NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA ISHIRINI NA SITA(26)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Siku hiyo kama kawaida, Jackline na Peter walipanda taksi ya kukodi na kwenda moja kwa moja kwa daktari mchoropoaji, Jackline alijua hatari ya kutoa mimba kubwa kama yake hivyo akaweka sharti kuwa lazima shughuli hiyo ifanyike kwenye hospitali kubwa ili kama akizidiwa iwe rahisi kufanyiwa matibabu.
Peter naye hakutaka kitu kibaya kimtokee Jackline kwa sasa, lazima kwanza mipango yake itimie kabla ya kuruhusu kifo kimtokee Jackline, hivyo akafanya anavyoweza kutafuta hospitali kubwa ya kufanya walichokitaka na ndiyo huko Tandika.
Walifika na kuonana na daktari wake aliyemueleza kwanza nini anachotakiwa kufanya, hakika hela ni mwanaharamu. Kama kawaida daktari alichukua vipimo vya ultra sound kuangalia hali ya mtoto tumboni. Mtoto akaonekana ni mwenye afya na hakuna tatizo litakalozuia mimba isichomoke.
Daktari huyo mzoefu akamchoma sindano ya ganzi, Jackline aliyelala kitandani akisubiri mikasi imuingie. Huko nje Peter alikuwa makini kuangalia huku na huko ikiwa mbwa wa maajabu atatokea na kuzuia walichopanga kitokee, safari hii alikuwa amejipanga vilivyo.
Huko ndani wakati Daktari akiwa anaanza kufanya yake, ghafla akashtukia Jackline akitokwa na jasho jingi. Akaacha mara moja kufanya alichokuwa akikifanya na kuchukua kifaa cha kupima presha ambacho mtu hufungwa kwenye mkono kwa kumbana. Akagundua mgonjwa wake presha yake imeshuka kwa kiasi kikubwa hivyo akahofia ikiwa atamtoa mimba basi kuna uwezekano mkubwa wa kumhatarishia maisha yake.
Kwa hofu akampatia huduma ya kwanza na kujaribu kumpa muda wa nusu saa wa mapumziko huku Peter aliyeketi nje akisubiria ushindi, akivunjika moyo baada ya yule daktari kumueleza kilichotokea.
“Tusubiri kwanza, akikaa sawa jaribu tena. Ni muhimu sana hiyo mimba ikitoka bila yeye kuathirika kwa chochote kile,” alisema Peter.
Yule daktari ambaye alionekana kuijua vilivyo kazi yake akarejea ndani kuangalia maendeleo ya mgonjwa wake.

Kama alivyotarajia, daktari alimuona Jackline akiwa kwenye hali ya kawaida, akamueleza kilichotokea lakini Jackline kwa kuhofia kumuudhi Peter akamuomba daktari aendelee kumtoa akiahidi kutoruhusu presha ishuke tena.
Daktari kama kawaida akaanza kwa kumchoma tena sindano ya ganzi na kusubiri dakika kadhaa akisubiri imkolee. Akachukua mikasi yake lakini kwa mara nyingine Jackline akaanza kutokwa jasho jingi sana zaidi ya mwanzoni huku mwili wake ukionekana kukosa nguvu. Hata pale Dokta alipomuita kwa kumtingisha alionekana kulegea kama vile anakaribia kufa.
Kwa wasiwasi akamuacha, tena safari hii akahakikisha harudii kosa ambalo litaweza kumfanya mgonjwa wake apate madhara. Akaenda moja kwa moja kwa Peter na kumueleza nini kilichotokea. Mara ya kwanza hakuamini lakini baadaye alijikuta akikubali matokeo na kukubali kurudi nyumbani na Jackline ambaye hali yake bado ilikuwa si imara.
Suzy akiwa na furaha ya kujua pengine zoezi hilo lilikuwa limeisha, alijipa jibu mwenyewe kwa kuwatazama tu usoni wakina Peter, jibu alilolipata ni kwamba, lazima kutakuwa na tatizo hivyo akatulia tuli akisikilizia kulikoni?
Waliingia ndani na kutulia sebuleni ghafla Jackline akagundua msichana mrembo mno aliyevalia kimini akiwa amekaa kwa adabu kwenye kiti, Macho yake, umbo lake na hata rangi yake alionekana wazi kuwa na asili ya Kinyarwanda.
Alikuwa mzuri kiasi kwamba hata mtu angemtazama akiwa kwenye spidi ya gari angegundua uzuri wa msichana huyo kiasi cha kumfanya arudishe gari yake nyuma na angalau kumsalimia.
Haraka Suzy akawahi na kuwatambulisha; “Jackline na Peter huyu ni rafiki yangu anaitwa Asteria nilisoma naye chuo UDOM, amekuja kunitembelea mara moja… Asteria huyu ni kaka angu Peter na huyu ni mpenzi wake anaitwa Jackline.”

Haraka Peter akajua kuwa huyo ndiye msichana aliyeambiwa na Suzy atakuja kwa ajili ya kumtetemesha, Jackline akajikuta akicheka kimoyomoyo na kumpongeza Suzy kwa ujanja wake maana kwa uzuri wa yule msichana hakuna mke wa mtu atakayependa hata amsogelee mumewe.
“Asante nafurahi kuwajua,” aliongea Asteria huku akiinuka na kumsalimia kwa kumshika mkono Peter na kumuachia tabasamu pana kisha akaja kwa Jackline huku kwa kuinuka kwake kukalifanya umbo lake maridhawa lililofanana na shepu ya Wema Sepetu lionekane wazi.
Jackline akionesha chuki yake wazi akagoma kutoa mkono wake kitendo kilichomfanya Asteria arudi na kuketi akijua fika kazi yake itakuwa rahisi mno.
“Mh, hongera kaka Peter naona tayari kijacho, mmetoka Klinik nini?” alijizungumzisha Asteria huku akiruhusu sauti yake mwanana ipenye katikati ya mwanya wake mwembamba ulioonekana vyema kushabihisha lengo la kauli yake ya kichokozi.
“Aahh! Hapana ni…Ooh ndiyo tumetoka hospitali,” alibabaika Peter.
“Sasa jamani wakati mnaingia mimi ndiyo nilikuwa naaga hapa , nadhani tutaonana siku nyingine.. kwa heri wifi,” aliongea Asteria na kuinuka akaligeuzia jishepu lake upande wa Peter tena akaongeza uchokozi kwa kuinama akijifanya anachukua simu yake pale kwenye kochi.
“oh lakini mbona mapema hivyo,” aliuliza Peter akionesha kumhusudu vilivyo msichana huyo.
“kaka bwana, mbona nilikuwepo tangu asubuhi?”
“oh sawa lakini karibu sana jisikie nyumbani,”
“mimi tena. Utanichoka wewe maana nimehamia hapo nyumba ya pili tu,” alisema Asteria kauli ambayo ilizidi kumrusha roho Jackline kiasi kwamba mgeni huyo alipoondoka tu huko nyuma moto ukawaka.
Eti kisa ni kwa nini Peter kamchangamkia yule msichana. Peter alimshangaa mpenzi wake kwa kulalamikia wivu wa kipuuzi suala lililomfanya Jackline ajishtukie na kukaa kimya.
Mpango wa Suzy umeanza kufanikiwa lakini Je, watafanikiwa kumfanya Jackline afanye kama wanavyotaka?


ITAENDELEA JUMAMOSI
Post a Comment
Powered by Blogger.