NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA SITA(6)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Maandalizi ya kumpokea Kapteni Tinonko yalifanyika majira ya asubuhi, baada tu ya kuhakiki kuwa ndege ya jeshi itatua katika Uwanja wa Kimataifa wa Dar es Salaam majira ya saa 6 asubuhi kisha msafara utaelekea makao makuu ya jeshi.
Kama hali ilivyokuwa kwe jeshi la Tanzania pia Mama yake Tinonko na mkwe wake wakafanya maandalizi ya kina nyumbani huku wakisubiri masaa yaende kidogo ili wafanye hima kuelekea makao makuu ya jeshi ili kumpokea mpendwa wao. 
Simba aliyekuwa mnyonge ndani ya banda lake alihisi mabadiliko siku hiyo baada ya kuona purukushani za walezi wake, akabweka na kutikisa mkia, lakini hakuna aliyeelewa ishara hiyo zaidi kukaripiwa kila saa kuacha kupiga makelele.
***
Mapema siku hiyo katika kambi ya majeshi ya Umoja wa Mataifa Goma, makomando wa kijeshi kutoka Tanzania nao si wengine ni akina Kapteni Tinonko waliagwa kwa gwaride la heshima na kupewa nishani za kufanya kazi iliyotukuka.
Wakapanda ndege na kuacha ardhi na hatimaye kuanza kuyakata mawingu. Kila mmoja akiwa na hamu ya kurudi nyumbani kusimulia habari njema ya ujasiri walioufanya nchini Congo.
Taarifa ni kwamba walisikia huko Tanzania wameandaliwa zawadi kemkemu, wakawa na uhakika kuwa lazima wataongezewa vyeo na kupokea tunu kibao za heshima.
Kwenye hali hii ya furaha, Kapteni Tinonko aliyeketi karibu kabisa na rubani akachomoa rozali yake na kuibusu kisha akairudisha kifuani pake kama ishara ya kumshukuru Mungu wake kwa kuwaepushia madhila na inda za vita.
Lakini ghafla kulikuwa na kitu kilichowafanya wote wapige kelele kwa hofu.

Mungu wangu! ndege yao ilikuwa imetunguliwa upande mmoja, moshi mkubwa ulikuwa ukifuka upande wa bawa la kushoto na propel iligoma kabisa kuzunguka hali iliyosababisha ndege kwenda upandeupande.
Lakini cha ajabu zaidi mlipuko mkubwa ukasikika kwenye upande wa kulia na kuzima injini ya ndege ambayo ilianza kushuka chini kwa kasi. Hawakuwa na chakufikiria zaidi ya kuchukua maparashuti na kuruka chini haraka.
Ndani ya sekunde chache kikosi kizima kilikuwa hewani huku mlipuko mkubwa ukitokea mbele yao. Mungu si Athumani wakatua salama ndani ya msitu mnene, uliowameza wote.
“Kapteni, tumepoteza kila kitu ndani ya ile ndege,” alisema Japhet mmoja wa makomando.
“Kwa vyovyote, aliyetungua ndege yetu atakuwa njiani kuelekea kwenye mlipuko ili kuhakikisha kama tumekufa au lah! Felix tuna silaha gani hapa?” aliuliza Kapteni Tinonko huku akimalizia kufungua kamba ya parashuti lake.
“Mimi nina kisu kidogo na bastola, kila kitu nilikiacha kwenye ndege,” alijibu Ngamize, walipoulizana ilionekana hawakuwa na silaha kubwa yoyote zaidi ya mabomu machache ya guruneti, visu vinne na bastola mbili.
Cha kushangaza Kapteni Tinonko peke yake ndiye aliyekuwa na silaha zake zote, hii ikawa somo kwao kuwa marufuku kujiamini sehemu yoyote ndani ya uwanja wa kivita.
“Tufanye hima tuelekee kwenye mlipuko, kuokoa vitu muhimu vilivyobaki,” alisema Kapteni Tinonko kisha wote wakaondoka kwa tahadhali wakifuata uelekeo wa ule moshi kwa kupita katikati ya msitu mnene ambao unaweza ukavuta picha kukutana na kila aina ya mnyama mkali.
Baada ya takribani nusu saa waliweza kuifikia ndege yao, na kuona vifaa vyote muhimu vikiwa vimeungua vibaya. “Kapteni, hatujashambuliwa, hapa kuna mabaki ya C4 ‘bomu la kutegwa kwa dakika.’ upande wa propela ya kulia na kushoto.
Sasa ilionekana wazi kuwa bomu hilo liliwekwa kabla ya ndege kuruka; “nani aliyetufanyia udhalimu huu!” aliongea kwa hasira Kapteni Tinonko.

