NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA HAMSINI(50)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Erick yule dereva wakati huo aliendesha gari kwa spidi ya ajabu lakini pia alihakikisha anawasiliana na viongozi wake ambao walimtaarifu meneja wa hoteli hiyo juu ya kupatikana kwa bibi harusi mbugani.
Kila mmoja alipigwa na butwaa juu ya taarifa hizo, hata hivyo kwa busara za meneja huyo aliyependa kujulikana kwa jina lake la Kibantu, Ndimbo kuliko Saidi, aliandaa sehemu ya huduma ya kwanza kwa mgonjwa huyo ambaye alitaarifiwa kuwa yupo katika hali ya mahututi.
Ndani ya nusu saa tayari Jackline alishushwa kutoka kwenye gari na kuanza kupatiwa huduma ya kwanza, lakini bwana Ndimbo alishangaa kuwa mbali na mgonjwa Jackline pia kulikuwa na mbwa.
“Erick hii ni nini?” alifoka Ndimbo baada ya kuona mbwa akishushwa naye kama majeruhi.
“ni hadithi ndefu bosi, naomba pia tumsaidie huyu mbwa,” aliongea Erick hasa baada ya kuguswa na kitendo cha mbwa huyo kupigana na chui ili kumuokoa Jackline.
“Ifanye iwe fupi!” alisema Ndimbo kwa ukali ikabidi Erick aanze kumuelezea meneja wake jinsi tukio zima lilivyotokea na kumfanya bosi huyo aingiwe na huruma pia.
Mr. Guillemo na mkewe Leornada walishuka kutoka kwenye gari wakiwa wameshangazwa sana na tukio hilo wakaambiana.
“How could the bride happen to be alone in one of the most perilous parks in Africa? Something fishy is going on my dear,” (inawezekanaje bibi harusi akaonekana peke yake ndani ya moja ya mbuga hatari zaidi Afrika, mpenzi hapa kuna kitu kibaya kinaendelea) alisema Leornada akimwambia mumewe.
Meneja Ndimbo akasikia kwa mbali maneno hayo na kuanza kujiuliza maswali.

Meneja Ndimbo akaanza kuunganisha matukio. Hapa akakumbuka wiki moja nyuma aliwapokea maharusi waliofika hotelini kwake kwa ajili ya fungate.
Akakumbuka pia jinsi siku moja baadaye alivyopokea habari kuwa bibi na mfanyakazi wake mmoja kuuawa na simba porini. Ukiachilia hayo siku hii ya leo anaonekana bibi harusi akiwa amelowa damu chapachapa kutokea porini.
Moja kwa moja Ndimboa akahisi pengine bibi harusi huyo ndiye yule aliyeripotiwa kuuawa, akavuta subira ili Jackline arejewe na fahamu kwanza.

***
Jackline alishtuka katika moja ya vyumba vizuri, akatazama huko na huku akidhania labda alikuwa hospitali, lakini lah.
Kuamka kwake kukamfanya Bi. Leornada aliyekuwa ameketi pembeni yake akiandika jambo kwenye laptop yake kushtuka na kumfuata Jackline.
“Haloo my dear!” aliongea Bi. Leornada, Jackline akatikia; “haloo!” Bi. Leornada akaendelea kuongea maneno mengi ambayo kutokana na Kiingereza kuwa tatizo kwa Jackline akashindwa kuelewa hivyo akajikuta akijilazimisha kuongea kiingereza kibovu; “Me is speak Kiswahili.”
Kwa maneno hayo Bi. Leornada akajua kuwa binti huyo anaweza kuzungumza kiswahili tu, haraka akatoka nje, alipoingia tena ndani alikuwa na mumewe Mr. Guillemo na Erick.
“Habari yako, unaendeleaje?” aliuliza Erick baada ya kufika na kuketi karibu na Jackline aliyesheheni bandeji za majeraha hasa miguuni na mikononi.
“salama tu,” alijibu Jackline akiona aibu wazungu hao waliomkodolea macho kwa shauku.
“usiogope huyu ni Mr. Guillemo na mkewe Leornada ni watalii waliokuokoa jana ulipokuwa ukishambuliwa na chui.”
Baada ya kuambiwa maneno hayo ndipo kumbukumbu zikamrudia akatokwa na machozi huku akiwashukuru kwa maneno ya kiingereza: “thank you very much.. Mungu awabariki!”
Mr. Guillemo na mkewe wakapokea shukrani na kumtaka mgonjwa anyamaze kulia suala ambalo Jackline alilimudu.

Habari za kuamka kwa Jackline zikamfikia haraka Meneja Ndimbo, akafika na kuanza kumhoji mgonjwa huyo lakini maswali yake yote yalikuwa yakilenga kuhusianisha matukio yaliyotokea hivi karibuni.
Akaanza kuuliza jina la mgonjwa, akajibiwa; Jackline. Meneja Ndimbo haraka akashtuka na kukumbuka majina ya wale maharusi waliofika wiki iliyopita hotelini hapo.
Akakumbuka kuwa bibi harusi aliandikishwa kwa jina la Jackline. Akaendelea na maswali.
“Ilikuwaje ukafika porini ukiwa hivyo?” aliuliza Mr Ndimbo kwa maneno hayo ya UKIWA HIVYO? alimaanisha kwanza kwa vile ni mjamzito lakini jingine ni kuwa na shela.
Hapo Jackline akaanza kuelezea kila kitu kilichotokea kuanzia alivyovutishwa dawa za kulevya na baadaye kujikuta akiwa amefungwa porini.
Kitu kilichowashangaza wote ni kuhusu mbwa aliyeitwa Simba ambaye ilikuwa wazi kuwa alisafiri umbali mrefu yaani kutoka Dar hadi Mikumi, kumuokoa mwanamke huyo, katikati ya wanyama wakali.
Alipofika hapo Jackline akamkumbuka simba, akaanza kumuulizia mbwa huyo na kuambiwa kuwa anapatiwa matibabu na saa chache zijazo atakuwa katika hali yake ya kawaida.
Meneja Ndimbo baada ya kupata taarifa hiyo haraka akapanda kwenye chumba chake na kuangalia video zilizorekodiwa na mitambo ya CCTV ili kuwatazama wale wanaharusi wawili waliofika fungate.
Kitu kilichomshangaza kuliko vyote ni baada ya kugundua kuwa msichana aliyefika siku ile ndani ya gauni la harusi na kujiandikisha kwa jina la Jackline hakuwa amefanana hata kidogo na Jackline huyu, japo kuwa mwanaume wake ndiyo hasa yule aliyempa fidia.
Jambo hilo likamfanya anyanyue simu haraka na kupiga makao makuu ya polisi Morogoro kuwataarifu kilichotokea.
Ndani ya saa chache za mawasiliano ilibainika kuwa tukio hilo linahusiana na tukio la mlipuko lililotokea siku zinazoendana katika hoteli ya Udzungwa na kuunganishwa na mtu mmoja ambaye ni Peter.
Hivyo haraka, Afande Sanga akataarifiwa kumfuata hospitali Peter kwa ajili ya uangalizi na maelezo ya awali, lakini cha ajabu baada ya kufika hospitalini hapo kitanda kilikuwa kitupu, hakukuwa na uwepo wa Peter wala harufu yake. Manesi walipoulizwa hawakuonekana kujua chochote zaidi ya kunyosheana vidole.

ITAENDELEA JUMATANO

Post a Comment
Powered by Blogger.