NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA AROBAINI NA NNE(44)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.Upande wa wanandoa wapya baada ya kuoana sasa walikuwa njiani kuelekea sehemu ambapo Jackline aliamini ni fungate, lakini kutokana na gari kuendeshwa na Peter kwa kasi zaidi huku kila kona ikionekana kuingia porini na si Hotelini kama walivyopanga, Jackline akaanza kuuliza uliza maswali.
Lakini pia Peter alikuwa mjanja hakutaka kumruhusu Jackline awe na maswali kiasi hicho kwa kuwa angekwamisha mipango yake. Hapo kupitia Suzy aliyekuwa ameketi siti ya nyuma akambana Jackline kwa kumziba na kitambaa cha madawa ya kulevya puani na kumfanya apoteze fahamu.
Gari liliyoyoma na kuingia barabara ya kuelekea mbuga adhimu ya Mikumi, ikaacha barabara kuu ya kuelekea Iringa na kuingia katika barabara ya vumbi iliyochana moja kwa moja kuelekea sehemu iliyoandikwa Simba Campsite, yaani sehemu ambayo watalii huweka kambi kuwaona simba.
Kwa maana hiyo ni kwamba, sehemu hiyo ndiyo sehemu ya mbuga ya Mikumi ambayo simba hurandaranda kwa wingi na ndiyo sehemu ambayo Peter, Suzy na Jackline aliyekuwa amelala fofofo walikuwa wakielekea.
“Suzy tambua nafanya haya yote kwa ajili yako,” alisema Peter.
“Ndiyo mpenzi, sitasahau tuombee tulichopanga kiende sawa,” alisema Suzy akimtazama Jackline ambaye alionekana amekolea usingizi.
Walisimama katikati ya mbuga, Peter akashuka na kumulika kwa tochi yake huko na huku kisha yeye na Suzy wakambeba Jackline na kumshusha chini kisha wakamfunga katikati ya mti mmoja na kummwagia damu ya nyani.
Kwa mbali wakaanza kusikia sauti za mafisi na simba wakinguruma kana kwamba wanakuja kwa kasi walipo, haraka wakamuacha hapo na kugeuza gari wakielekea kilomita zaidi ya themanini kuifikia hoteli ya kitalii inayoitwa Gurunet Hotel inayopatikana ndani ya mbuga 
hiyohiyo wakati huo Suzy akachukua gauni la shela na kulivaa ndani ya gari..
“Pale una uhakika atakufa kweli?” alionekana kuuliza kwa shauku Suzy.
“Wasipomuua fisi; watumuua simba; wasipomuua simba watamuua chui, nyoka, ngiri na kila aina ya mnyama wa porini..akiwa mwenye bahati sana hataweza kupona mbele ya njaa na kiu,” alisema Peter akiwa na uhakika.
“Mh na vile alivyo na mimba, simba atafaidi!” alisema Suzy maneno ya kikatili kiasi kwamba hata Peter alijisikia vibaya.
Mpango wao hapo ni kwamba Peter aliweka oda ya fungate ya chumba kimoja kwenye hoteli hiyo, fungate hiyo ndiyo badala ya kuitumia na Jackline alikuwa amepanga muda mrefu kuitumia na Suzy baada ya kumuua Jackline kikatili porini.
Hiyo ilikuwa inamfanya Peter aweze kuwa na uwezo wa kutengeneza mpango kabambe.
Mpango huo kwanza, ulilenga kuwaaminisha wale wahudumu wa hoteli kuwa siku hiyo alikuwa hotelini na mkewe. Na pili ni kwamba alipanga yeye na Suzy mapema kesho watembelee hifadhi ya simba ambapo wakiwa huko watamuua yule msindikizaji watalii kisha mwili wake wataupeleka kule walipokuwa wamemfunga Jackline, kisha Suzy ataenda hoteli nyingine kusubiri mambo yapoe. 
Baada ya hapo Peter alipanga kufika hotelini hapo akijifanya kujeruhiwa na mnyama na kutoa taarifa ya kupotelea kwa mkewe na msindikizaji wa wataalii kule porini kisha akapanga baada ya hapo yeye na Suzy watarudi kijijjini kwa akina Jackline ili kutoa habari za kifo.
Hiyo itampa nafasi sasa ya yeye kuwa mrithi wa mali zote za mkewe na hapo ndipo pa kukomba mkwanja wote na kupotea nchini akiwa na Suzy.
Ili kutimiza mipango hiyo Suzy na Peter wakapiga magoti kwa furaha wakisema kwa pamoja; “Mungu tusaidie.”
Kisha wakakumbatiana kwa furaha na kulala unono kwa uhuru baada ya muda mrefu sana. Ilionekana kuwa walichagua sehemu nzuri ya kujificha ambayo kamwe wengi hawakuwa wakiifikiria; mbuga za wanyama.
Farudume usiku huo akapokea simu kutoka kwa vijana wake kuhusu mpango mzima ulivyoenda, akafurahi na kusubiri taratibu habari yoyote ya mlipuko itakayotokea huko Morogoro.
Salama ya akina Peter ilikuwa ni kutofungua yale maboksi mawili ya zawadi, lakini kama wakiyafungua tu basi watakutwa wakiwa mishikaki iliyoungua kabisa.
Farudume alikuwa na uhakika kila kitu kitaenda vizuri, wakati huohuo uso wake ukakunjuka akiwa anasherehekea jiwe moja kuua ndege wawili, yaani wakati mauaji ya akina Peter yatatokea maana yake na mke wa Tinonko naye atakufa hivyo kisasi chake kwa kitakuwa kimetimia nusu na bado nusu.
Akiwa katika mawazo hayo ndiyo ghafla akapokea simu kutoka kwa yule mzungu wa Kituo cha Utafiti alipomuuzaga Tinonko.
“The man has surprised us, he is cured and walking toward the source, hahaa we are watching can you join us. We are celebrating (huyu mtu ametushangaza, ameponeshwa na sasa anatembea kuelekea kwenye mali zetu. Tunasherehekea tukiangalia tukio zima njoo ujiunge nasi)” alisema Mzungu huyo jambo lililomuacha mdomo wazi Farudume.
Hiyo ni kwasababu hakutaka Tinonko apone japo kuwa alitaka afike salama na kuwaonesha mali hizo zilipofichwa ndani ya himaya ya Mbirikimo. Lakini yote yalikuwa heri kwa kuwa alitaka mali hizo azipate pia, baada ya hapo ndipo kisasi chake na Tinonko kiendelee.

ITAENDELEA ALHAMISI

Post a Comment
Powered by Blogger.