NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA THELASINI NA NNE(34)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Sajenti Ngowi akashuhudia roho yake ikiwa mikononi mwake, wakati huo yule muuaji wake akaendelea kukaza kamba hadi kuhakikisha upepo wa pumzi hautoki katika mwili wa Sajenti Ngowi.
Hatimaye akamwachia, akadondoka kama mzoga ardhini. Muuaji yule ambaye alionekana kuwa ni mmoja wa wale watu wawili anaowatumia Farudume, baada ya kumaliza azma yake akapekuapekua baadhi ya vitu kutoka ndani ya kile chumba cha Sajenti Ngowi kisha akatoka na mafaili kadhaa na kuwasha moto lile godauni kisha akateleza kama nyoka akitoka mle ndani.
Wiki tatu baadaye sajenti Ngowi akawa amesahaulika kama marehemu wengine na mbaya zaidi hata jina lake halikutajwa kokote.
***
Peter kwa upande wake aliendelea na maisha yake na Suzy huku akifurahia kukutanishwa na ndugu wa upande wa Jackline ambao japo walishangaa suala la ndoa ya mtoto wao kuwa haraka kiasi hicho, lakini walikosa usemi na kukubali mtoto wao aolewe.
Kutokana na ushawishi wa Peter, ndoa hiyo ilitakiwa kufanyika Morogoro ambapo ndiyo mahali bibi harusi na bwana harusi watarajiwa walihamia ili kukwepa macho ya mapaparazi jijini Dar.
Mali zote zilizopo jijini Dar Peter alimshawishi Jackline aziuze na kujipatia mabilioni ya fedha yaliyowatosha kujichimbia maeneo ya Kihonda Morogoro bila kumsahau Suzy ambaye alikuwa akiwaganda kila waendako akiwa na mpango mmoja tu akilini mwake; Pesa. 
Yeye na Peter Waliendelea kucheza mchezo wa siri bila Jackline kujua huku wakijihakikishia utajiri huo kuwadondokea wao siku chache zijazo, hivyo wakasubiria ndoa ambayo ilikuwa ni wiki chache tu zijazo.

Kapteni Tinonko akiwa kama kawaida katika chumba chake siku hiyo alishangaa kutolewa na kupelekwa katika chumba kingine ambacho ndani yake kulikuwa na mtu mmoja aliyeonesha sura yake wazi.
Nyuma yake kulikuwa na kioo chenye giza mno ambacho kilionesha kuwa ni chumba cha mahojiano.
“Tinonko, naitwa Freddy Gama, nataka utuelezee kwa kifupi juu ya misheni yako Congo,” alisema mtu huyo aliyekuwa akimhoji.
Tinonko akaelezea mwanzo mwisho lakini akaruka stori kuhusu mbirikimo na hata maajabu yote aliyokutana nayo akiwa huko.
“Tinonko, kuna watu muhimu ninahitaji unielezee. Una wajua mbirikimo wa Kivu?” alihoji mtu huyu swali lililomfanya Tinonko ashtuke, akijiuliza watu hao wamejuaje.
“Mbirikimo gani?” aliuliza Tinonko huku akijifanya hajui.
“Tinonko, kuna mambo mengi ambayo yanaendelea hivi sasa huko nje kuhusu familia yako. Mama yako mgonjwa, mkeo Jackline ameshachumbiwa, na ndani ya wiki ijayo ataolewa rasmi. Sasa usijipotezee muda nijibu swali langu tukuchie,”
Tinonko kwa hasira akavuta picha ya maneno hayo kama ni ya kweli au lah, lakini akaona hana haja ya kuficha kitu kwa kuwa alikuwa akitaka kuondoka humo ndani kuliko mtu yoyote, japo kuwa alikuwa na wasiwasi kama watu hao watamwachia kweli au lah. Bila hiyana akaanza kuwaelezea kila kitu kilichotokea na mpaka alivyofika hapo kambini.
Alipomaliza kusimulia alishangaa kuona mtu yule akitoka nje, ndani ya dakika chache akasikia harufu nzito mle ndani iliyomfanya ajisikie kizunguzungu na kudondoka chini akikosa nguvu.
Bila kujua alitumia muda gani kabla ya kurudiwa na fahamu, alishtuka yupo kwenye kitanda kwenye chumba fulani kama vile hospitali. Yule mtu aliyekuwa akimhoji humo alionekana amevalia koti la daktari na ndiye aliyemchoma sindano fulani yenye maji ya Kijani.

Hapo akajikuta akipitiwa na usingizi mzito, alipoamka jasho likawa linamtoka mno huku hali yake ikidhoofu.
Yule daktari aliyekuwa amekaa karibu yake akasimama na kumtazama akamwambia; “Tino, damu yako tumeichanganya na virusi wa aina tatu hatari duniani; Kirusi wa mafua (Influenza Virus), Kirusi wa Ukimwi (Human Immunodeficiency Virus) na wa mwisho ni Kirusi wa Ebola (Ebola Virus).
“Tumegundua kwa uwezo wa ndugu zako wa kimbirikimo unaweza kupona ugonjwa wowote ambao utakupata kupitia dawa zao, na kama utapona ugonjwa huu basi dawa hizo zitatufanya tuwe matajiri sana. Na wewe ukiwa kama mfano wetu wa kwanza kabisa,” alisema yule daktari bila chembe ya huruma.
“ila kwa bahati mbaya kutokana na virusi hao kuanza kukushambulia, ukipita wiki moja bila dawa zao hakika utakufa, na hilo hatujali,” aliongeza kupigilia msumari.
Dokta akacheka na kumtazama Tinonko ambaye mwili wake ulikuwa umeshaanza kubadilika na kuota malengelenge mwili mzima. Ngozi yake ikavutika na kuvimba kila sehemu. Macho yakawa mekundu na mgongo wake ukapinda na kufanya kibiyongo huku nywele zikimpukutika kama kuku mwenye mdondo. “Kwanini mmeamua kunifanyia hivi?” alilia Tinonko akitazama shepu yake ya kibinadamu inavyobadilika. “Sijui lakini tunachojua tumeuziwa uhai wako na jeshi kwa ajili ya majaribio,” alisema Dokta Freddy Gama huku akimtahadharisha kuwa wamemuwekea kifaa maalumu cha GPS karibu na moyo wake, ili wajue uelekeo wake.
“Fikiria mama yako na mkeo, fanya bosi anachokuagiza. Safari ya Kongo ni kesho asubuhi,” alisema Dokta Fredy na kuondoka huku maandishi ya koti lake la kidaktari yakisomeka; Institute of Supernatural Research (Kitengo cha Tafiti za Mambo ya Dhahania)
Kapteni Tinonko anakutwa na majaribu makubwa safari hii, anagundua kumbe amehamishwa jeshini na kuuzwa kwenye kitengo cha Tafiti ya mambo ya dhahania, na kuchomwa sindano za magonjwa yakiwemo ya Ukimwi.

ITAENDELEA JUMAPILI
Post a Comment
Powered by Blogger.