunua ekari 240 eneo la Iyumbu, ekari saba Chamwino, nne Bahi na Chemba ekari nne pia ikiwa ni kuunga mkono azma ya serikali ya awamu ya tano kuhamia Dodoma.

Alisema fedha nyingine zitapatikana baada ya nyumba 97 za shirika hilo zilizopo Medeli mjini Dodoma kuuzwa.

Post a Comment
Powered by Blogger.