NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA THELASINI NA NANE(38)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Katika kuonesha uwezo wake wa kupiga risasi Tinonko akaikoki bunduki yake aina ya SMG na kulenga alama iliyowekwa kwenye jiwe moja kubwa lililokuwa kama jabali kambini hapo.
Ukubwa wa jabali hilo ulifanana sana na yale mawe makubwa ya jijini Mwanza. Alama ya kidoa chekundu ilikuwa imewekwa katikati ya jiwe hilo ikizungukwa na rangi ya njano kuonesha kuwa hapo ndiyo panapotakiwa kulengwa ili kupata mshindi atakayevuka hatua ya Ukuruta na kuingia moja kwa moja katika kikosi cha udunguaji ‘Sniper’.
Wengi walikuwa wamejaribu na kukosa kulenga alama hiyo na wengine kukaribia kulenga lakini hakuna hata mmoja aliyepiga katikati. Hata Eddy alikuwepo naye alikosa tena risasi yake haikulenga hata jiwe lenyewe ambalo hata kipofu angepewa asingekosa.
Zamu ya Tinonko kuonesha uwezo wake ilifika akatumia dakika nzima kuchungulia jicho lake kupitia mtalimbo wa bunduki, akapima upepo, akapima umbali wake na hilo jabali kisha akafyatua, risasi ikachomoka na kulenga moja kwa moja kwenye ile alama.
Kwa kasi ya ajabu ikadunda na kupotelea hewani. Lakini alama ya risasi ya Tinonko kuchubua ile rangi nyekundu ilikuwa imebakia palepale kwenye lile jabali. 
Walipoona uwezo wa shabaha ya Tinonko waliishia kumpongeza na hapo ndipo akagundua kuwa tangu jeshi lianze kwenye kitengo hicho cha kulenga shabaha hakukuwa na mtu yeyote aliyewahi kulenga alama ile kwa ukamilifu kama yeye.
Tinonko akafurahi na kuungana na wenzake wachache wakisherehekea kuingia rasmi katika kitengo cha udunguaji.
Wakati hayo yanaendelea ndipo ghafla ikasikika kuwa palepale uwanjani kuna kijana alikuwa amezungukwa na dimbwi la damu. Sherehe nzima ilizizima baada ya kugundua kuwa kumbe ile risasi baada ya kudunda kwenye jiwe haikupotelea hewani badala yake ilirudi na kutua kichwani mwa Eddy.

Taarifa zilifika kwa kaka yake Eddy ambaye ni Farudume aliyeungana na wanajeshi kadhaa wakimkimbiza mgonjwa huyo Hospitali kwa ajili ya matibabu ya haraka.
Farudume akiwa na ghadhabu zake akauliza swali moja tu; “nani aliyefanya hivi?”
Mkuu wa kitengo cha shabaha huku akitetemeka akajibu; “ Risasi ya kuruta, anaitwa Tinonko Morato.”
Farudume hakutaka kuelewa ilikuwaje japokuwa aliambiwa kuwa risasi hiyo ilidunda kwenye jiwe na kurudi nyuma kwa bahati mbaya hivyo Tinonko hakufanya kwa makusudi.
AKiwa mwenye hasira baada ya kusikia mdogo wake Eddy hatakuwa na akili sawasawa kutokana na kuharibika ubongo wake, Farudume aliinuka na kutafuta bastola yake na kuapa kumuua Tinonko mara moja, hapo ndiyo Uku-Uku aliyegundua hasira za rafiki yake akarusha mavumba hewani akitabiri nini kitatokea endapo Farudume ataenda kumshambulia Tinonko siku hiyo.
Alichokiona kilimshangaza na kumfanya hata Farudume aghairi ubaya wake na kumuweka kiporo Tinonko siku zote hadi hivi leo.
Uku-Uku alisema kuwa Tinonko anaonekana kuja kufanya mambo makubwa na hatimaye kumpa Farudume utajiri maradufu.
“Una maanisha nini?” Farudume aliuliza akionekana hajaelewa chochote.
Uku-Uku akaweka tambala lake mezani na kumwagia vumba jekundu, ghafla likabadilika na kuwa kama televisheni, akaonekana Tinonko akiwa ya kambi ya jeshi, akiwa hapo ndipo mara wakatokea wanajeshi wengine wawili waliomsimamisha kwa kumuelekezea mitutu ya bunduki na kumtaka aweke kila kitu chini.
Moja ya vitu alivyoviweka chini ni pamoja na mfuko mdogo wa aina ya Kalabashi unaosokotwa na Mbirikimo wa Kivu peke yake dunia nzima. Ulipofunguliwa ulionekana kujaa madini na lulu za kila aina. 
Kwa mshangao Farudume akajiona ametokea nyuma ya Tinonko, akiwapiga risasi wale wanajeshi wawili na kumpiga kiwiko Tinonko aliyepoteza fahamu palepale.

Farudume akajiona akichukua madini yale kisha ile Tivii ya asili ikakata mwanga na kurudia katika hali yake ya tambala kama kawaida.
Farudume baada ya kuona hayo akafungua kinywa chake na kusema; “mambo hayo yatatimia lini?”
Uku-Uku akajibu; “yajayo yapo mikononi mwako.”
Kwa kauli hiyo Farudume akapiga moyo konde na kutumia nguvu zake za fedha kama mtaji wa kumuandaa Tinonko ili aweze kumletea madini yale kama alivyoona.
Kwanza alianza kuhonga wakuu wa jeshi ili kumpitisha Tinonko kwenye kila jambo, na kwa kuwa Tinonko mwenyewe alikuwa na uwezo mkubwa pia, ilikuwa rahisi hata Tinonko mwenyewe kubebeka.
Hayo yanaelezea kwanini Tinonko alijikuta akipanda vyeo harakaharaka pale jeshini kwa muda mfupi. Na wakati akijua kuwa Mungu amemfungulia kufikia malengo yake na kuamua kuoa kumbe Tinonko ndiye aliyekuwa akitekeleza mpango wake. 
Na ndiye aliyefanya hata harusi ikatike kwa ajili ya misheni ya Kongo, na ndiye aliyefanya mtu apandikize bomu kwenye ndege ya Tinonko na wenzake ili idondokee sehemu ileile ya Mbirikimo wa Kivu.
Alijua kwa vyovyote vile lazima Tinonko atafanikiwa kama alivyomtabiria Uku-Uku, hata kama atapitia mitihani ipi? Akajiwekea ahadi kuwa kisasi chake daima kitasubiri mpaka utabiri wa Uku-uku utimie.

ITAENDELEA ALHAMISI
Post a Comment
Powered by Blogger.