NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA HAMSINI NA MOJA(51)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.Afande Sanga haraka akawasiliana na wakubwa wake na kuwapa taarifa hiyo, ingawa hakuweza kuepuka lawama kuhusu kutokomea huko kwa mtuhumiwa namba moja wa matukio tata kutokea ndani ya kipindi cha muda mfupi.
Hata hivyo hakuna kifungu cha sheria ambacho Afande Sanga alikuwa amekiharibu kwa sababu hata suala la kuhakikisha Peter alikuwa akilindwa pale hospitali halikuwa chini yake, bali ni kitengo cha vidhibiti na ushahidi ambacho kilikuwa chini ya OCS yaani mkuu wa Upelelezi wa kituo husika.
Hivyo haraka taarifa zikasambaa na kuanza kumsaka Peter sehemu mbalimbali, lakini kikwazo kikubwa kikawa kwenye suala la picha, Je watatumia picha ipi kutangaza kuwa huyu ndiye Peter tunayemtafuta?
Fahamu tu kwamba mara ya mwisho sura ya Peter ilikuwa imeharibika vibaya kiasi cha kutotambulika kutokana na kuungua kwa moto na kwa bahati mbaya hakupigwa picha akiwa katika hali hiyo. Kwa hiyo wakitumia picha ya Peter enzi hizo akiwa mzima hakuna mtu atakayemgundua hata akimuona, hivyo wakalazimika kutangaza tu kuwa ni mwanaume na ameungua vibaya usoni.
Kwa vigezo hivyo wakajikuta kwa mkoa mzima wa Iringa wakiwakamata watu walioungua usoni zaidi ya themanini na hawakuweza kumtambua yupi ni Peter na yupi siye kwa kuwa hakukuwa na kithibitisho hasa hata kama Peter naye walimkamata na kumuhoji.
Afande Sanga na uongozi mzima wa polisi ukainua mikono na kutaka kujua pia tukio hilo kwa upande wa Jackline ambaye waliwatumia askari wa Morogoro kupata maelezo yake yote na kwa kuwa hawakuwa na mtu wa kumshikilia ambaye ni Peter, basi hawakuwa na la kufanya zaidi ya kufunga faili la kesi hiyo.

Jackline na simba nao baada ya kupata unafuu, sasa waliweza kurudia hali zao za kawaida na kuwaaga wenyeji wao waliowasaidia kwa fedha kidogo na usafiri hadi Morogoro Kihonda kule kwenye nyumba ya Jackline aliyokuwa wakiishi na Peter.
Alifahamu kuwa ikiwa atarudi nyumbani hapo ataweza kuchukua stakabadhi na nyaraka mbalimbali zikiwemo kadi za benki na kuweza kujikimu kimaisha kwa muda kabla hajaanza kufikiria nini cha kufanya.
Maskini kumbe alichokiwazia kilikuwa tofauti kabisa na hali halisi, hizo stakabadhi, nyaraka na baadhi ya kadi za benki na hela zote tayari Peter na Suzy walikuwa wameshazikomba zamani sana na jambo la kusikitisha ni kwamba hata wao mali hizo zimewatokea puani baada ya kila kitu kuungua kwenye mlipuko uliotokea kule Udzungwa na kumuua Suzy.
Jackline hakuyajua hayo na hata polisi hawakumueleza kuwa Suzy amekufa wala Peter hali yake ilivyo, Jackline alichojua ni kwamba Suzy na Peter walikuwa wamemkimbia na mali zake na kamwe hakujua kama watu hao waliweza kuingia hadi ndani ya kabati lake na kuchukua nyaraka nyingine muhimu, wazo hilo hakuwa nalo kabisa.
Safari ikafikia nyumbani kwake akashuka na kutembea kwa mguu njia nzima watu wakimshangaa mwanamke huyo anayetembea na mbwa mkubwa bila wasiwasi. Alifika karibu na nyumba yake na kukuta ikiwa na kufuli kubwa kwenye geti huku maandishi makubwa yakisomeka inauzwa kwa maelezo piga namba 0716681121.
Jackline akajikuta akichanganyikiwa kwa kutoamini alichokiona.

***
Mbali juu ya milima Gangilonga katika mitaa ya Kiyesa mjini Iringa, Peter akiwa na mashuka mazito aliyojitanda nayo kama mzee kikongwe alikuwa amekaa akiota moto. Moto ulikuwa ni adui yake namba moja. Hakuupenda kabisa lakini kwa baridi kali la Iringa, ngozi yake iliyoungua na kubakia makovu matupu ilikuwa ikimuuma sana hivyo dawa pekee ni joto la moto huo alioukoka akiwa peke yake juu kabisa ya pori la mlima Gangilonga.
Maumivu makali yalikuwa yakimsumbua hakuweza kulala kwa amani kwa kumbukumbu za mpenzi wake Suzy. Kuna wakati akatamani kujiua kwa kujinyonga kwa jinsi alivyokuwa na shida. 
Akafikiria jinsi utajiri ulivyompokonyoka baada ya kila kitu chake kuungua, akafikiria jinsi alivyohangaika kuupata utajiri huo na kisha kumpotea mkononi mwake.
Akajitahidi kuvuta kumbukumbu na kugundua kuwa lazima mtu aliyehusika na lile bomu hakuwa mwingine zaidi ya Farudume. Akasikitika sana kwa nini hakuwa makini kumlinda Suzy. Sasa mali pekee ambayo ilikuwa imebakia ilikuwa ni ile nyumba ambayo alikuwa akiishi na Jackline kule Morogoro ambayo alikuwa akiiuza. Akaona cha msingi ni kurudi kule kwanza ili atulize akili yake na si siku nyingine alitaka kuondoka siku hiyo. 
Akaondoka na kujipanga kwenye stendi ya Kihesa kutokana na ulemavu wake na watu kumhurumia, akafanikiwa kupanda magari ya mizigo ya usiku na kufika Morogoro usiku wa manane, akatembea taratibu kuelekea kwenye ile nyumba.
Cha kushangaza aliposogea karibu zaidi, alijikuta akivamiwa na mbwa mkubwa aliyemng抋ta na kumuumiza vibaya, isingekuwa majirani yule mbwa angemuua kabisa.
Peter alijizoazoa na kusimama akajikuta akikutana uso kwa uso na mzimu wa Jackline hapana ni Jackline mwenyewe na yule mbwa akiwa si mwingine bali ni simba.
"Mungu wangu!" akashangaa nusura ya kuzimia.

ITAENDELEA ALHAMISI
Post a Comment
Powered by Blogger.