NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA THELASINI NA SABA( 37)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Farudume anakumbuka akiwa mikononi mwa mbirikimo huyu aliyeonekana mwenye nguvu kiasi cha kumbeba mtu mzima kama yeye, alipoteza fahamu akijua pengine mtu akiwa anaelekea kuzimu ndiyo hukutwa na hali kama yake. Yaani ya kukutana na Izraili akiwa na umbo la mbirikimo mwenye madevu meupe kama alivyokuwa Uku-Uku.
Alipata fahamu baadaye na kujikuta akiwa katika pango moja kubwa, lakini alijishangaa akiwa na nguvu na kuhisi hakuwa na ugonjwa wowote uliokuwa ukimsumbua.
Pembeni yake alionekana amekaa Uku-Uku akichanganya majani kadhaa na wadudu. Alipomuona Farudume ameamka akamsogezea jani la mgomba likiwa na vyura na konokono wasio na magamba. Akamwambia kwa lugha asiyoijua.
“manga”
Farudume akimtazama kwa mshangao kiumbe huyo mfupi, ambaye alimuonesha ishara ya mkono kwa kuupeleka kinywani. Farudume, akaelewa kuwa alitakiwa kuwala wadudu hao. 
Akafumba macho na kuwabugia kwa kuogopa kumuudhi mtu aliyemuokoa na kifo.
Hayo ndiyo yakawa maisha yao na wawili hao waliishi porini hapo kwa muda mrefu kiasi cha kila mmoja kuanza kufahamu lugha ya mwenziye.
Hapo ndiyo Farudume akatambua kuwa mbirikimo huyo mzee alikuwa amefukuzwa kijijini kwao na siku ile aliyokuwa akikimbia na kumkuta yeye akiwa katika hali ya nusu mfu ndiyo alikuwa akikimbia.
Farudume akamfungukia rafiki yake huyo mpya na kumwambia hitaji lake la kumiliki madini yenye thamani zaidi yanayopatikana huko Kivu, hapo ndipo Uku-Uku akafungua guo lake chafu na kumuuliza; “madini yenyewe ni haya?”

Hapo ndiyo Farudume akagundua kuwa mbirikimo huyo pamoja na kumiliki mawe hayo alikuwa hajui thamani yake. Kwa sababu alikubali kubadilishana madini hayo ya thamani kwa ajili ya usalama wake.
“Nikikaa hapa sana naweza kuuawa kwa sababu nimefanya kosa kubwa sana huko nitokako. Hivyo naomba kwa dhamana ya haya mawe, unitafutie sehemu ili nistarehe kwa amani.” Alisema Uku-Uku.
Kwa maneno hayo ndipo Farudume akagundua rafiki yake huyo alikuwa akihitaji nyumba na maisha mazuri, akawaza kuwa hayo yanaweza kupatikana Tanzania tu.
Akapiga hesabu ikiwa atafanikiwa kuyauza mawe hayo atapata hela ya kutosha kununua na kujenga nyumba nzuri na bado akawa na mahela ya kutosha.
Tatizo lilikuwa moja tu, je, atawezaje kufika Tanzania kwa muda sahihi. 
Uku-Uku aliweza kuyasoma mashaka ya rafiki yake, alipogundua tatizo ni nini, akacheka na kuchorachora alama pale chini kisha akamwambia afumbe macho na kuvuta picha sehemu anayotaka kwenda. 
Farudume akafanya kama alivyoamrishwa Uku-Uku naye akajishikiza mkono wake kwenye mkono wa Faru akimtahadharisha asifungue macho yake mpaka asikie amefinywa mkononi.
Kwa kitendo hicho wakajikuta wamesafiri na kuibukia jijini Dar, kwenye pori la mikoko baharini karibu kabisa na daraja la Selander. 
Giza la usiku liliwahifadhi wakatoka hapo bila kuonwa na mtu, wakaelekea kwenye kituo cha daladala cha darajani na kupanda taksi na kuelekea maeneo ya kigogo mwisho, sehemu ambayo Farudume alikuwa akiishi na mdogo wake Eddy.
Kuanzia hapo unaweza ukaelewa jinsi gani Farudume aliweza kuwa tajiri ghafla na kuishi na Uku-Uku ambaye anaonekana kujua vilivyo uchawi na mbinu za mambo ya ajabu za Kivu.
Lakini swali bado linabakia huyu Uku-Uku ni nani hasa?

Swali hili halikuwa muhimu kichwani mwa Farudume aliyebadilika na kuwa tajiri ghafla kwa kuwa alichokitaka alishakipata. Hivyo nitakujibu baadaye.
Farudume baada ya yeye kurejea jeshini akitunga uongo wa namna alivyookoka kwenye mashambulizi ya waasi na kurejea nchini kwa kupitia mipaka ya Rwanda, aliweza kupewa nishani kibao za ushujaa bila kujulikana kama alitelekeza misheni kwa ajili ya kusaka mali.
Kama mwanajeshi pekee aliyepona kutoka Kongo, Farudume alipata heshima hiyo, na wakati maswali yalipoanza kuibuka aliliweza kutumia pesa zake kwa kuwahonga wakubwa wote na hilo linaelezea jinsi alivyoweza hata kupewa vyeo vya juu jeshini na uhuru wakufanya chochote kwa kuogopwa. 
Miaka zaidi ya minne ilipita, hapa ndipo alipoibuka kijana mwenye bidii na ushupavu aliyeingia jeshini hapo kama Kuruta, Tinonko Morato ambaye moyo wa Farudume leo hii unamuweka kama adui yake namba moja baada ya kusababisha ulemavu wa kudumu kwa mdogo wake.
Farudume kwa wakati huo ndiyo alikuwa amemshawishi mdogo wake Eddy kuingia kwenye jeshi ambapo walijikuta wakiwa katika kikosi kimoja cha mafunzo na Tinonko.
Hawakuwa marafiki kwa kuwa hawakuwa wakijuana kabisa, Eddy alikuwa mdogo wa mtu mwenye cheo kikubwa hapo jeshini ambaye ni Farudume.
Tinonko kwa upande wake alikuwa ni kijana kutoka familia ya kimasikini, akiwa na ndoto za kujikomboa yeye na mama yake alikuwa akijituma kwenye mazoezi kila siku.
Siku hiyo Tinonko na makuruta wenzake akiwemo Eddy walikuwa kwenye mazoezi ya kulenga shabaha, mazoezi ambayo alikuwa akiyapenda sana kwa kuwa alikuwa mahiri wa kulenga shabaha. Siku hiyo walitakiwa kulenga jiwe fulani. Karibu na Tinonko alikuwepo Eddy.
Na ndiyo siku hiyo Tinonko alifanya jambo lililomsababishia Eddy ulemavu aliokuwa nao hadi hivi leo kiasi cha kumfanya Farudume amuwekee kisasi na kumpa malipizi kama anayompa hivi leo.


ITAENDELEA JUMATANO
Post a Comment
Powered by Blogger.