NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA AROBAINI NA MOJA(41)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Haraka akabadilisha laini na kumtumia ujumbe Peter, akaandika; ‘Tinonko amerudi.’
Peter akaipokea ile meseji kama kawaida, akaisoma na kumuita Suzy, kwa hofu aliyonayo akampigia Farudume na kumueleza yaliyotokea. Farudume akamwambia amuachie kazi hiyo yeye, alichotaka ni namba ya mtu huyo ambaye anaonekana kumkosesha amani Peter katika kipindi hicho ambacho mambo yote yalionekana kwenda sawa sawia.
Suzy akiwa hajui kabisa kuwa Peter alikuwa akiwasiliana na watu wenye madaraka makubwa kama Farudume, aliendelea kujifanya mnafiki kwa Peter, tayari alichokitaka alikipata. Peter alionekana mwenye hofu na mawazo sana juu ya mtu huyo ambaye alimtumia meseji zinazoonekana kuonesha jinsi gani anamfahamu, lakini kidogo alipata faraja baada ya kuongea na Farudume kwa kuwa siku zote hakuna jambo atakaloahidi asilitimize.
Hata hivyo aliona lazima Farudume afanye bidii kumuibua mtu huyo anayemtumia meseji hizo kwa sababu lolote ambalo linamhusu Tinonko na mkewe Jackline, pia lilikuwa likihatarisha kuvuja kwa siri yao wote.
Wakati huo, Farudume akawapigia watu wawili watatu anaowafahamu wa mitandao ya simu na kuwataarifu kuhusu namba hiyo akitaka kuijua inatokea wapi na inatumiwa na nani.
Katika chimbachimba ndipo akagundua namba hiyo imesajiliwa kwa mtu anayeitwa Pendo Omary, mwanamke mwenye miaka 23 mkazi wa Mabatini Mwanza. 
Cha kustajaabisha meseji zile zote zilionekana kutumwa kwa Peter zikitokea maeneo hayohayo ya Kihonda, Morogoro. Kwa mujibu wa mtandao ilionesha mtumiwaji na mpokeaji meseji hiyo walikuwa karibu.
Farudume akanyanyua simu yake na kumpigia Peter; “Panya yupo nyumbani kwako, chunguza kisha muondoe,” alisema Farudume kwa lugha ya kijasusi akimaanisha; “mnafiki upo karibu naye, chunguza kisha ukimgundua muue.”

Peter alijikuta akianza kuhisi anazungukwa, kwa mara ya kwanza jambo hili akaona asimwambie Suzy maana tayari alishaanza kumshuku.
Lakini pia alikuwa na sababu za kuanza kumhisi hata Jackline mwenyewe kuwa huenda alikuwa akijua mumewe ni mzima na kujua siri zake zote. Wazo hilo akalipuuzia baada ya kuona Jackline akiwa hajabadilika chochote na hata alipomchunguza aligundua hakuwa anajua chochote kuhusu Tinonko kuwa hai wala uhusiano wake na Suzy.
Akawatazama wageni waliohudhuria maandalizi ya harusi yao, wote walionekana watu kutoka mikoani wasiojua chochote kuhusu yeye. Mishale yote ilikuwa ikimuelekea Suzy.
Akaanza kumfuatilia taratibu huku kila hatua anayopiga alihakikisha anakuwa makini asije akavuruga na Jackline akafahamu ukweli.
Kwa mtindo huo siku ya pili yake wakati Peter akiwa ameketi kama kawaida yake, alipokea ujumbe kwa simu ile ile ukiwa umeandikwa; “Unajisikiaje kumuoa mwanamke ambaye ana mimba ya mtu?”
Mara baada ya kupokea meseji hiyo haraka Peter akatoka mbio kuelekea mahali alipokuwa Suzy.
Kwa upande wa Suzy baada ya kutuma meseji hiyo akatabasamu na kuzima simu akijiandaa kubadili laini yake, ghafla akamuona Peter akimkimbilia huku akihema.
Suzy akaanza kujishtukia, huenda Peter alikuwa amemgundua taratibu akaizungusha simu yake na kuificha nyuma ya kiti huku akiketi kama vile hakuna kitu kinachoendelea.
“Suzy naomba simu yako,” aliongea Peter akionekana kushindwa kuzuia ghadhabu zake.

“Simu yangu, wewe ya nini?” alisema Suzy akijichekelesha.
“Nipe simu yako sasa hivi?” aliongea kwa hasira zaidi Peter jambo lililomfanya Suzy ajishtukie akijiuliza ikiwa hatampa simu yake Peter, basi ataonekana yeye ndiye aliyekuwa akituma meseji zile.
Hivyo akafikiri haraka, pembeni yake akagundua kuna ndoo ya maji, akapiga hatua chache kuelekea upande huo, Peter akamvuta na akilenga kumzuia kuondoka popote. 
Suzy aliyekuwa na akili kama nyoka akatumia mwanya huo kuiachia simu yake ambayo ilidondoka moja kwa moja na kuingia kwenye ndoo ile ya maji.
Kesi ikabadilika na kumgeukia Peter aliyetakiwa kulipa simu ya Suzy, kwa kuwa alisababisha iingie kwenye maji. Suzy aliyaongea hayo huku akiwa hana haraka kuiokoa simu yake akihakikisha inywe maji vyakutosha ili isiwake kabisa.
Peter alishtukia kosa alilofanya akagundua pia janja ya Suzy na kuona ile siyo ajali bali alidondosha ile simu kwa makusudi kabisa ndani ya ndoo ile ya maji. Peter akaingiza mkono wake ndani ya ndoo ya maji na kuchukua simu ile na kuitoa laini na kuondoka nayo.
Wakati huo Suzy akatumbua macho kwa kuwa hakuwa ameitabiri hatua hii ya Peter.
“Simu yako nitakununulia mpya, lakini kwanza nataka nihakikishe kama laini yako siyo ile inayonitumia meseji za vitisho. Na kama nikigundua, kichwa chako halali yangu,” alipiga mkwara Peter huku akipiga hatua.
Akaiweka laini ile ndani ya simu yake na kugundua ilikuwa nzima akajitumia meseji na kushangaa ikitokea namba ileile iliyokuwa ikimsumbua. Suzy kwa kutambua kosa lake akamuwahi yeye mwenyewe.
“Sikia Peter, ukijaribu kufanya chochote nitamwambia Jackline yote, sasa nataka uwe mpole, nilikuwa nakuchemsha tu lakini kama utataka kunidhuru kivyovyote jua Jackline atajua kila kitu.” Alisema Suzy huku akitetemeka.
“Natakiwa kujua nini?” alisema Jackline aliyetokea ghafla upande ule waliokuwa Suzy na Peter.

ITAENDELEA JUMAPILI
Post a Comment
Powered by Blogger.