NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA NNE(4)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Mara baada ya kupokea maagizo yake, Kapteni Tinonko alianza kuona ukubwa wa ile misheni aliyoamrishwa na mabosi zake, maana huyo Ntaganda wanayepaswa kumkamata hakuwa mtu wa mchezo hata kidogo, ni muuaji aliyekubuhu ambaye marais wa Kiafrika hasa wa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati hawakulala kwa amani kila waliposikia jina lake.
Baada ya kujua kila kitu walichotakiwa kukifanya, kesho yake waliondoka mara moja kuelekea msitu wa Virunga katikati ya Congo ambapo inasemekana kuna mambo ya ajabu sana na humo ndimo Temineta Ntaganda alikuwa amejificha.
Moja kati ya vitu vilivyomuogopesha Tinonko na wenzake zilikuwa simulizi za kuwepo kwa watu wafupi mno ndani ya msitu huo maarufu kama Mbilikimo ambao sifa yao kubwa ni kula nyama za watu.
“Safari tutaianza kesho asubuhi na mapema, kumbuka siku zote mnapokuwa uwanja wa mapambano mbali na nyumbani, hakikisha unalinda mgongo wa mwenziyo,” alisema Kapteni Tinonko.
Mbali na kikosi chake alipewa wanajeshi wawili wenyeji watakaomuongoza kuelekea msituni ambapo huko wanajiunga na mwanajeshi mwingine mamluki ambaye alipandikizwa ndani ya jeshi la waasi wa Bosco Ntaganda kwa siri kubwa.

Kwa upande wa Jackline hakuna hata siku moja iliyokuwa ikipita bila kumkumbuka mumewe Tinonko. Kwa yaliyotokea siku ya harusi yake, alitokea kuichukia mno kazi ya jeshi na kujuta kwa nini hata aliamua kuolewa na mwanajeshi.
Siku ile ya harusi alikumbuka jinsi alivyopata simanzi ya kuachwa na jinsi alivyolazimika kusimama peke yake jukwaani ambapo sherehe nzima ilipooza kwa kukosa bwana harusi.
Japokuwa zilikuwa zimepita siku mbili, kila siku aliingia kulala na kuonja joto la jiwe yaani kupigwa na baridi la wasiwasi kuwa huenda mumewe ameishauawa kwa wakati huo au ndiyo atakaribia kuuawa kwa muda mchache ujao.
Hata hivyo majuto yake yalikuwa upuuzi mbele ya mama mzazi wa Kapteni, ambaye yeye maumivu ya mwanaye kuondoka yalikuwa mara kumi zaidi yalivyokuwa kwa Jackline. Hakuwa na mtoto yoyote mwingine zaidi ya huyo na alimpenda na kumlinda kama mboni ya jicho lake.
Suala la kwenda vitani kwake lilikuwa kama kumtosa mwanaye kwenye midomo ya mamba. Hivyo basi mama huyo aliyekosa usingizi, kila kukicha alimuomba Mungu amlinde mwanaye na kujiapiza ikiwa atarudi safari hii, atamkataza kabisa kwenda tena vitani na hata kufikiria kumwachisha kazi kabisa.
Siku hiyo ndoto mbaya zilimuandama, akashtuka katikati ya usiku na kuanza kusali rozali ya mama Bikira Maria, lakini hiyo haikuweza kupoza kasi ya mapigo yake ya moyo.
Kitu mfano wa donge zito likambana, akashindwa kuhema vizuri lakini alijitahidi kuita jina la mke wa mtoto wake, Jackline ambaye naye kwa kukosa usingizi alifika haraka kumpa huduma ya kwanza ya huo ugonjwa wa presha anaoupata kila mwanaye anapoondoka nyumbani.

Kapteni Tinonko na wenzake walikuwa tayari barabarani wakiwa wamesheheni silaha za kila aina anazopaswa kuwa nazo mwanajeshi aliyekamilika huku wakiwa na vifaa vya kisasa kuanzia; patrol pack, Kurunzi, kifaa cha GPs, body armour, headset helmet na kadhalika.
Walifika karibu na tambalale za Rwindi na kupumzika, wakisubiri giza liingie kabla ya kuingia katika msitu wa Virunga ambapo huko watakutana na huyo mwanajeshi aliyepandikizwa ili kuwaelekeza sehemu alipo Temineta Ntaganda.
Walitumia muda huo kula na kulala kidogo, huku wakipokezana lindo ambapo mmoja alipaswa kuwalinda wanzake dhidi ya maadui.
Jua lilipozama juu ya msitu mnene wa Virunga, wakaanza safari yao kwa miguu, wakilazimika kuvuka mito minene yenye kila aina ya wanyama na kutokea kwenye kijiji kimoja ambacho hakikuwa mtu hata mmoja.
Mwanajeshi mmoja mwenyeji waliyeongozana naye, akawaambia kuwa katika kijiji hicho wanaume wote walikuwa wameuawa na wanajeshi wa Ntaganda.
Wanawake walibakwa na watoto wakalazimishwa kuingia ndani ya jeshi la mtu huyo katili kama;“Les petits tueurs” neno la Kifaransa lenye maana ‘wauaji wadogo’.
Kwa ukatili walioupitia watoto hawa walikuwa wakitumwa kuua na kufanya kila aina ya uchafu. Kutokana na maumbo yao madogo ilikuwa rahisi kuwalaghai watu kuwa hawana madhara lakini waliyoyafanya kwenye kijiji cha Kivu Kaskazini na Ituri, hakuna mtu hata mmoja aliyeweza kuwadharau tena.
Kapteni Tinonko alionywa kuhusu hilo, akajiandaa kisaikolojia. Wakiwa wanamaliza kupita magofu ya kile kijiji ghafla walisikia harufu kali sana, walipoenda kutazama mioyo yao ilizizima baada ya kuona mamia ya miili ya watu waliouawa ikiwa imerundikwa pamoja.
Mwanajeshi yule mwenyeji aliyetambulika kama MP Muganza aliwaambia kuwa mauaji hayo ni moja ya matukio ya kinyama ya Temineta na jeshi lake la watoto. Wakiwa katika maongezi hayo wakagundua kuwa pale chini kulikuwa na alama za nyayo za buti za kijeshi, wakagundua kuwa hao waliofanya unyama huo walikuwa wameondoka muda mchache uliopita.
Wakati wale wanajeshi wenyeji wakionekana kujaa hofu na kutamani kurudi nyuma, wakina Tinonko na wenzake walipanda morali wa vita juu ya Temineta wakakaza mwendo kuwafuatia.

ITAENDELEA IJUMAA
Post a Comment
Powered by Blogger.