NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA THELASINI NA TATU(33)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Yule mtu baada ya kuona Peter akiingia kwenye lile geti la kambi akamuamuru yule dereva bodaboda ageuze na kurudi walipotoka. Hapo ndipo akapiga simu kwa yule mtu aliyekuwa akizungumza naye mwanzoni akimtaarifu kuwa kweli Peter ni mwanajeshi.
Safari ya pikipiki hiyo na mtu wake wa ajabu ikaishia getini kwa Jackline.
Mtu huyo ambaye alijidhihirisha sasa kuwa ni mwanaume mwenye uso ulionyooka na macho yaliyozama ndani kidogo. Sura yake ikiashiria mtu huyo hana masihara hata kidogo, lakini akaweka tabasamu pana usoni. 
Hata alipobonyeza kengele nje ya geti la nyumbani Kwa Jackline alihakikisha anafanya hivyo kwa usahihi wake kwa lengo la kutompigia kelele mtu yeyote zaidi ya kufikisha ujumbe wake kuwa kuna mtu mlangoni ambaye anahitaji kuzungumza na mwenyeji.
“Jackline yupo?” alizungumza mtu yule akimwambia mlinzi.
“Yupo, nimwambie wewe ni nani?”
“mwambie ni dokta ,” Mlinzi kwa haraka akaingia ndani na kumwambia Jackline kuhusu mgeni huyo.
“kwani amevaajevaaje?” “anaonekana mstaarabu na mtu wa ofisini hivi,” alisema yule mlinzi.
“sawa, mwambie aingie,”
Wakati huo yule mtu akaingia ndani na akajikaribisha mwenyewe kwa kukaa kwenye kiti akitazamana uso kwa uso na Jackline.
“Jackline, unanikumbuka?” aliuliza mtu huyo.
“ndiyo,” alijibu Jackline kwa aibu baada ya kugundua huyo ni daktari wa hospitali ya Lugalo aliyekuwa akimtibia mama mkwe wake, yaani mama yake mzazi Tinonko.
Aibu iliyomfika hapo ni kuhusu kujisahau na kutomtembelea mgonjwa wake hospitali kumjulia hali kwa chochote ambapo mpaka sasa yapata mwezi mmoja.

“Najua una majukumu mengi yanayokufanya ushindwe kuhudhuria hospitali, lakini kuna jambo moja ningependa ujue,” alisema daktari huyo aliyejitambulisha kwa jina la dokta Aquinas.
“jambo lipi?” aliuliza Jackline.
“hali ya mgonjwa mpaka sasa bado siyo nzuri kabisa, wiki moja tu tangu mlipomleta hospitalini, kuna jaribio la mauaji lilifanywa na mtu ndani ya hospitali kwa mgonjwa wako.
“Tuligundua alikuwa amechomwa sindano ya sumu lakini kwa bahati nzuri tuliligundua hilo na kumpa matibabu na sasa bado yupo katika hali mbaya zaidi,” aliongea Dokta Aquinas na kuweka kituo.
“He! Nani anaweza kuwa katili kiasi hicho? “ aliuliza Jackline akishangaa taarifa hizo.
“Tulianza uchunguzi wa mtu huyo palepale hospitali na baadaye tulipoangalia kwenye kamera zetu zilikuwa zimenasa picha za mtu huyu akiingia,” aliongea Dokta Aquinas huku akitoa picha kadhaa zilizoprintiwa kwenye karatasi. Lakini hazikuwa zikimuonesha vizuri mtu huyo usoni. 
Jackline akazitazama picha zile kwa mshangao.
“anaonekana kama mtu wa kuajiriwa na suala hili limenitisha sana ndiyo maana nimeamua kuja kwako kukueleza,” alisema Dk Aquinas suala lililomuacha Jackline na maswali kibao.
Dk Aquinas akasimama na kuaga akaondoka kama alivyoingia, cha kushangaza huko nje akaingia ndani ya gari iliyopaki mkabala na nyumba ya Jackline na kuyoyoma zake.
Akiwa humo alipiga simu akimueleza mtu wa upande wa pili; “nimefika nyumbani kwake, nimezungumza naye lakini anaonekana hajui chochote, kuhusu mtu anayeishi naye.
“Ndiyo, kila kitu kinaonesha aliyefanya tukio lile si mwingine bali ni Peter…. Yah lazima kuna watu wengine anaoshirikiana nao na siyo Jackline.” Aliongea Dk Aquinas.

Giza liliingia kama kawaida na kutanda kuanzia anga la mashariki na kuelekea magharibi. Sajenti Ngowi akiwa katika chumba cha ofisi yake baada ya kumaliza kuweka hesabu ya mbwa wote na kuwachunguza afya zao, aliinua simu yake ya mkononi na kumpigia simu mkewe Bi. Magreth.
Mara nyingi hufanya hivyo, lakini pia ilikuwa ni kawaida yao asipompigia simu yeye, basi mwenzake ndiye humpigia na kuzungumzia siku zao zilivyokwenda.
Maongezi hayo pia mara nyingi hufanyika hata wakifika nyumbani, Magreth akionekana kupenda kujua mambo mengi anayoyapitia mumewe, na pindi maongezi hayo yanapoisha hujikuta wakidodosa umbea wa hapa na pale.
Hivyo basi hautashangaa kusikia kuwa hata habari za Tinonko kuzungumziwa ndani ya nyumba ya Sajenti Ngowi, ni jambo la kawaida.
Kwanza alikuwa rafiki yake mkubwa enzi hizo wakiwa mafunzoni huko Makutupora, lakini waliendelea na urafiki wao na kila mmoja akiendeleza utaalamu wake jeshini hapo na kugawana njia.
Wakati Tinonko akipanda cheo haraka na kuwa Kapteni, Ngowi alifanikiwa kuwa Sajenti, cheo ambacho japo kuwa alikuwa hapendi kubaki nacho muda mrefu, lakini alikipenda na kukitumikia vyema.
Stori ya leo kwa mkewe ilikuwa ni jinsi alivyomrudisha mbwa wa Kapteni TInonko aliyefika kimaajabuajabu kambini kwao, na lile suala la mwanajeshi mwenzao kutembea na mke wa Kapteni Tinonko muda mchache baada ya kifo chake.
Wakati akiendelea kuongea na mkewe alihisi amesikia mlango wa godauni la ofisi alizopo umefunguliwa, akakatisha maongezi na kuzuga anaendelea na kazi zake.
Kufumba na kufumbua macho, kamba nyembamba ikavishwa kuzunguka shingo yake na mikono yenye nguvu ikavuta kamba zile kwa nyuma, ikidhamiria kumtoa uhai.

ITAENDELEA JUMAMOSI
Post a Comment
Powered by Blogger.