NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA ISHIRINI NA TATU(23)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


 • Ilikuwa ni simu ya Peter ndiyo iliyovunja ukimya kati ya Suzy aliyekuwa akiugulia maumivu ya kidonda chake na Jackline aliyekuwa akiisikilizia ganzi inayoisha taratibu kutoka katika mwili wake.
  Haraka Suzy akaipokea ile simu na kuongea bila kumeza mate; “Kaka lile limbwa si nilikwambia lina matatizo, sasa hapa limetoa kali ya mwaka maana limetufata hadi tulipokuwa hospitali na kutushambulia, hapa ninavyoongea limening’ata mguu!”
  Inawezekana Peter hakuwa ameamini maneno ya Suzy, ndiyo maana alitaka kuongea na Jackline, Suzy akampa simu yake Jackline naye akaanza kuendeleza kipande cha stori yake.
  “Mimi sijui, lakini nilisikia mbwa akibweka mle ndani ya zahanati na pale nje kila mtu alikuwa akikimbia na kupiga makelele kuwa amemwona mbwa, ila uhakika kabisa kama ni huyu simba wangu mimi sijui,” alisema Jackline.
  “kwa hiyo imeshindikana kutoa?” aliuliza Peter jibu akiwa tayari ameshalijua. “ndiyo, sasa ulitegemea nini!” alijibu Jackline kwa ukali, ikabidi Peter ajishushe na kumbembeleza Jacky na wakayamaliza.
  Peter wakati huo alikuwa ameanza kupata wasiwasi kuhusu yule mbwa, iweje awe mkali sana kwao? Akahisi kuna jambo linaloendelea japo kuwa hakutaka kumwambia bosi wao Faru Dume kuwa kikwazo cha yeye kutofanikiwa kumtoa mimba, Jackline siku hiyo kumetokana na mbwa.
  Akaona wenzake watamcheka na kumchukulia mtu asiye na akili timamu, hivyo akatulia kimya na kutaka kufanya uchunguzi kuhusu mbwa yule kimyakimya huku akijiapiza kuwa ikibidi lazima amuue.

 • Kapteni Tinonko akiwa ndani ya chumba cha mateso, mwili wake ukiwa na majeraha na vimbe zilizovilia damu kila sehemu, alikuwa nusu mfu nusu hai.
  Lile zoezi la kujisahaulisha maumivu kwa kuvuta taswira nzuri za maisha aliyokuwa nayo hapo awali, lilishindikana. Na badala yake alizidi kujiongezea maumivu kwa kukumbuka mabaya yanayomkabili.
  Alimfikiria mama yake mzazi aliyekuwa kwenye kitanda cha umauti, bila ya yeye kufanya chochote, akamfikiria mke wake ambaye ndani ya miezi michache alikuwa ameshampata mbadala wake, haya yote yaliongeza machungu yasiyoelezeka.
  “Mungu wangu, nimekosea wapi?” alijiuliza na kupoteza fahamu kwa dakika kadhaa. 
  Akiwa ndani ya dimbwi la machungu, ghafla alishangaa kuona wanajeshi wa kawaida wanaingia kwenye chumba kile alichomo tofauti na wale wa mateso aliowazoea. Wakamchukua katika udhaifu wake na kumpeleka kwenye chumba kingine, humo kulikuwa na bafu, na mazingira mazuri ya kulala.
  Humo akashangaa akipewa chakula kizuri na hata matibabu lakini wanajeshi wale walikuwa hawamsemeshi chochote.
  Hivyo hakujua nini walichompangia pengine akadhani huenda walikuwa wamegundua hakuwa na hatia kati ya madai yote waliyomwambia hapo awali.
  Lakini bado alipata wasiwasi akahisi pengine kuna jambo kubwa zaidi litakalomkabili kwa kuwa mpaka siku hiyo bado hakuwa amekutana na Luteni wala Mkuu wa majeshi watu ambao wangekuwa wa kwanza kabisa kumfuata kutokana na makosa makubwa aliyodaiwa kuyafanya kwa sababu pia ndiyo wao walioidhinisha ile oparesheni ya Congo ya yeye kuondoka na wale makomando wenzake kumi.
 • Jioni ya siku hiyo Peter alionekana akiwa na wenzake wanne katika mkutano wa siri ndani ya chumba kidogo. Wote walionekana kuwa na wasiwasi wakiwa wanamsubiri mtu mmoja ambaye ndiye anayejulikana kwa jina la Farudume.
  Ndani ya dakika chache, mlango wa chumba hicho ulifunguliwa na jitu lenye miraba minne na sura kama katuni za kutisha zinazochorwaga likatokea.
  Jitu hili lilipoingia ule ukimya waliokuwa nao wakina Peter hapo awali ukazidi mara tatu yake kiasi cha mtu kusikia hata mshale wa saa unapogonga kuashiria sekunde mpya au hata mapigo ya moyo na pumzi za hofu zilizokuwa zikivutwa na kutolewa kwenye miazi ya pua zao.
  Farudume akaketi katikati yao, yeye akiwa na simu yake mezani na bastola yake aina ya Revolver akaiweka juu ya meza na kuwatazama, Peter na wale wenzake waliohisi lazima atakufa mtu siku hiyo.
  “Richard, nilikutuma umchome sindano yule mama pale hospitalini ili afe taratibu. nimeona tena umefanya vizuri sana,” alizungumza Farudume kwa sauti lake zito.
  “Ali, Goodluck na Zacharia, niliwatuma mhakikishe mnamtesa Tinonko kiasi cha kutosha pindi alivyokuwa mle selo, mmefanya hivyo zawadi yenu ipo,” akaongeza Farudume kisha akamgeukia Peter huku amekunja sura lake baya.
  “Peter, wakati wenzako nimewatuma kazi za hatari na wamefanya, wewe nilikutuma kitu rahisi sana, nilitaka umtoe mimba yule binti na umuoe na vyote havijafanyika, mpaka sasa.”
  Wakati akiongea hivyo Farudume akachukua ile bastola yake na kuiweka risasi moja kisha akaikoki na kuizungusha ile revolver kisha akamuelekezea Peter aliyekuwa akilia kwa uchungu akimuomba Farudume ampe siku mbili tu kutimiza kazi yake.
  Alijua mtu huyo katili hakuwa na mzaha na alishawaua wengi walioshindwa kutekeleza maagizo yake, siku hiyo alijua ni zamu yake maana Farudume akimnyooshea mtu risasi hairudishi mkono hadi awe amefyatua. Basi akavuta kidole chake na kufyatua.

ITAEDELEA JUMATANO

Post a Comment
Powered by Blogger.