NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA THELASINI NA TANO(35)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Kapteni Tinonko akaanza kuhesabu masaa kuanzia siku hiyo mara baada ya kuambiwa ana wiki moja tu ya kuishi kabla hajapata dawa.
Kadri saa zilivyozidi kwenda mbele alishuhudia mabadiliko yake yakizidi kasi. Ebola, Ukimwi na Influenza wote alikuwa nao mwilini mwake na virusi hao walionekana kumshambulia kila sehemu ya mwili wake kwa kasi mno.
Kwa bahati mbaya akiwa anaangazaangaza macho yake chumbani humo, alijikuta akiitazama sahani ya dawa yenye rangi ya fedha ambayo ilimuonesha vyema taswira ya uso wake.
Akajitazama sura yake ilivyobadilika na kuwa ya kutisha mno, Malengelenge yakiwa yamejaa uso mzima. Tinonko akatamani kujiua lakini akashindwa kwa kuwa hakufunzwa kukata tamaa.
Akamuomba Mungu wake ampiganie maisha yake ili apone, na kama akipona akajiapiza kiapo cha damu dhidi ya wote waliomfanyia hivi. Yaani kiapo cha kuhakikisha anawaua wote waliomtendea mabaya kuanzia yule mwanajeshi aliyeonekana wazi kuwa ni Farudume.
Kwenye chumba cha pili, Farudume alionekana na wale madaktari akimtazama mateka wake, Tinonko. Akafurahia kila maumivu aliyokuwa akiyapata.
“Kamanda, hauoni kama umemtesa kiasi cha kutosha,” aliuliza Daktari Gama akimtazama Faru. “Hapana, bado nataka azidi kuteseka kiasi kwamba mwenyewe atamani kifo chake,” alijibu Faru.
“lakini kwanini mpaka uamue kumfanyia hivi mwenzako, kwani alikufanyia nini?” Swali hilo la Dokta Gama likayafanya macho ya Faru yabadilike rangi na kuwa mekundu kwa hasira, akamtazama Gama kama anataka kumshambulia, lakini akaghairi.
“Alichonifanyia ni zaidi ya hiki kinachomkuta leo.” Aliongea Faru na kuondoka zake.

Farudume akapanda gari na kuondoka akitokea kwenye jengo hilo la mambo ya tafiti na kuelekea moja kwa moja nyumbani kwake.

Alifika na kufunguliwa geti na mlinzi kisha akaingia ndani ya jengo kubwa lilionekana kusheheni kila aina ya utajiri.
Lakini tofauti na majengo mengine ambayo utajiri kama huo huendana na neema ya familia nzuri zenye furaha, nyumba ya Farudume ilijaa upweke na ukimya uliopitiliza.
Mwenyewe akaingia sebuleni kwake akiwapita wafanyakazi wake wawili na kupanda hadi ghorofa ya juu, akaingia ndani ya chumba kimoja ambacho mlango wake ulionekana ukiwa umefunguka kidogo.
Sauti ya televisheni ilisikika na mtazamaji alionekana akicheka kwa sauti akifurahia kipindi cha katuni, Farudume alisimama nyuma ya mtu huyu na kumtazama kwa makini kisha akadondosha chozi akisema; “Eddy, aliyekufanya hivi, leo nimemfanyia mara mbili yako..”
Yule mtu aliyeitwa Eddy akageuka na huku akicheka na kumtazama Farudume, kicheko kikazidi akacheka kama mwendawazimu hadi udenda ukawa unamchuruzika.
Kutoka kwenye kinywa chake akatamka neno moja tu lililo sahihi; “Kaka…!” akarudia neno hilo na mengine ambayo hayakusikika vizuri.
Eddy kwa furaha yake akataka kusimama kumkimbilia huyo anayemwita kaka yake, ambaye si mwingine bali ni Farudume. Katika kusimama akadondoka chini mguu wake mmoja ukaonekana umekatwa, na upande mmoja wa kichwa chake ukiwa na tundu moja kubwa lililochimba katikati ya ubongo wake na kufanya kichwa chake kuwa kama vile kimebonyea.
Kwa uchungu, Farudume akaenda na kumnyanyua bila kuona kinyaa chochote, akamuweka tena kwenye kiti chake na kuchukua pipi alizobeba mfukoni, kisha akampatia Eddy ambaye alizipokea kwa furaha na kuanza kuzibugia.

Farudume akamtazama mdogo wake ambaye kwa mbali walionekana kufanana, akasimama na kutazama picha iliyokuwa kwenye meza yake.
Picha hiyo ilimuonesha yeye Faru akiwa na mtu mwingine ambaye alionekana kijana kuzidi yeye, kwa ukaribu mtu huyu alionekana ndiye Eddy ambaye amebadilika na kuwa mlemavu kabisa.
Kuna baadhi ya picha wote wawili walionekana wakiwa na mavazi ya kijeshi, na nyingine akiwa na wanajeshi wenzake. Kuna moja ambayo Eddy alionekana akiwa juu ya kifaru na Kapteni Tinonko.
Faru alipoitazama picha hii hasira zilimpanda akaichanachana na kupiga kelele kwa hasira. Kwa hofu, Eddie akaanza kulia kwa sauti, Faru akamkimbilia na kumbembeleza. Eddy alitulia na kulala kabisa.
***
Mapema asubuhi timu ya watu walioonekana ni madaktari waliingia chumbani kwa Tinonko wakiwa na mavazi ya manailoni yaliyoziba miili yao yote. Tinonko alijua kuwa walikuwa wakijilinda na maambukizi ya ugonjwa alionao. Akiwa haelewi nini kinachoendelea akajikuta akipigwa sindano iliyomfanya apoteze kabisa fahamu.
Alikuja kushtuka baadaye akiwa ndani ya kitu mfano wa jeneza ndani yake akiwa na mikate, kisu na matunda, begi na manguo makubwa mfano wa shuka.
Alihangaika kupiga kelele na kupigapiga lile boksi lililoonekana kufungwa ndindindi. Baadaye akagundua kuna ufa mkubwa kwenye kona ya boksi hilo. Akatumia kisu kulifungua.
Hewa na mandhari ya sehemu aliyotokea ilimshangaza, akatazama lile boksi akagundua lilikuwa limefungwa na parashuti na kutua hapo. “Kwa hiyo nipo Kongo, Kivu? Mungu nisaidie” alijiuliza Tinonko akasimama huku maumivu makali ya mwili mzima yakimkabili hasa kwenye yale malengelenge na kibiyongo chake.


ITAENDELEA JUMATATU
Post a Comment
Powered by Blogger.