NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA ISHIRINI NA TISA(29)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Aliposema hivi yule mzee wa kimbirikimo akapigiza mguu wake chini pakatokea vifupa fulani kama vile ambavyo alikuwa akitumia Aka-Baka kule Congo kisha akavitupa chini.
Kwa jinsi vilivyokaa akavitazama na kucheka akamwambia Faru; “hakuna kitakachobadilika lakini fanya haya mambo haraka, ukifanya kosa lolote sasa hatutaweza kurudi nyuma.”
Farudume akaitikia kwa kichwa na mdomo akijiapiza kufuata masharti yote atakayopewa ili mradi amuone Tinonko akiwa na tabu na dhiki ya aina yake.
Yule mzee wa Kimbirikimo akacheka tena na kumpatia Farudume unga fulani wa rangi ya njano na kumtaka afike kwenye banda alilofungwa Simba na kuumwaga unga huo kisha tatizo lake na huyo mbwa litaisha.
Farudume akaipokea kwa heshima na kuondoka na gari yake aina ya Range Rover kutoka kwenye mapori usiku huo.
***
Wakati huo Jackline alikuwa amelala nyumbani kwake bila kumuona Peter wala kusikia meseji kutoka kwa mwanaume huyo kwa siku nzima. Alifikiria jinsi mchana mzima alivyompigia bila mafanikio.
Hilo lilimfanya awe na wasiwasi sana na kukosa usingizi mara kadhaa. akajifikiria kwenda kumgongea Suzy ili angalau amsaidie kumuuliza alipo kaka yake lakini aliona kama vile atamsumbua mwenzake kwa kuwa ilikuwa ni usiku mno.
Lakini mwishowe uzalendo ukamshinda akainuka kutoka pale kitandani na kwenda moja kwa moja hadi chumbani kwa Suzy, aliyekuwa hana hata lepe la usingizi wakati huo kumbe alikuwa akichati na simu.
“suzy afadhali haujalala,” aliongea Jackline na kwenda kuketi pale kitandani kwa mwenzake aliyemshangaa kulikoni Jackline akamfuata usiku huo.
“Hivi Peter uliongea naye tangu mchana wa leo?” aliuliza Jackline.

“Hapana sijampata tangu asubuhi, yaani leo nina gundu kweli maana hata yule rafiki yangu Esteria sijampata tangu asubuhi,” alizungumza Suzy akiamini ujumbe wa maneno yake umemfikia Jackline.
“Nini? Ina maana watakuwa pamoja au?” alijikuta akiropoka Jackline.
“He! We Jackline kwani una nini? Wivu gani huo wa kishamba watu hawajuani hata kidogo utawaongeleaje vibaya hivyo!” Suzy alimshushua Jackline ambaye kwa aibu na hasira aliamua kufunga mlango kwa nguvu na kurudi zake chumbani mwake.
Akilini akiwaza lazima kulikuwa na jambo linaloendelea kati ya yule msichana wa siku ile na Peter akihisi pengine Suzy atakuwa alimuunganishia kaka yake kwa msichana huyo kwa sababu kwa kuwatazama tu kwa macho Peter alionekana kuvutiwa na msichana huyo naye alionekana kama vile alikuwa akimtaka Peter.
Kila dakika ilivyoyoyoma ilikuwa ikimtesa Jackline akajikuta akiwa na mawazo kibao huku fikra zake zikimtuma kuwa Peter alikuwa amelala na msichana huyo.
Kwa uchizi wake akamfuata tena Suzy na kumng’ang’aniza ampe hiyo namba ya Esteria.
Akaipiga akashangaa kuiona inapokelewa na msichana huyo aliyeongea kwa sauti nyororo na kwa upole.
“haloow nani mwenzangu?” Bila ya kuchelewa Jackline akaanza kumporomoshea matusi msichana huyo huku akimtupia kila aina ya kashfa mrembo huyo na kumtaka akae mbali na Peter.
Esteria bila kuzungumza chochote akatulia na kucheka kidogo kisha wakati Jackline akiwa amemaliza alichokitaka na kusubiri Esteria aropoke chochote ili amtafutie sababu, Esteria kwa upole tena akamjibu Jackline; “samahani nadhani utakuwa umechanganyikiwa wewe mwanamke, nakushauri kwanza jikague unamnyima nini mume wako, halafu mpe anachokitaka ili umdhibiti asiende kwa wengine,” aliongea na kukata simu Esteria, akiwa bado hatabiriki kama kweli yupo na Peter au Lah.

Maneno hayo yalimfanya Jackline apande hasira maradufu na kuipigiza simu yake ukutani ikavunjika vipandevipande.
Wakati huo Suzy aliyekuwa akimchungulia wifi yake wa uongo akacheka kinafki na kupiga simu kwa namba ya siri akimpigia Peter na kumueleza kinachoendelea.
Peter naye akacheka na kumpongeza Suzy kwa mpango wake ulioonekana kumfanya Jackline achanganyikiwe na kujifungia ndani akiwaza maneno ya Esteria kuwa ajikague anachomnyima mumewe.
Maneno hayo yakamsumbua Jackline kiasi kwamba akaanza kujikagua mwenyewe kwenye penzi la Peter akijiuliza nini asichofanya.
Akaona kitu kikubwa pengine ni suala la yeye kumkatalia Peter kuolewa naye mapema kingine ni suala la mimba, akahisi hivyo ni vitu pekee ambavyo huenda Peter alikuwa akiona vinamnyima nafasi ndiyo maana anataka kumwacha.
Jackline akajikuta akipatwa na kizunguzungu na kudondoka ghafla chini akipoteza fahamu.
Hakuna aliyejua kilichokuwa kikiendelea hadi baada ya nusu saa ambapo Suzy alihisi ukimya wa ajabu kutoka chumbani kwa Jackline, akahisi kuna jambo.
Alipoingia ndani alishangaa kumuona jackline akiwa sakafuni, haraka akachukua simu na kumpigia Peter.
“Weee! Jacky ameanguka chini sijui amekufa! Jamani huu msala Peter nifanyeje.. nifanyeje?” aliuliza Suzy kwa kuchanganyikiwa.
“Hebu mpime kama anapumua itakuwa presha yake imeshuka lazima tumuwahishe hospitali la sivyo?” alisema Peter naye akionekana muoga kuliko.
“Anahema kwa mbali, hebu njoo haraka asije akatufia,” alisema Suzy na kukata simu.

ITAENDELEA  JUMANNE
Post a Comment
Powered by Blogger.