NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA THELASINI NA MOJA(31)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Sajenti Ngowi haraka akaenda kuwatazama mbwa wake na kuwafungulia kwa ajili ya mazoezi ya kila siku ambayo hupewa na wataalamu wa mazoezi ambao walikuwa katika eneo maalumu la uwanja lililotengwa.
Kwa upande mwingine Simba peke yake ndiye aliyeachwa ndani ya chumba maalumu akipewa matibabu ambayo hata hivyo yalionekana kumponesha haraka vile vidonda vyake.
Nadhani hauwezi kuamini kama sajenti Ngowi alikuwa siyo makini kwa kiasi hicho hadi akaamua kumuacha Simba nje. Yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kugundua kuwa mbwa huyo ni wa Kapteni Tinonko, kitu kingine ni kwamba aligundua wanyama hao huwa na akili za ziada kiasi kwamba hutunza kumbukumbu za muda mrefu sana za wapendwa wao, hivyo suala la mbwa huyo kurudi kambini hapo lilimshtua sana Sajenti Ngowi akahisi kuna jambo linaloendelea kuhusu Tinonko.
Sajenti Ngowi anakumbuka mara kadhaa kabla ya kuja kwa mbwa huyo kambini hapo, alikuwa akiota ndoto za ajabuajabu kuhusu Tinonko, lakini mara baada ya kumpata mbwa huyo siku mbili nyuma akiwa kambini hapo, alihisi kuna kitu kinaendelea na hilo lilimfanya amfiche na kumweka nje mbwa mwingine anayefanana naye.
Yeye alifikiri huenda mbwa huyo alikuwa amevutiwa na harufu ya vitu alivyoacha Tinonko kambini hapo hadi kuingia kwenye jengo lile, akajiuliza vitu hivyo ni vipi?
Akakumbuka tena suala la Farudume kuonekana akizungushia unga kwenye banda la mbwa aliyemweka nje. Akahisi kuna jambo jingine zito zaidi ya lile alilokuwa ameliwaza ambalo linaunganisha mambo yote haya.

Mara wakati Sajenti Ngowi akiwa katika mawazo hayo ghafla akashtuka baada ya kusikia sauti ya mwanajeshi mmoja akipiga makelele kutokea uwanja wa mazoezi ya mbwa.
Alipotoka nje alishtuka baada ya kumuona yule mbwa aliyemfungia kwenye banda la nje ambaye alimwona Farudume akimzungushia unga, akiwa anakimbia hovyo huku akiwang’ata baadhi ya walimu waliokuwa uwanjani pale.
Hakukuwa na njia nyingine zaidi ya kumtuliza mbwa huyo kwa kumpiga risasi na kumuua papo hapo huku kila mmoja akihisi mbwa huyo labda alikuwa amepandwa na kichaa.
“kwa hiyo hiki ndiyo yule kiongozi alikuwa akikitaka kimtokee mbwa wa Tinonko? Mbona haya mambo siyaelewi kuna nini?” alijiuliza Sajenti Ngowi kisha akaelekea ofisini kwa mkubwa wake wa kazi, Kapteni Sesela na kumuelezea maendeleo ya yule mbwa ambaye sasa kila mtu alimjua kuwa ni wa Kapteni Tinonko.
“Mkuu, nimeshamaliza kazi, inaonekana yule mbwa yupo mzima kiafya hivyo tunaweza kumrudisha kwao,” alieleza sajenti Ngowi suala ambalo Kapteni Sesela alikubaliana nalo na kumtaka achukue usafiri na makoplo wawili wa kwenda nao. Wakati huo akatafuta kwenye makabrasha anuani ya makazi ya nyumba ya Kapteni Tinonko na kumkabidhi.

Wakati huohuo huko nyumbani Suzy, Peter na Jackline walikuwa wamerejea nyumbani kutokea hospitalini, wakatulia nyumbani na kumalizia usingizi wao hivyo nyumba nzima ikawa imetulia tuli.
Baada ya nusu saa wakiwa katikati ya usingizi kengele ya mlangoni ilisikika ikiwabugudhi Peter na Jackline waliolala zao chumbani kama mke na mume.
Suzy alionekana kulala fofofo kiasi cha kutosikia chochote, Peter akajikaza kiume na kuamka akiwa na singleti na bukta huku Jackline naye akamfuata akiwa na night dress.
akaona si vyema kumuacha Peter aende peke yake kwa kuwa si mwenyeji wa nyumba hivyo akaona watoke wote nje, yeye akatoka na night dress.
Mlinzi akamueleza Jackline kwa sauti ambayo Peter hakuisikia; “mama kuna gari ya jeshi imekuja ipo nje hapo, wamekuja na simba, unataka kuongea nao au niwaruhusu waingie?” aliuliza mlinzi.
“we vipi? Waruhusu, kwanini uwagandishe nje?” aliongea kwa hasira Jackline jambo lililomfanya Peter aliyekuwa hatua chache nyuma asogee kidogo akistaajabu kitu gani kinachoendelea.
Mlinzi harakaharaka akafungua geti, gari la jeshi likaingia ndani. Peter ambaye siku zote hakuwa akitaka Jackline ajue kazi yake ni jeshini, alitamani kujificha lakini alikuwa ameshachelewa mno.
Sajenti Ngowi alikuwa wa kwanza kumgundua Peter aliyeonekana kujificha na kutembea haraka kuelekea ndani ya nyumba.
“Koplo!” aliropoka Sajenti Ngowi suala lilomfanya Peter ageuke kwa aibu ya kuumbuka lakini kutokana na Sajenti Ngowi kuwa juu yake kicheo akalazimika kupiga saluti kwanza.
Yote haya Jackline aliyashuhudia huku akishangaa Peter anajuanaje na watu wa jeshini?
“kumbe unakaa hapa eeh!” aliuliza sajenti Ngowi kwa kuchimba zaidi.
“ndiyo mkuu aaah eeeh,” alibabaika Peter.
“kama sijakosea wewe ni mjane wa marehemu Tinonko..” aliongea Sajenti Ngowi akimuelekea Jackline ambaye alikuwa ameduwaa kwa alichokisikia.
“ndiyo mimi?” “tumemleta mbwa wako, aliingia kambini kwetu na kuleta fujo, lakini kwa bahati nzuri tuligundua kuwa ni wa Tinonko,” alisema Sajenti Ngowi huku safari hii akimtazama Peter na kugundua singleti na kaptura yake na jinsi uso ulivyojikunja ukimaanisha alitoka usingizini.
Akawaza lazima akalifuatilie suala hilo kambini.

ITAENDELEA ALHAMISI
Post a Comment
Powered by Blogger.