NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA ISHIRINI NA SABA(27)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Wakati Sajenti Omary akiinua mkwaju wake tayari kushusha mpigo wa kumi ghafla sauti ya daktari wa mbwa ambaye pia ni sajenti mmoja wapo katika kitengo hicho alifika na kuzuia adhabu hiyo isiendelee.

Hiyo ni baada ya kugundua kuwa mbwa huyo ana utofauti mkubwa na wale mbwa wengine;
“Omary hauoni huyo si mbwa wetu!” aliwaka Sajenti Ngowi na kufanya Sajenti Omary na wenzake wamsogelee na kumtazama vizuri mbwa Simba aliyekuwa hoi kwa majeraha ya bakora.
“Huyu si mbwa wetu anaonekana ametokea nje na hii haukupaswa kuwa adhabu yetu kabisa, inawahusu watu wagetini. Mtazame jinsi alivyo mnene na humuoni kama ana kola ya kawaida na si ya hapa,” alisema daktari yule na kumnusa simba.
“Ona hata shampoo anayonukia siyo ambayo tunayowaoshea mbwa wa hapa. Na wasiwasi ni mbwa wa raia wa jirani na kama atamuona mbwa wake katika hali hii lazima tutaingia matatizoni,” alisema Sajenti Ngowi kwa woga ingawa ugunduzi wake ulimfanya Sajenti Omary akimbie haraka hadi kwa Kapteni aliyefura kwa hasira.
Baada ya kumueleza yaliyotokea, Kapteni Sisele naye kwa kutaka kuepuka adhabu aliyopewa akaenda haraka kwa mkuu wake kwenye lile jengo ambalo mwanzoni aliipokea adhabu. 
Akasikia ndani sauti ya Luteni akiwa ofisini mwake. Akapiga saluti na kusimama kwa unyoofu.
“Unatatizo gani Sisele?” ilisikika sauti ya Luteni aliyeacha kuandika jambo na kuketi huku amekunja sura yake akitegemea malalamiko ya adhabu kutoka kwa Kapteni Sisele.
“Luteni, tumegundua yule mbwa si wa kwetu bali ametokea nje kabisa,” alisema Kapteni Sisele huku akiwa bado amekakamaa.

“Unasemaje?” aliuliza kwa mshangao Luteni Mshagama akasimama na kutembea na Kapteni hadi nje kuhakikisha anachoambiwa kuwa ni kweli au uongo.
Akatembea hadi kwenye yale mabanda ya wale wanyama na kumtazama simba aliyekuwa kwenye bado amefungwa barabara kwenye kibao.
“dokta, una vithibitisho gani kama mbwa huyu sio wa kwenu!” aliuliza Luteni yule sajenti Ngowi ambaye ni daktari wa wanyama hao kwa ukakamavu akamuelezea Luteni Mshagama kama alivyowaambia wale wengine mwanzoni.
Tena akampeleka kwenye hesabu ya mbwa wao na huyu alionekana kutokuwepo kwenye orodha. Hakika kwa kuangalia tu hata Luteni aliweza kuona kulikuwa na utofauti kati ya wale mbwa, hivyo akaamuru afunguliwe na kutibiwa mara moja kisha arudishwe nje alipotokea huku pia akisamehe adhabu aliyoitoa japo iliwahamia walinzi wa geti la kuingilia.
Wakati wakiwa wanashangilia ushindi wao, wote waliondoka na kumuachia sajenti Ngowi kazi ya kuhakikisha anamtibia mbwa huyo ambapo shughuli hiyo ilianza mara moja kwenye chumba maalumu.
Alianza kwa kumchoma sindano ya kupooza maumivu, kisha akamshona yale majeraha ya bakora sambamba na kumuweka dawa ya kuua bacteria na kumuandalia sehemu nzuri ya malalo.
Akiwa amembeba mbwa huyu kwa ajili ya kumlaza ndipo alipogundua baka jeupe mgongoni mwake, mbwa huyu japo kuwa alikuwa mweusi mno lakini alikuwa na rangi nyeupe mgongoni mwake.
Hilo likamfanya akumbuke jambo, haraka akatafuta kitu kwenye begi lake, akatoa simu yake ya smartphone na kuangalia moja ya picha alizoziweka mtandaoni.
Picha moja alionekana Sajenti huyo akiwa amesimama na Kapteni Tinonko enzi hizo akiwa kuruta wakiwa na mbwa mdogo mweusi. 
Picha hiyo anakumbuka aliposti kwenye mtandao miezi minne nyuma mara baada ya kupata taarifa ya kifo cha Kapteni Tinonko alipokwenda kwenye misheni ya Kongo.

Alikumbuka fika kuwa ukiacha wakubwa wake pale kazini, yeye pekee ndiye aliyekuwa na picha ya marehemu kwenye simu yake na walipiga siku wakati wanamkabidhi mbwa huyo kwa Tinonko baada ya kugundua hakuwa anaweza chochote hapo kambini.
Kilichomfanya Sajenti Ngowi awe na wasiwasi kuwa mbwa huyo ndiye yule aliyemkabidhi Tinonko ni lile baka ambalo lilikuwa limefanana mno na ramani ya Tanzania na mara kadhaa alikumbuka walivyokuwa wakibishana kuhusu ramani ile wakati Simba alipokuwa bado mdogo.
Lakini hakutaka kujipa matumaini sana kwa kuwa mbwa huweza kuzaliana na watoto kufanana na yule mbwa wa awali waliyekuwa wakimfahamu, hivyo akahisi huenda mbwa huyo alikuwa ana ukoo mmoja na mbwa yule wa Tinonko.
Safari hii akafungua tena kwenye makabrasha, ndani yake akatoa mafaili yenye picha za mbwa mbalimbali waliokuwa wakipewa mafunzo ndani ya kambi, akatafuta sana na baadaye akaona mbwa yule aliyekuwa akimtafuta.
Akaangalia upande wa jina lake na kuona limeandikwa simba, akakumbuka sasa kuwa kweli mbwa yule waliyempa Tinonko alikuwa akiitwa simba. Akaona njia pekee ya kuhakikisha kuwa mbwa yule ni simba au lah ni kumuita kwa jina lake.
“Simba!” aliita sajenti Ngowi.
Yule mbwa akafumbua macho yake na kubweka sauti ya maumivu, hapo moja kwa moja Sajenti Ngowi akahitimisha uchunguzi wake. Akainuka haraka kwenda kuwaambia wenzake alichokigundua.
Siku iliyofuatia taarifa zilikuwa zimekwisha enea kambi nzima kuwa mbwa wa marehemu, shujaa Tinonko amerudi kambini, taarifa hizo zikafika kwenye masikio ya mtu ambaye naye alionekana katikati ya wanajeshi wenzake mtu huyo si mwingine bali alikuwa ni Peter. Peter huyuhuyu aliyekuwa akimuandama Jackline kwa kivuli cha penzi.

ITAENDELEA JUMAPILI
Post a Comment
Powered by Blogger.