NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA THELASINI NA TISA(39)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.Enzi hizo ndipo Farudume aling’amua mahusiano kati ya Tinonko na Jackline, katika kuchimba historia ya binti huyo akagundua alikuwa akipendana na mtu anayeitwa Peter kijana muuza mtumba maeneo ya Ubungo Darajani.

Akagundua kuwa Peter alimuacha msichana huyo kwa msichana mwingine aliyekuwa akimuweka mjini ambaye ni Suzy, hivyo Farudume akaona huyo ni mtu sahihi kuandaa malipizi ya kisasi chake kwa Tinonko.
Hilo likamvutia Farudume amtafute kijana huyo na kumuahidi mshahara mnono jeshini ili mradi aanze kazi ya kumrudisha Jackline kwenye mikono yake hata kama atakuwa akimuongopea, Faru alijua kupitia mwanamke hata mtu awe na nguvu vipi lazima aanguke.
Akapanga kumuumiza Tinonko kwa upande huo pia, ndiyo maana Peter mara baada ya Tinonko kupotea huko Kongo na kudhaniwa amefariki ndiyo akatokea na kujifanya anampenda sana Jackline. Tena kwa msaada wa Suzy tayari wameonekana kumteka na kushinda azma yao ya kuwa mabilionea kupitia mgongo wa mtu.
Taarifa ni kwamba hata kazi ya jeshi kwa sasa Peter alikuwa ameshaacha na maisha yake sasa huko Morogoro ni ya bata kila kukicha na Jackline huku yeye na Suzy wakifanya yao kisirisiri wakingojea siku ya ndoa ili wammalize Jackline ambaye kitumbo chake kilikuwa ndii.
Hapo mwanzo wakati Tinonko bado yupo Kongo, Farudume na Uku-Uku kazi yao kubwa waliyokuwa wakiifanya ilikuwa ni kuhakikisha yeye na Uku-Uku wanamfuatilia Tinonko kila hatua anayopiga huko Kongo ili kujua siku na muda atakaofika hapo kambini kama utabiri ulivyoonesha lakini kikubwa zaidi kujua kama madini hayo ya thamani atakuwa ameyapata au lah.

Kipindi hicho ndiyo hata Aka-Baka alipopata wasiwasi kuwa kuna jambo baya litamtokea Tinonko na kuamua kutazama mtu huyo kwenye tambaa lake, huku nyuma akina Uku-Uku walikuwa wakiyaona yote na kuzuia wasionekane kimazingara.
Kama unakumbuka hapa ndipo Aka-Baka alishangaa na kusema; “inaonekana mtu huyu naye anajua teknolojia yetu.”
Kwa maana hiyo aliyekuwa akiijua teknolojia hiyo si mwingine bali ni UKu-Uku na si mwingine. 
Kwa hiyo siku hiyo Farudume na Uku-Uku walikuwa wakiijua na kupanga shambulio lao ambalo lilienda vilevile kama walivyoliona mwanzoni.
Ngoja sasa nikusimulie habari za huyu mtu wa ajabu Uku-Uku na kwanini anajua mambo mengi hivyo.
***
Historia inaanzia katika kijiji hicho cha Kivu katikati ya msitu wa maajabu wa Kongo ambapo kuna makazi ya viumbe wengi wa ajabu wakiwemo mbirikimo.
Mbirikimo wote walikuwa wakilindwa na kuongozwa na waona mbali au viongozi wa kimila wenye uwezo wa ajabu ambao ni mtu na kaka yake wanaoitwa Aka-Baka na Uku-Uku. Wote hawa wakiwa chini ya mfalme Twa.
Enzi hizo ndipo Uku-Uku ambaye ni mdogo wa Aka-Baka aligundulika kutumiwa na waasi kwa siri, kwa kutoa mali zao zikiwemo madini na kuwapa waasi hao kisha yeye kupewa wanawake wazuri ambao ndiyo starehe yake kubwa. Madini hayo waasi waliyatumia kununua silaha mbalimbali za mapigano na kuchochea vita zisizoisha Kongo.
Hilo lilifanya siri za mali za mbirikimo wa kivu kujulikana na kuwafanya wawe hatarini kuvamiwa huku majaribio hayo yakifanyika mara kadhaa. Aka-Baka baada ya kugundua kuwa ndugu yake ndiye aliyefanya uasi huo alimuanika kwa wanajamii wenzake na kutoa adhabu ya kumfukuza kutoka kwenye himaya yao kwa kiapo cha kifo ikiwa atapatikana tena katika msitu wa Kongo.
Siku hiyo akiwa anatimua mbio ndipo alipokutana na Farudume na kuomba hifadhi na usalama nchini Tanzania. Hayo yanaelezea kwanini Uku-Uku anaonekana kuwa na nguvu sawa na Aka-Baka ingawa mmoja ni muovu kiasili na mwingine ni mwenye busara.

Turudi wakati huu ambapo tunamuona Tinonko ambaye masikini hafahamu mipango yoyote ya watesi wake, akijikongoja kwa takribani siku tatu ndani ya msitu wa Kongo.
Mbaya zaidi hamjui Farudume, wala Uku-Uku lakini alichokijua kuna watu ambao ni zaidi ya mmoja walioonekana kumchukia kiasi cha kuwa tayari kuutoa uhai wake kinyama kama hivyo.
Kama kawaida drone iliendelea kurusha picha za Tinonko usiku mzima na wale watu waliokuwa kwenye kile kitengo walitulia kimya wakifuatilia kama Tinonko atafika na kuwapatia utajiri wa kuitawala dunia kwa kuwaonesha sehemu ambayo wale Mbirikimo wanaishi na kuficha mali zao.
Unaweza sasa kuona kuwa Farudume alipokea fedha ngapi kutoka kwa watafiti hao ili mradi tu kufanya jambo hilo la kibaladhuri.
“Bosi anaonekana kama vile atakufa, bado siku tatu tu na hali yake inaonekana mbaya sana,” aliongea dokta Gama akimwambia mzungu mmoja anayeitwa Duncan aliyeonekana amesimama wima kwa muda mrefu akimtazama Tinonko aliyejilaza juu ya majani mabichi akionekana kuelemewa.
Kwa maneno hayo Duncan akainua simu yake na kupiga kwa Farudume;
“Our guy seems weaker, can he make it! (mtu wetu anaonekana mdhaifu sana, atafika kweli!)” aliuliza Duncan, Farudume akacheka kisha akasema; “atafika amini, mtapata mali zenu.”
“Assuredly (unahakikisha hilo)!”
“Nina uhakika,” alijibu Farudume na kukata simu.


ITAENDELEA IJUMAA
Post a Comment
Powered by Blogger.