NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA TANO(5)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Wakiwa wamekaza mwendo wakawaona maadui zao wakitembea taratibu mwendo wa ushindi huku wakiimba nyimbo za ushindi kwa lugha ya Kilingala huku wakiwa na vijinga vya moto kutokana na giza la usiku. 
Hawakuweza kabisa kuwaona akina Kapteni Tinonko wakiwa wanawafuatilia kwa nyuma.Walipofika karibu zaidi, Kapteni Tinonko akanyosha mkono wake na kuonesha ishara ya ngumi, kikosi kizima kikatulia tuli. 
Akaonesha ishara ya vidole vitano na kama alama ya kuelekeza makomando wake watano waende upande wa kushoto akaonesha tena hivyo kwa upande wa kulia, makomando watano nao wakaingia msitu wa upande wa kulia.
Yeye na wale wanajeshi wawili wa Kikongo, wakatulia pale katikati, wenyewe waliita hiyo kama Amoeba Formation, yaani mtindo wa kijeshi wakuwazunguka maadui kila upande kisha wanawaweka kati na kuwashambulia.
Ghafla risasi ya kapteni Tinonko ndiyo ilikuwa ya kwanza kupasua hewa na kutua mgongoni mwa hayawani mmoja ambaye alionekana akimkokota mtoto mdogo wa kike, huenda alikuwa akielekea naye kambini kumfanya mke wake.
Baada ya risasi hiyo, iliyowashtua mahafidhina hao na kugeuka nyuma, walishangaa baada ya kujikuta wakipokea risasi kutoka upande wa kulia, kisha ukafuatia upande wa kushoto na kabla hawajafanya lolote risasi zikawaandama kutoka upande wa mbele.
Ndani ya dakika 10 za shambulio hilo la kushtukiza liliwaacha waasi wote wakiwa chini wakitapatapa ndani ya dimbwi zito la damu, ukaguzi ukaanza kuwaangalia kama kulikuwa na yeyote aliyekuwa hai.
Kwa msaada wa tochi zao walihesabu harakaharaka miili ya waasi walio ndani ya kombati za kijeshi, na kugundua walikuwa zaidi ya sabini na tatu, wanne kati yao wakiwa ni wanawake walionekana wamefungwa kamba mikononi na yule mtoto mdogo wa kike.

Waliwakagua wale wanawake na kugundua risasi zao walizilenga vyema kutowagusa hata kidogo, hivyo wakawafungulia na kuwaacha waondoke zao.
Wale wakina mama walioonekana wameshafanyiwa kila aina ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia, waliwashukuru akina Kapteni Tinonko na kutokomea gizani huku wakiomboleza kwa uchungu mno.
Si Tinonko pekee aliyejisikia huruma kwa jambo hilo, bali hata wanajeshi wenzake, hapo ndiyo unaweza kugundua kuwa katika huruma hiyo ya haki ya mnyonge kupotea, ndiyo unaweza ukaona kwa nini mwanajeshi anakuwa radhi kuua hata mabedui ishirini ili kutimiza haki ya mtu mmoja tu.
Ghafla askari mmoja aliyekuwa akikagua upande wa kaskazini mwa wale wafu akapiga makelele na kuwaita wenzake wajongee upande wake.
Kapteni Tinonko alipofika aligundua maiti ya mtu mmoja ambaye ni muasi ikiwa imefanana kabisa na mtu wanayemtafuta kwa udi na uvumba, naye si mwingine bali ni kiongozi wa waasi, Bosco Ntaganda.
Hilo likawafanya wote wajazane na kufananisha picha waliyonayo na ile maiti inayodhaniwa kuwa ni ya Ntaganda, bado kutokana na usiku ule waliona wasubiri hadi asubuhi kwa hadhari kubwa.
Ilipofika mapema alfajiri, akajitenga pembeni na kufungua simu yao ya upepo na transmitter waliyokuwa nayo na kuwapigia makao makuu Goma juu ya mtu waliyedhania ndiye Ntaganda.
Ilikuwa ni siku nyingine ya furaha kwa kikosi cha Kapteni Tinonko kwa kuwa kwa mujibu wa taarifa za makao makuu ya vikosi vya Kulinda amani huko Goma walisema wazi kuwa ndiye Temineta Ntaganda.
Kwa mujibu wa yule mwanajeshi mamluki alisema kuwa Jenerali Ntaganda na wanajeshi wake wachache walitoka jana usiku kwenye oparesheni ya kuvamia kijiji kimoja huko Kibengoma lakini hawakurudi mpaka saa hiyo hivyo ilikuwa wazi kuwa ndiye waliyemuua.
Kapteni Tinonko alijikuta akitabasamu na kupongezana na wenzake hasa baada ya kugundua kuwa wamemaliza kazi iliyowashinda makomando wa umoja wa mataifa kwa miongo mitatu wakati wao wameifanya kwa siku moja tena masaa machache tu.

Ilipofika muda fulani asubuhi walishuhudia vikosi vya serikali ya Congo DR na vile vya umoja wa Mataifa vikifika eneo la tukio na kuungana nao kila mmoja akishangaa jinsi kazi ilivyofanywa na kikosi hicho kwa muda mfupi.
Kila walipokuwa wakiitazama maiti ya Jenerali Ntaganda hakuna aliyekuwa na mashaka, hata asubuhi hiyo yule mamluki wa serikali aliyetoa taarifa jana yake alifika eneo la tukio na kuungana na wanajeshi wa serikali akidai kuwa kambi nzima ya waasi imevunjika kutokana na taarifa za kifo za kiongozi wao.
Naye alifunua maiti ya Ntaganda na kuiangalia akathibitisha kuwa ndiye yeye mwenyewe, hivyo wakaibeba na kuipandisha kwenye gari na safari ya kuelekea makao makuu ikaanza. Kila mwanajeshi hapo akawatazama na kusema lake.
Upande wa Kapteni Tinonko hakuna alichojali zaidi ya kutamani kurudi nyumbani mapema siku iliyofuatia kwa kuwa walikuwa wameshamaliza kazi waliyoifuata.
***
Siku hiyo Jackline aliyekuwa na majonzi mengi kama ndege mkiwa alishtushwa baada ya kuona simu yake ikiita, aliitazama na kuona ni namba ngeni yaani hata namba zake za mwanzo zilionekana ni za nje ya Tanzania.
Akaipokea akijua pengine ni mitandao ya simu, alishangaa baada ya kuona kumbe ilikuwa ni simu kutoka kwa mumewe, Kapteni Tino aliyeongea moja kwa moja kutokea Congo.
Hilo lilimripua moyo hata mama yake mzazi ambaye alijisikia mzima kabisa baada ya kugundua kuwa mwanaye atarejea siku moja ajayo akiwa mzima wa afya. 
ITAENDELEA JUMAMOSI
Post a Comment
Powered by Blogger.