Ndani ya pori la Mbuti, watu wafupi jamii ya Bambega au kwa Kiswahili tumezoea kuwaita Mbirikimo walishtushwa na mlipuko mkubwa nje kidogo ya makazi yao.
Wengi katika kizazi chao hawakuwahi kuona wala kusikia jambo kama hilo. Isipokuwa mzee mmoja ambaye alikuwa akiheshimika na jamii yote ya Mbirikimo ndani ya msitu huo wenye koo zaidi ya sabini na tano.
“Tumufateni Aka- Baka, tumeingiliwa!” alizungumza kwa sauti ya wasiwasi kiongozi wa Mbirikimo hao aliyeitwa ‘Twa’. Haraka wanaume shupavu zaidi ya thelathini na saba waliungana wakiwa na zana zao za kivita ambazo ni marungu, mikuki na mishale wakatokomea kuelekea kule kulipotokea mlipuko.
Haraka wakati huohuo kundi la akina mama na watoto wao walikimbilia moja kwa moja ndani ya mapango ya maporomoko ya mto Congo kujificha huku wanaume waliobakia wakiweka ulinzi dhidi ya adui yoyote atakayetokea kuvamia ardhi yao.
Twa na walinzi wake wakaingia moja kwa moja kwenye kibanda cha Aka- Baka, mzee kati ya Mbirikimo wote wa kizazi hicho ambaye anajua mengi kuhusu ulimwengu huu na ulimwengu usioonekana.
“Npe lokoloko,” alisema Aka –Baka kwa lugha ya Kimbirikimo na kuchukua vipande vya mawe manne ya kilindi aliyoyafunga vyema ndani ya kitambaa kichafu cha rangi nyekundu na kuyatupa juu ya ubao wa Mninga.
Akashtuka kidogo na kuangalia jinsi yale mawe yalivyojipanga baada ya kudondoka juu ya ule ubao. Cha kushangaza badala ya yale mawe kudondoka kila moja upande wake kama ambavyo ni kawaida, mawe yote yalikuwa yamezonga kijiwe kimoja chekundu.

“ni mutu makubwa, amekuja kwa amani. amemaliza alichokifuata, lakini amedondoshwa hapa na Mungu wa Bambega kutuvusha kwa mkosi wa Muzungu. Huyu mmocha wao anaonekana kuzongwa na mambo matatu lakini hachui.” Alisema Aka-Baka kwa Kiswahili kibovu na kumtazama mfalme Twa, aliyetoka haraka na kuwapoza mzuka wa vita Mbirikimo wenzake ambao walikuwa wakipiga ngoma za kishujaa tayari kupambana na adui yoyote atakayeingia kwenye msitu wao. ***
Kule msituni Kapteni Tinonko alikuwa wa kwanza kugundua sauti za mtikisiko wa vichaka vya karibu na eneo walilopo. Mara ya kwanza alihisi ni wanyama wadogo lakini alipogundua alikuwa katikati ya kundi la Mbirikimo alikuwa amechelewa Kufanya chochote maana alianza kwa kusikia kitu mfano wa mwiba ukiwa umemchoma shingoni, kilichofuatia baada ya hapo ni kuishiwa nguvu na kuanguka chini kama mzoga.
Kitu cha ajabu ni kwamba, japo kuwa alikuwa anashindwa kunyanyua mkono wala mguu lakini aliweza kutazama tukio zima jinsi Mbirikimo hao waliotisha kwa mtazamo walivyowapulizia vishale na kuwadondosha makomando wake wote kama mabua ya mahindi huku nao wakiwa wazima wa akili kama yeye.
Ndani ya dakika chache walikuwa wanaburuzwa huku wakiwa wamefungwa mikono na miguu kwenye miti mikubwa kama mizoga ya wanyama.
Moja kwa moja akajua wanaelekea kuuliwa kwa kuwa habari za hao Mbirikimo zimekuwa zikisambaa kila sehemu kuwa wanakula nyama za watu. “Eeeh Mungu naomba usinifanye nife kwenye mikono ya watu hawa,” alisali kimoyomoyo Kamanda Tinonko.
ITAENDELEA JUMAPILI
Post a Comment
Powered by Blogger.