NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA TISA(9)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Kiukweli Jackline alikuwa amebadilika sana ule upendo wake juu ya mumewe, hakuwa nao tena huenda ni kutokana na ushawishi wa Suzy au pengine ni kutokana na mimba yake changa ilivyompeleka lakini ilishangaza kwa kuwa alitokea kumpenda Peter zaidi. 
Huyo ni mwanaume ambaye alikuwa naye hapo mwanzoni kabla ya Tino na ndiye aliyemfundisha mambo mengi sana Jackline na ndiye aliyemtoa usichana wake na kumuingiza katika ulimwengu wa mapenzi.
Lakini, mapenzi yao hayakudumu na kila mtu akawa na maisha yake japo kuwa bado wifi yake wa zamani Suzy alikuwa bado rafiki yake mkubwa hata wakati alipoolewa na Tino.
Jackline akiwa amelala chumbani kwake alianza kuvuta picha juu ya maneno aliyoambiwa na Suzy, akaona yana busara ndani yake japo kuwa kila tendo alilolisema lilikuwa limejaa ukatili. Akajishika tumbo lake lililoanza kuumuka kwa kuashiria kitoto kinakua kwa afya nzuri.
Akawaza ikiwa atarudiana na Peter, lazima mtoto wa Tino atakuwa tatizo kubwa kwenye uhusiano wake, akaona lazima afanye jambo moja yaani aitoe ile mimba, ikiwa wazazi wake watauliza atasingizia kuwa imeharibika kwa bahati mbaya.
Hata hivyo wazo hilo baya lilipata nafasi zaidi kichwani mwa Jackline kwa kuwa si mara ya kwanza kutoa mimba, alikumbuka jinsi alivyowahi kupewa ujauzito akiwa shule na mwanaume ambaye si mwingine zaidi ya Peter. Na aliyemshawishi akatoe mimba hiyo hakuwa mwingine zaidi ya Suzy huyuhuyu.

Kwa hiyo sasa unaweza ukaona Jackline alikuwa amezungukwa na watu wa aina gani.
Jackline aliamka asubuhi na mapema siku hiyo na kwenda moja kwa moja kwenye chumba cha mama mkwe wake, hiyo ni baada ya kukagua chumba kizima na kugundua hakukuwa na hati wala kadi za benki za mumewe.

Bila kuogopa kuonekana, alizama ndani ya mabegi ya mama Tino na kuanza kupekua, baadaye aligundua bahasha kubwa ya kaki, alipoikagua vizuri akagundua kulikuwa na makaratasi kadhaa yakiwemo aliyokuwa akiyataka, akayabeba na kujiandaa kutoka nje kwa furaha.
“Jack mwanangu, vipi unatafuta nini?” alisema mama Tino kwa uchovu wa maradhi akiwa hajiwezi kitandani. Badala ya kujibu Jackline alimsindikiza kwa msonyo mrefu balaa.
Suzy aliyekuwa amejiachia sebuleni kama kwake alishuhudia rafiki yake akitoka na ile bahasha mkononi, akatoa macho akimtazama Jackline.
“Ndiyo hizi hebu ziangalie, si unajua tena wewe mwenzangu umesoma,” alisema Jackline na kumpa ile bahasha Suzy akimruhusu akague karatasi moja hadi jingine.
“hee! Umezitoa wapi?” alisema Suzy.
“kwa mama yake huko ndani, tena kwenye begi,”
“si nilikwambia! Ona sasa asingekuwa anaumwa yule mama hii ingekula kwako shoga. Na hivi mwanaye amekufa ndiyo angekutimulia mbali.”
“Kweli tena nashukuru umenifumbua macho,” alisema Jackline.
Katika kupekua kwao ndani yake waligundua kulikuwa kila kitu cha Tino mali zote, akagundua kumbe alikuwa na viwanja maeneo ya Salasala, nyumba za kupangisha na zaidi alikuwa na mashamba ya migomba ya biashara mamia ya mahekari huko kwao Musoma.
Wakafurahi kwa kujipongeza, lakini ndani yake akagundua kulikuwa na karatasi ambayo iliandikwa juu mirathi. Kila mmoja wasiwasi ukamjaa.
“huyu mwanaume anaonekana kabisa alijua atakufa, hii ni karatasi ya mirathi,” alisema Suzy akimwambia Jackline.

