NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA AROBAINI(40)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Tinonko alikuwa akionekana kupitia ile kamera ya drone kuwa hatembei kabisa. Hapo ndiyo rubani wa kile chombo ambaye alikuwa akiendesha kwa njia ya rimoti mwenyewe akiwa Tanzania, akaamua kukishusha chini kabisa ili apate picha nzuri kama Tinonko amekufa au lah.
Kwa juu walikuwa wakiona guo lake lakini walipovuta kwa karibu waliona lile guo likiwa tupu. Kwa maana hiyo Tinonko alikuwa amewadanganya kwa kujifanya mfu kumbe aliliweka lile guo lake pembeni kisha yeye kutoka.
Inawezekana kabisa alifanya hivyo baada ya kuhisi anafuatiliwa na drone ambayo hupaa na kutoa mlio kama wa mbu hivyo si rahisi mtu kushtuka kama siyo mtaalamu wa masuala hayo.
Wakati huo yule rubani aliyekuwa akitumia Kompyuta kukiendesha kifaa hicho alichokishusha hadi chini kabisa, akahisi kamera ikimuonesha kitu kikitembeatembea. Kwa vile ilikuwa usiku hakuweza kuona vizuri akaanza kuipandisha ile drone yake kwa juu ili apate picha ya chini kwa uzuri.
Akiwa katika kunyanyua juu kifaa hicho ndipo Tinonko aliyekuwa amejibanza pembeni akiwa kifua wazi alivuta jiwe na kukiponda kiasi cha kushindwa kuruka tena. Akakitazama kile kifaa na kuhakikisha sasa kuwa ni kweli alikuwa akipigwa picha.
Akatazama juu kama kulikuwa na kifaa kingine lakini hakuona, hivyo akavaa guo lake na kusonga mbele usiku mzima.
Mungu ashukuriwe kuwa pamoja na kuumwa kwake lakini hakupumzika, alitaka afike kabla hajafa, hivyo siku zake za mwisho alitaka kuzitumia kufanya chochote ili mradi aende mbele, iwe kwa kutambaa, kukimbia au kutembea.


Wakati huo ndugu na jamaa walikuwa wamejazana kwenye jumba la Jackline na Peter, wakiwa wanasubiri ndoa ikamilike siku chache zijazo.
Wapo waliostaajabu kwa nini Jackline aliwahi kuolewa tena baada ya kifo cha mumewe, lakini wengine walilazimika kuendana na ukweli kuwa pengine Jackline alikuwa na upweke hivyo kuwa na Peter hasa katika kipindi hiki cha ujauzito kulikuwa kukimpa faraja.
Katikati ya wageni Suzy alionekana, lakini hakuwa akichambua mchele wala kutandika majamvi kama wageni, yeye alionekana kumtazama Peter aliyekuwa akizungumza na baadhi ya ndugu wa kiume wa Jackline.
Suzy aliyevalia nguo zake maridadi kiasi cha kumfanya aonekane mrembo zaidi, aliinua simu yake na kubadilisha laini kisha akatazama baadhi ya picha za Peter akiwa na nguo za jeshi na kuzisendi kwa namba ambayo iliandikwa Peter.
Mara Peter alifungua simu yake na kutazama meseji hiyo mpya, akainuka kwa wasiwasi akionekana kuhaha kuipiga simu ile, wakati huo Suzy akaitoa ile laini na kuweka laini yake ya awali. Alipowasha simu tu, simu ya Peter iliingia.
“Suzy, hebu njoo mara moja,” alisema Peter kwa wasiwasi zaidi.
“Nini hebu niambie,” “Njoo kwanza kuna ishu hapa,” “Ok,” Suzy akasimama na kumfuata alipojibanza bwana harusi mtarajiwa, Peter. “suzy kuna mtu amenitumia picha yangu nikiwa na gwanda, yaani nimeshangaa sana,” alisema Peter.
“duh! Sasa huyo mtu atakuwa nani?” “sijui, mbaya zaidi amenitumia meseji anasema harusi njema, huyu inawezekana kabisa ananijua na anamjua Jackline,” alisema Peter kwa hofu.
“Mh kweli, tena anaonekana anajua unamficha Jackline kuwa wewe ni mwanajeshi,” alikazia Jackline na kumfanya Peter ajae wasiwasi.


“Sasa nifanye nini Suzy?” “Cha msingi muulize anataka nini. Isiwe anataka kuharibu harusi yako kwa kumtumia Jackline hizo picha.”
“Lakini hata hivyo bado naona haitatosha, kwa sasa nimeacha huo uanajeshi na hata kama Jackline atagundua nitamzuga na kumuomba msamaha. Atanisamehe tu kwa sababu ni jambo la zamani, hata kama nilimficha,” alijipa moyo Peter jambo lililoonekana kumuudhi Suzy.
Suzy akaondoka taratibu kuelekea sehemu aliyokuwa ameketi mwanzo, wivu ukiwa umemjaa, alihisi pengine Peter akimuoa, Jackline hatadiriki kumuua kama walivyopanga. Lakini alijua hapaswi kuharibu mipango yao kwa kumuwazia Peter mabaya.
Alikubali aishi maisha ya hofu na wasiwasi lakini hakutaka kuwa mjinga wa kusubiri nini Peter afanye, alichojua mwanadamu haaminiki linapokuja suala la pesa. Hivyo akataka kipimo cha wasiwasi wake kimkumbe na Peter pia, akagundua jambo pekee linaloweza kumpa wasiwasi Peter si lingine bali ni suala la siri zake kwa Jackline.
Moja ya siri hizo ni suala la kumficha Jackline kwamba alikuwa mwanajeshi jambo ambalo Peter alijifanya kulipangua kwa sababu eti anasema lilikuwa ni jambo la zamani.
Siri nyingine ni suala la Peter kuwa na uhusiano wa mapenzi na yeye, lakini kubwa jingine ni kuhusu mpango wao wa kudhurumu Jackline mali za Tinonko, lakini hilo hawezi kumtikisa nalo kamwe.
Akaona atupie suala la pili yaani amtumie Peter picha za mapozi za mahaba akiwa naye, kwa kuwa hilo linaweza kumtikisa kidogo kuliko kawaida hasa pale atakaposema kuwa anataka kumtumia Jackline. 
Lakini wakati akiwaza hayo, ghafla alimkumbuka Tinonko mwenyewe ambaye alijua wazi kuwa yupo hai kwa mujibu wa Peter ingawa hakujua wapi. 
Akapanga kufanya ujanja wowote ili amuoneshe Jackline kuwa Tinonko ni mzima, ili ampime kama atamuacha Peter au ataendelea naye. Akaona hili alifanye peke yake japokuwa alikiri kufanya utundu huu kwa wivu tu na si kingine.


ITAENDELEA IJUMAA
Post a Comment
Powered by Blogger.