NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA HAMSINI NA MBILI(52)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.Kwa aibu Peter alimtazama Jackline akashangaa mwanamke huyo ameokoka vipi kutoka mikononi mwa simba wa porini, akawaza kuwa amefikaje hapo. Akaanza kujiuliza je, anafahamu kuwa yeye ni Peter? lakini kwa kumuangalia kwa ukaribu akagundua hajamfahamu bado hivyo akaona haina madhara.
“Samahani kaka yule ni mbwa wangu, pole,” alisema Jackline akimuomba msamaha kiungwana mwanaume mwenye sura mbaya iliyoungua vibaya kiasi cha kutisha akiwa mbele yake. Hakujua kama huyo ni Peter na laiti kama angejua sijui ingekuwaje.
“usijali dada, bila samahani.” Aliongea Peter wakati huo simba alikuwa akikimbizwa na wanakijiji waliodhania ni mbwa kichaa, hivyo naye akakimbia na kwenda kujificha maporini, lakini akijua fika kuwa Jackline hayupo kwenye mikono salama.
Baada ya Jackline kuongea na Peter akainuka na kwenda kukaa pembezoni mwa aile nyumba aliyokuwa na uhakika ni yake, akazitazama zile namba na kubakia akisikitika, akaazimia kulala hapohapo hadi kesho asubuhi ili afanye utaratibu mwingine kuanzia kuulizia kwenye ofisi za serikali ya mtaa na sehemu nyingine.
Angeweza kusaidiwa na majirani kama angekuwa akiishi nao vizuri hapo mwanzoni, lakini maisha yake ya kujificha na ya kitajiri yalimfanya asijulikane hata na jirani zake hivyo kulala hapo nje kwa aibu ya kuomba msaada lilikuwa ni suala lisilopingika kabisa.
Maskini Jackline akatandika kanga na kuweka begi lake upande wa kichwani kisha akajifunika na shuka lake kimya akifumba macho.
Wakati huo Peter aliyekuwa akizungukazunguka maeneo hayo aliona mipango yake ikiharibika tena akaona ikiwa Jackline ataendelea kuwa mtaani hapo itakuwa ngumu kwake kuipata nyumba hiyo hivyo akajiongeza haraka.
Akatembea na kuelekea dukani kwa mangi. Akatoa shilingi elfu moja pengine ndiyo pekee aliyobakiwa nayo duniani.

Akaomba kumpigia simu ya mangi kwa muda na hela hiyo ikawa kama vile dhamana yake. Akampigia simu dalali wake akamtaka afike na funguo haraka usiku huohuo huku akimwambia ameghairi kabisa masuala ya kuuza nyumba.
Hata hivyo ikambidi atumie ujanja kuwa dalali huyo anatakiwa kufika nje ya nyumba hiyo na kumkabidhi ufunguo mlinzi ambaye ni mwanaume aliyeungua kwa moto uso wake. Alifanya hivyo kwa kuwa alijuafika kuwa kama dalali huyo atajua kuwa yeye ndiye aliyemuomba ufunguo atakataa kumpa baada ya kumuona kwa kuwa alikuwa na majeraha makubwa yaliyomfanya asijulikane kabisa.
Kweli baada ya robo saa yule dalali alifika na kuangazaangaza macho pale mtaani akimtafuta mtu aliyeelekezwa kuwa ndiye anatakiwa kumpa ufunguo.
“Samahani nimetumwa na Peter nikupe ufunguo,” alisema yule dalali akimkabidhi Peter ufunguo bila kujua kuwa ndiye mwenyewe.
Baada ya kuuchukua ufungo huo haraka Peter alirudi hadi pale alipokuwa amelala Jackline akamuamsha na kujifanya anamuuliza.
“dada kwani wewe ni nani?”
“mh! Naitwa Jackline.” Alijibu kimkato Jackline akiwa amekasirika kuamshwa.
“mbona umelala hapa!”
“nilikuwa nimesafiri sasa nimerudi ndiyo nakuta nyumba yangu imefungwa na imeandikwa inauzwa. Usiku huu nimeona bora nilale hapahapa hadi asubuhi ndiyo niende serikali ya mtaa.”
“ha! Kumbe wewe ndiye mwenye nyumba wangu? mimi nilikuwa nimeambiwa nilinde tu hapa na nilikuwa nakaa hapa ndani, ufunguo huu hapa.” Aliongopa Peter na uongo wake ukaonekana kumuingia Jackline aliyeutazama ule ufunguo na kuona ukifungua kweli.

“kwa hiyo nani aliyekupa kazi ya kulinda hapa?” aliuliza Jackline kwa mshangao.
“nilipewa kazi na mwanaume mmoja anaitwa Peter. Aliniambia kuwa yeye na mkewe ambaye nahisi ndiyo wewe mnaenda fungate hivyo niliinde kwa sababu kama unavyoniona alinionea huruma kwa vile sina kazi.”
“sasa mbona pale mbele kumeandikwa Nyumba inauzwa, nani aliyeandika maneno yale?” alihoji tena Jackline
“Bosi Peter ndiye aliyeniambia niandike kwa sababu alitaka kuiuza hii nyumba. Kwani hakukwambia?” alisema Peter akimsingizia Peter, Jackline akajifikiria na kuamua kuachana kwanza na mlinzi huyo. 
Haraka akaingia hadi ndani na kufungua mlango wa nyumba kubwa akaingia hadi ndani na kulala kwanza ili apunguze uchovu.
Alipoamka asubuhi kazi ikawa ni kutafuta kila kitu chake kuhakikisha kama kimekaa vizuri. Kwa mshtuko alishangaa kuona kabati lake likiwa limekombwa kila kitu. Akashika mikono kichwani akithibitisha ukaliti wa Peter na Suzy.
Baadaye akakumbuka kuwa kuna hela kidogo alikuwa amezihifadhi kwenye begi lake la nguo, akafungua na kukuta kiasi cha fedha takribani shilingi laki saba. Cha kufanya haraka asubuhi hiyo ni kwenda dukani na kununua simu na laini mpya kisha akarudi nyumbani.
Wakati huo Peter alikuwa akijifanya kufagia uwanja na kupanga vitu, alipomwona Jackline anaingia, alimuamkia kwa adabu kama vile walinzi wafanyavyo. Jackline akampa shilingi elfu 10 na kumtaka angalau akapate kifungua kinywa.
Hiyo ikawa msaada mkubwa kwa Peter, haraka akaenda kunywa supu ya kongoro maana hata mara ya mwisho kula hakuwa akikumbuka kabisa.

ITAENDELEA IJUMAA
Post a Comment
Powered by Blogger.