“Twende kwenye pointi inasemaje?” aliuliza Jackline akimuamini Suzy kutokana na elimu yake kuwa kubwa zaidi yake, yaani mwenzake alikuwa amemaliza digrii ya chuo kikuu wakati Jackline alikuwa ndiyo kwanza wa darasa la saba.
“Hapa inaonekana kuwa amesema ikiwa atatangulia kufa kabla ya mama yake mzazi (kutokana na mazingira ya kazi yake) basi mali zote zitasimamiwa na mama yake mzazi.
“mali hizo zitakuwa ni haki ya mwanangu na mtoto wangu (kama atazaliwa salama) na ikiwa hatazaliwa basi mali zote zitaendelea kusimamiwa na mama yangu mzazi.
“mimi Tinonko Marato, 12 April 2010. Saini yake. Shahidi J&C Advocates, hawa J&C ni wanasheria wake,” alisema Suzy na kushusha pumzi.
“Mh kwa hiyo nikizaa mtoto, mali zinakuwa zangu, lakini asipozaliwa ndiyo zinarudi kwa mama yake si ndiyo?” aliuliza Jackline swali lililoonekana kumuuzi Suzy maana alihofia Jackline atagoma kuitoa ile mimba na kumnyima uhuru kaka yake.
“ndiyo lakini..” alibabaika Suzy.
“Sasa mimi ninaona bora nighairi kutoa mimba, naona niendelee kubaki hapahapa na maisha yangu. hayo mambo ya kudhulumiana tuyaache kwanza.” Aliongea Jackline.
“Wewe haujui mwenzako anachokupangia, si umeona hizi karatasi alikuwa nazo yeye, shauri yako mimi yangu macho, maana naona haushauriki,” alizungumza kwa hasira Suzy na kuondoka zake na kumwacha shoga yake akiwa mdomo wazi.

“Umeona?” alisema Kapteni Tinonko akiwaonesha akina Niko kitu baada ya kutembea kwa muda wa takribani wiki nzima ndani ya pori kubwa wakiwa na wale wanapiganaji wa Kimbirikimo.
Kwa hadhari kila mmoja alitulia kimya na kuchungulia kitu walichooneshwa na Kapteni Tinonko. Kwa umbali wa mita kumi walionekana watu wamevalia mavazi ya kijeshi kama wale waasi wa Ntaganda waliowaua kule Kivu. Walionekana wamepumzika na wengine kulinda doria.
Ilionekana kama vile ni kambi kubwa kuliko zote walizowahi kuziona. Kapteni Tinonko akauliza kwa mfalme wa Mbirikimo Twa, “ndiyo hapa?”
Akaitikia kwa kutingisha kichwa. Kapteni Tinonko akaagiza watulie hapo hadi giza litakapoingia ndiyo wawavamie na kuchukua kilichowaleta na si vinginevyo.
Wakati huo, Tinonko akawaita Makomando wake pembeni na kuzungumza nao; “Hii siyo vita yetu na nyie wote mnajua, lakini hatuna budi kuwasaidia hawa watu kama walivyoahidi kutusaidia sisi kurudi nyumbani salama.
“kama kweli wanasema mtoto wao ametekwa na yupo ndani ya kambi hii basi mimi moyo wangu unanituma niwasaidie, lakini sikulazimishini kwa sababu ni hatari sana na hili linaweza kutusababisha tukapoteza uhai,” alisema Kapteni Tinonko na kujitenga mbali nao.
Kuonesha walikuwa pamoja naye, wote kumi pamoja na yule rubani wao wakamfuata na kuahidi kupambana sambamba naye.
Wakati huo kijua ndiyo kilianza kufifia angani, kapteni Tinonko akachomoa darubini yake na kutazama ile kambi ya waasi, akahesabu kwa upande huo akaona wanafika takribani kumi na nne na wote walikuwa wana silaha ambazo ndiyo hasa walikuwa wakizihitaji kwa wakati huo.
Lilikuwa ni jambo la dakika chache baada ya makomando wake kutambaa kama nyoka kwenye nyasi mbichi, kipigo kiliwakuta wale waasi na bila kelele ndani ya dakika tano makomando walirudi na bunduki zilizowatosha wote na sasa wakaingia uwanja wa kivita kumuokoa huyo mtoto wa Mbirikimo. 


ITAENDELEA JUMATATO
Post a Comment
Powered by Blogger.