NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA NANE(8)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Subira ni tunu kwa mwenye subira lakini si kwa mwenye haraka zake, hiyo ndiyo hali iliyomkuta Jackline ambaye alishuhudia miezi mitatu na wiki zake zikikatika bila kusikia habari za mumewe, tetesi za shujaa huyo wa vita kuwa amefariki katika ajali ya ndege iliyotokea miezi michache nyuma zilikuwa zimetapakaa kwa kasi mno kisha akasahaulika kama upepo.
Sasa hakukuwa na habari hizo tena, kila mtu alikuwa kimya, jeshi likafanya kitu kinachoitwa kitaalamu Assumed Dead ‘Dhanio la Kifo’. Familia zao zikatakiwa zikubali kuwa wapendwa wao Wamefariki wakiwa wanaitumikia serikali.
Mama yake Tinonko hakuweza kupokea taarifa hizo moja kwa moja kwa kuwa hali yake ilikuwa taabani kwa jinsi alivyopooza, alikuwa mtu wa kufanyiwa kila kitu na Jackline.Suzy ndiye alikuwa mfutaji mkubwa wa machozi ya Jackline. 
Siku hiyo usiku wakiwa nyumbani baada ya kumaliza kumpeleka mama yake Tinonko kitandani, Suzy alimuita rafiki yake Jackline na kuanza kumueleza jambo.
“Shoga yangu nilikuwa nataka kufahamu jambo moja tu kutoka kwako, hivi umeshajipanga?” “una maanisha nini Suzy?” “Namaanisha umejipanga masuala ya mirathi au ndiyo unamuachia huyu mama,” alisema Suzy.
“Mbona sikuelewi, hayo mambo ya mirathi yanakujaje sasa?”
“Sikia wewe usiwe kama huna akili, huyo mumeo ameshakufa, na wewe hapo ulipo ni mjane, tena bado binti mdogo sana na hivi mama yake yupo wewe utaendelea kumuuguza hapa mpaka uchakae tena vizee kama vile kufa ni vigumu kweli!”

“mbona unasema hivyo vipi leo wewe Suzy!” “wewe si umekurupukia kuolewa na hawa wanajeshi, haya ona sasa kafa vitani si bora ungetulia na kaka yangu Peter mngekuwa mnayajenga sasa hivi, haya roho juujuu kila siku ndiyo nini?”
“Acha kusema hivyo Jackline, Tino alinipenda kama mke wake, huyo Peter siyo muoaji na wewe unajua!”
“Mh kaka yangu Peter ana akili siku hizi kila siku anajutia kukuacha, anatamani leo kesho mrudiane, hapa shosti yangu hauna chako naona huyo mama yake huko ndani anasubiri ujifungue umpe mtoto wakufukuzie mbali, na usipoangalia utachakaa kwa kumuuguza,” alisema Suzy wakati huo maneno kidogo yakamuingia.
“Sasa shoga yangu nitafanyaje na kama mimba ndiyo tayari nimeibeba nani atanitaka,” alisema Jackline kama vile anaanza kujutia.
“Nilishakwambia Peter anakutaka leo kesho,” alisisitiza Suzy.
“Sasa hapa nyumbani nitatokaje wewe unavyofikiria, maana marafiki zake wote wananijua,” alisema Jackline huku akimsikiliza rafiki yake kwa ushauri.
“Nani kakwambia unaondoka! Acha utoto wewe, hizi mali ni nyingi sana cha msingi zuia hati za nyumba mapema, hiki kibibi kizee kinachokaribia kujifia humo ndani kitilie hata sumu kife haraka, halafu si tuishie zetu,”
“we! Suzy hivi una akili kweli? mimi siwezi kufanya huo unyama,” Alisema Jackline.
“nani kakwambia unafanya wewe, Peter atakuja na kumaliza kila kitu, usijali,” “wewe suzy unataka kuniweka matatizoni, huyu ni mama mzazi wa Kapteni wa jeshi siyo mtu mdogo, tukigundulika si ndiyo nitaingia jela na mimba yangu,” “sikia kama vipi tutafanya hata ujanja wa kufanya kama vile mmevamiwa na majambazi, halafu ndiyo wanakomba kila kitu na huyo mama wanamuua na kuondoka zao,” alisema tena Suzy mara ghafla huko nje Simba akabweka kwa nguvu sana, Jackline akapiga kelele akimkumbusha hausiboi kumpa chakula mbwa huyo.
“na hili jibwa silipendi basi tu,”aliongea kwa ukali Jackline huku akikubaliana sawasawia na mpango wa Suzy.

ITAENDELEA JUMANNE
Post a Comment
Powered by Blogger.